SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, September 20, 2013

MAKALA YA ULINZI SHIRIKISHI KATIKA MICHEZO MKOA WA MBEYA.

 
 [DIWANI ATHUMANI – ACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.


 Katika maisha ya kila siku ya binadamu suala la ulinzi na usalama wa mali na maisha ni muhimu sana. Binadamu huishi kwa kutegemeana basi ndivyo ilivyo hata katika suala la ulinzi wa mali na maisha yetu. Unaweza kujiuliza je,ni nani mwenye jukumu la ulinzi?je,ni mimi au wewe? Au ni sisi sote.
Basi katika miaka ya hivi karibuni Jeshi la Polisi Nchini limeendeleza dhana ya ulinzi shirikishi na ulinzi jirani kwa lengo la kushirikisha jamii kwa karibu zaidi katika suala zima la ulinzi na usalama. Zana hii imekuwa ikitoa fursa kwa jamii na wadau mbalimbali kutoa taarifa za kuzuia uharifu hali inayofanikisha kudhibiti vitendo hivyo.
Ni wazi kabisa kuwa kila mmoja wetu ana jukumu la kushiriki katika ulinzi.Ushirikishwaji huu wa wananchi katika kuzuia na kudhibiti vitendo vya uharifu ni mpana zaidi, kwani vitendo vya uvunjifu wa amani na utovu wa nidhamu si vya kuvumilika katika jamii. Kila mmoja wetu anapaswa kujua nini cha kufanya pale anapoona vitendo ambavyo si vya kiungwana vikitendeka.
Katika siku za hivi karibuni hususani  katika mechi za ligi kuu Tanzania bara kumekuwa kukitokea vitendo ambavyo si vya kiungwana wala kinidhamu katika mchezo wa mpira wa miguu. Vurugu mbalimbali kutoka mashabiki wa timu zinazoshiriki ligi kuu zimevuka mipaka kwani imefikia hatua hata ya kurushiana mawe.Katika mechi ya hivi karibuni kati ya Mbeya City dhidi ya Yanga mechi iliyofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine kulitokea vitendo visivyo vya kiungwana katika medani ya michezo.
Ikumbukwe kuwa suala la ulinzi katika sehemu mbalimbali ni jukumu letu sote. Kila mmoja wetu awe mlinzi wa mwenzake katika kuhakikisha amani na utulivu vinachukua nafasi yake katika michezo ili kwa ujumla wananchi wapate burudani.
Vurugu na vitendo visivyo vya kimichezo vina athari kubwa si tu kwa timu bali hata kwa mashabiki na wananchi wa mkoa husika kwani inapotokea timu kufungiwa kutofanya michezo yake katika uwanja wa nyumbani ni athari hata katika shughuli za kiuchumi pamoja na kuua mapato ya mlangoni. Pia vurugu kama hizi ni athari pia katika shughuli za uwekezaji na kuzuia upatikanaji wa fursa ya ajira kwa wananchi.
Yapo mapendekezo mbalimbali ya wananchi juu ya suala hili la kudhibiti vurugu katika michezo. Itambulike kuwa ni suala la kila mwananchi kwani kama kila mmoja wetu ataona umuhimu wa kutoa taarifa pale anapotilia mashaka mtu/watu kwa vyombo vya ulinzi na usalama, basi suala hili tunao uwezo wa kulidhibiti na kulimaliza kabisa.Kila mwananchi atoe ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kufanikisha kudhibiti na kutokomeza vitendo vya vurugu uwanjani na katika michezo kwa ujumla.
Pengine kwa sasa ni muda muafaka kwa uongozi wa timu pamoja na shirikisho la soka nchini ni kuliangalia suala hili kwa kina zaidi ili kujiepusha na madhara makubwa zaidi. Kuwepo na adhabu kali zaidi kwa timu itakayo shindwa kuwadhibiti mashabiki wake dhidi ya vitendo visivyo vya kimichezo.
Ni imani yangu kuwa kila mwanamichezo na wadau wote wa michezo watashiriki kikamilifu kuzuia na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pale waonapo dalili za vurugu kutoka kwa mtu au  kikundi cha watu kikipanga njama za uvunjifu wa amani katika michezo hasa mechi za ligi kuu zinazoendelea.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Kamishina msaidizi, DIWANI ATHUMANI anawakumbusha mashabiki na wadau wote wa michezo kuwa “michezo ni uchumi, michezo ni burudani, michezo ni upendo/amani na kila mmoja wetu aone kuwa ana kila sababu ya kutekeleza hili”

Imetolewa na:
[DIWANI ATHUMANI – ACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

CHANZO: MBEYA YETU BOG

0 comments:

Post a Comment