;

Rais Jakaya Kikwete ameikataa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel
Bendera kuhusu waathirika wa mafuriko na waliokosa makazi na kumpa siku
moja kukaa na timu yake kuandaa nyingine inayoendana na
hali halisi ya janga hilo.
hali halisi ya janga hilo.
Eneo la Dumila, Morogoro lilikumbwa na mafuriko makubwa na kusababisha
wakazi wake kupoteza makazi na mali huku mamia ya magari yakiwamo mabasi
yanayosafirisha abiria kukwama baada ya kubomoka kwa Daraja la Magole
linalounganisha Barabara ya Dar es Salaam na Dodoma.
Mvua hizo zilizonyesha kwenye Wilaya ya Kilosa, ndizo zilisababisha kufurika kwa Mto Mkundi unaopita kwenye eneo hilo.
Taarifa ya Bendera
Bendera alitoa taarifa ya mafuriko kwa Rais Kikwete kwa niaba ya
viongozi wa mkoa, wakiwamo wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa
taasisi mbalimbali akisema wananchi 12,472 wamepoteza makazi. Alisema
pia kuwa nyumba 1,141 zilibomoka na 2,551 ziliingiliwa na maji huku kaya
2,759 zikiathiriwa na mafuriko. Bendera alisema misaada ya mahema na
vyakula imeanza kutolewa pamoja na dawa za kukabiliana milipuko ya
magonjwa endapo itatokea.
Alisema pia kuwa tayari baadhi ya miundombinu imeanza kurejea kama
kawaida huku huduma za majisafi zikitolewa na magari ya Jeshi la Ulinzi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha Zimamoto Morogoro na Kampuni
ya China ya High Quality Consulting and Development Solutions. Bendera
alisema pia kuwa jumla ya Sh53.7milioni zinahitajika kwa ajili ya ujenzi
wa makazi ya muda ya waathirika hao.
JK aikataa taarifa
Rais Kikwete aliyekuwa akikatizakatiza taarifa hiyo ya Bendera kwa
maswali na ufafanuzi, alizikataa takwimu hizo akisema hazionyeshi
uhalisia. Akizungumza na wananchi wa eneo hilo wakiwamo waliokuwa kwenye
kambi iliyoko Sekondari ya Magole, Rais Kikwete aliwahakikishia
upatikanaji wa vyakula, dawa na majisafi na salama.
Pia aliviagiza viwanda vya magodoro kuzisaidia haraka iwezekanavyo,
familia zilizoathirika na kuahidi kuwa Serikali italipa baadaye ili
kuwaepusha wakazi hao na hasa watoto na athari za kiafya.
Alisema kazi ya ujenzi wa makazi ya muda itafanywa JWTZ na si
makandarasi kuepusha baadhi ya viongozi kujinufaisha kwa mafuriko hayo.
Rais Kikwete aliwataka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuangalia
uwezekano wa kutoa magogo yaliyoziba katika makaravati na kuzibua
mifereji ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi.
Akizungumzia ripoti hiyo Rais Kikwete alisema: “Mmeshindwa kufafanua
watu walioathiriwa na mafuriko hayo ni wangapi na wanasaidiwa vipi hasa
katika mahitaji mbalimbali na muhimu ya kimsingi kama chakula.
“Taarifa yenu inanitia shaka. Sasa ninawataka viongozi wa mkoa pamoja na
Mkuu wa Mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote wa halmashauri
kurudia upya kumbukumbu zenu na kupata idadi kamili ya waathirika ili
kujua namna ya kuwasaidia. “Ninyi kama viongozi na mnashughulikia maisha
ya watu, mnatakiwa kuwa na kumbukumbu zenye usahihi wa majina na kama
hamna uhakika wa majina mnaomba vyakula kwa ajili ya nani? Misaada
mingine kwa wahisani ya nini?
MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment