James Kisaka enzi za uhai wake.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa kocha wa makipa wa
Simba, James Kisaka (57) kilichotokea leo asubuhi (Desemba 25 mwaka huu)
katika Hospitali ya Burhani, Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika familia ya
mpira wa miguu kwani Kisaka kabla ya kuwa kocha alikuwa mchezaji katika
nafasi ya kipa. Mbali ya Simba, timu nyingine alizowahi kudakia ni Ndovu
ya Arusha, Volcano ya Kenya na Small Simba ya Zanzibar.
Akiwa mwanafunzi Shule ya Sekondari
Tambaza jijini Dar es Salaam aliwahi kuchezea timu za Oysterbay Stars,
Eleven Stars ya Msasani, Sigara wakati ikicheza Ligi ya Temeke na Nyota
Nyekundu kabla ya kutua Simba.
Pia alikuwemo kwenye timu ya Taifa ya
vijana iliyokwenda Zimbabwe kwenye sherehe za uhuru wan chi hiyo mwaka
1980. Vilevile alikuwa mmoja wa wachezaji waliounda kombaini ya Tanzania
ya UMISSETA akiwa na akina Said George, Nico Njohole, George Kulagwa na
wengine. Hivyo mchango wake katika mchezo huu tutaukumbuka daima.(P.T)
Kwa mujibu wa kaka wa marehemu, Benny
Kisaka, James alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa miguu kufa ganzi na
matatizo ya kutoona vizuri.
Msiba uko nyumbani kwake Mbezi Mwisho (Kwa Yusuf), na anatarajia kuzikwa nyumbani kwao Kijiji cha Lusanga, Muheza mkoani Tanga.
TFF tunatoa pole kwa familia ya
marehemu Kisaka, klabu ya Simba na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar
es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi
hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Marehemu Kisaka ameacha mjane na watoto wanne. Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
CHANZO: MJENGWA BLOG
0 comments:
Post a Comment