SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Monday, July 16, 2012

MWANAFUNZI WA MAREKANI ATOA ZAIDI YA MILIONI 30 KUSAIDIA UCHIMBAJI KISIMA SINGIDA.


Mtambo wa kuchimba visima ukichimba kisima cha maji  cha kijiji cha Sekoture jimbo la Singida Kaskazini.
Mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini Mh. Lazaro Nyalandu akiwa na mke wake Faraja Kota, muda mfupi baada ya kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Sekoture.
Mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini Mh. Lazaro Nyalandu akiwa kwenye picha ya pamoja na mwanafunzi Leah Singer (katikati) kutoka Marekani aliyetoa msaada wa shilingi milioni 30 za kugharamia uchimbaji wa kisima cha kijiji cha Sekoture. Wa kwanza kulia ni mke wa Nyalandu Faraja Kota.
Mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Lazaro Nyalandu akikagua uchimbaji wa kisima cha maji cha kijiji cha Sekuture kata ya Ilongero.
Mwanafunzi aliyemaliza masomo yake kwenye shule ya High school Coval Reef Miami nchini Marekani Leah Singer, akichukua picha za hafla ya uzinduzi wa uchimbaji wa kisima cha maji cha kijiji cha Sekoture anachokigharamia kwa zaidi ya shilingi milioni 30. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mwanafunzi wa shule ya Covel Reef High School ya jimbo la Miami nchini Marekani Leah Singer (18), ametoa msaada wa zaidi ya shilingi milioni 30 kwa ajili ya kugharamia uchimbaji wa kisima kirefu cha kijiji cha Sekoture kata ya Ilongero jimbo la Singida Kaskazini.
Mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini Mh. Lazaro Nyalandu amesema hayo muda mfupi baada ya kumaliza kukagua maendeleo ya uchimbaji wa kisima hicho kitakachowakomboa wananchi 4,850 wa kijiji cha Sokoture ambao, wamekuwa wakipata adha kubwa kutokana na uhaba wa maji safi na salama.
Amesema mwanafunzi huyo kijana mdogo amefikia uamuzi huo wa kutoa msaada wa kuchimba kisima, baada ya kusoma taarifa ya hitaji la maji kwa wakazi wa kijiji hicho kwenye mtandao wake (Nyalandu).
“Leah baada ya kusoma habari hiyo, alitambua umuhimu wa hitaji hilo na mara moja alianza kuchangisha fedha na hatimaye amefanikiwa kutimiza lango lake na sasa tunashuhudia kisima hiki kirefu kinachimbwa” alifafanua Mh. Nyalandu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo alitumia fursa hiyo kuwataka vijana nchini kuiga mfano wa Leah wa kuwa na moyo wa kujitolea.
Mh. Nyalandu amesema vijana wanapaswa kutambua kuwa kutoa misaada ni moyo na wala si kwa sababu mtu ni tajiri wa kiwango gani.
Akifafanua zaidi, amesema vijana wanao wajibu mkubwa wa kuanzia kuzisaidia familia zao kwa hali na mali na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Leah ambaye baadaye mwaka huu anatarajiwa kujiunga na chuo kikuu maarufu nchini Marekani cha Havard, amesema ataendelea na juhudi zake za kuchangisha fedha za kusaidia makundi ya watu wenye mahitaji muhimu yakiwemo ya maji safi na salama.
CREDIT TO DEWJI BLOG

0 comments:

Post a Comment