
Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe
akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu msimamo wao wa kutorudi
bungeni kujadili Rasimu ya Katiba Mpya. Wengine ni wenyeviti wenza wa
umoja huo, Profesa Ibrahim Lipumba (kulia) na James Mbatia. Picha na
Michael Matemanga
----
. Joto la Katiba Mpya linazidi kupanda nchini,
huku baadhi ya wasomi na makundi mbalimbali ya watu wakizidi kutilia
shaka utapatikanaji wa Katiba hiyo.
Mkurugenzi wa Shule ya Sheria ya Kenya (KSL),
Profesa Patrick Lumumba na mwandishi wa habari mkongwe nchini, Jenerali
Ulimwengu wameonya kwamba kwa hali ilivyo hivi sasa hakuna Katiba Mpya
inayoweza kupatikana.
Wakizungumza katika mdahalo uliohusu mivutano ya
makundi katika mchakato wa Katiba Mpya jana jijini Dar es Salaam,
walisema kuwa CCM haikuwa na nia njema tangu mwanzo, huku Rais Jakaya
Kikwete akitajwa kushindwa kusimamia ipasavyo.
Profesa Lumumba alisema Katiba ya Tanzania imejaa
viraka na kwamba inahitajika Katiba Mpya ambayo itakidhi matakwa ya
Watanzania na karne ya 21, itakayokwenda sambamba na changamoto za
Afrika Mashariki.
Alisema nchi za Afrika Mashariki zilipata katiba
zao kwa njia ya machafuko, hivyo Tanzania lazima itafute njia sahihi
inayokubalika kwa wananchi wote bila ya kuwepo kwa kundi moja linalotaka
kuhodhi mchakato wa Katiba Mpya.
“Tanzania ina nafasi ya pekee na kihistoria
kujipatia Katiba Mpya bila vita na itakuwa ni jambo la kusikitisha ikiwa
kwa mtazamo finyu ya kivyama utanyimwa na wanasiasa ambao fikra zao si
za kukidhi matakwa ya katiba,” alisema Profesa Lumumba.
Alieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete amekiri kuwa
alifanya makosa katika kusimamia mchakato wa Katiba Mpya, hivyo
Watanzania wanapaswa wamsamehe ili mambo yaende sawa.
“Nimesikiliza hotuba za Rais (Jakaya Kikwete)
alikubali kwamba alikosea, tukumbuke Rais wa nchi hawezi akaja akapiga
magoti, cheo chake cha rais hakikubali hivyo, akisema alitoa maoni kama
mwananchi kile ambacho anasema ni kwamba nisameheni,” alisema huku
akishangiliwa na wajumbe ukumbini. Aliongeza kuwa iwapo Watanzania
watataka Rais afanye jambo la ziada kuliko hilo alilofanya watashusha
hadhi ya kiongozi huyo wa nchi.
Alisema Watanzania walipotunga sheria ya kufanya
marekebisho ya katiba walifanya dhambi mbili za asili. Alizitaja dhambi
hizo kuwa ni kuruhusu kuyataja baadhi ya mambo kwenye katiba kuwa ni
matakatifu na kuvunja tume ya mabadiliko ya katiba.
“Mkiwa mnazungumzia mambo ya katiba hakuna mambo
matakatifu yote lazima yazungumziwe. Tanzania siyo nchi ya kwanza Afrika
Mashariki kutafuta katiba ni nchi ya mwisho,” alisema huku
akishangiliwa na wajumbe wa kongamano hilo.
Akiizungumzia dhambi ya pili alisema: “Lakini jambo ambalo
halieleweki na wengi ni kwa nini Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Jaji
Warioba (Joseph) iliyokuwa na uzoefu ikavunjwa ? Katika mataifa yote
unaihifadhi tume mpaka mwisho.”
Alisema tume hiyo ilitekeleza kazi yake kwa
kiwango kikubwa na kwamba hakuna nchi Afrika iliyowahi kukusanya maoni
kutoka kwa kila mwananchi.Kwa habari zaidi Bofya na Endelea......




0 comments:
Post a Comment