SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Monday, May 28, 2012

MAMBO YALIYOJIRI VISIWANI ZANZIBAR

 Mmoja wa waandamani wa Kundi la Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIKI) Kisiwani Unguja,Zanzibar akionyeshan kitambaa kilicho na Damu mapema leo Asubuhi wakati wakiendelea na maandamano yao ambayo yamesababisha vurugu kubwa kisiwani humo,iliyopelekea kuchomwa moto kwa moja ya makanisa pamoja baadhi ya magari yaliyokuwa yameengeshwa karibu na njia wapitazo.vurugu hizo zimeanza jana usiku baada ya kukamatwa kwa kiongozi wa Juimuiya hiyo
 Maelfu wa wazanzibari wakiongozwa na Taasisi za Kiislamu na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) wakifanya matembezi ya amani katika barabara za Zanzibar na kupeleka ujumbe wao kwa viongozi wa serikali za Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Umoja wa Mataifa wakitaka Zanzibar huru ambapo baadhi ya watembeaji hao wakiongoza na Kiongozi wa Jumuiya hizo, Sheikh Farid Hadi Ahmed na viongozi wengine
 Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) liliopo mtaa wa Kariakoo mjini Unguja limechomwa moto jana usiku wa kuamkia leo na watu wasiojulikana
 Gari la Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Bishop Dickoson Maganga lililochomwa moto usiku wa jana katika eneo la Kariakoo nje ya kanisa hilo ambapo uharibifu wote unaelezwa kuwa umegharimu shilingi millioni 120.
 Kikosi cha Kuzuwia Fujo FFU kikizunguka kikiwa kimejihami katika maeneo ya Michenzani ambapo tayari jeshi la polisi limepiga marufuku mikusanyiko yoyote Mjini hapa
Katibu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) Sheikh Abdallah Said Ali ambaye ni miongoni mwa wanaotafutwa na jeshi la polisi akizungumza na Radio DW asubuhi mapema kabla ya taarifa ya kutafutwa kwao kutolewa kwa vyombo vya habari
---
Maelfu ya wazanzibari leo wamefanya maandamano amani kuishindikiza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuitisha kura ya maoni juu ya Muungano na kupeleka ujumbe kwa Umoja wa Mataifa wa kutaka Zanzibar kujitenga kama ilivyofanya Sudan ya Kusini.

Wazanzibari hao wakiongozwa na Sheikh Farid Hadi Ahmed walitembea kutoka viwanja vya Lumumba na kupitia barabara ya Kinazini, Mpigaduri, Michenzani Maskani ya CCM Kisonge, kwa Biziredi na kurudi tena viwanja vya Lumumba.

Maandamano hayo walioyaita matembezi ya amani yalifanyika na kuhudhuriwa na maelfu ya wazanzibari ambapo awali kuliandaliwa kongamano kubwa lililoandaliwa na Taasisi za Kiislamu kwa kushirikiana na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) kwa lengo la kuzungumzia mfumo wa elimu Zanzibar.

Akizungumza na maelfu ya wazanzibari kabla ya kuanza maandamano hayo yaliitwa ni matembezi ya amani, Sheikh Farid alisema wazanzibari wana haki kama walivyokuwa na haki wananchi wengine ulimwenguni kote kudai haki yao ndani ya nchi yao.

“Sisi wazanzibari kama wananchi wengine wowote duniani tuna haki ya kikatiba kudai nchi yetu kama walivyodai Sudan ya Kusini, mbona Sudan ya wameweza kujitenda na kupata nchi yao kwa nini sisi kama wazanzibari tusikubaliwe kudai nchi yetu sasa sisi tunampelekea salam katibu mkuu wa umoja wa mataifa kumwambia kuwa wazanzibari sasa wanataka nchi yao” alisisitiza Sheikh Farid huku akiungwa mkono kwa mamia hao kuinua mikono na kusema ndiooooo.

Awali Sheikh Farid alisema salamu hizo anataka zimfikie Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Kin moon ambaye kwamba wazanzibari wamechoshwa na kuwepo ndani ya Muungano ambao umedumu kwa miaka 48 lakini bado ukiwa na kero nyingi na malalamiko ambayo yanaonekana utatuzi wake ni mdogo na usiowezekana ambapo alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hauna manufaa yena na wazanzibari.

Katika kuonesha kwamba hawataki tume ya katiba ije kuchukua ya maoni ya katiba mpya Sheikh Farid alisema wanataka kwanza kuamuliwe suala la Muungano kabla ya jambo lolote na kuahidi kwamba wataendelea kufanya makongamano, mihadhara na maandamano kwa kadiri wawezavyo hadi hapo serikali itakaposikia kilio hicho.

“Ujumbe huu tunautoa kwa Ban Kin moon, na kwa ulimwengu mzima lakini pia tunataka rais wetu Dk Shein asikie kilio hiki na Rais Kikwete ambaye yeye ni mtetezi wa haki za binaadamu na pia ni mfuatiliaji wa nchi zinazovunja haki za binaadamu tunataka asikie kilio cha wazanzibari kuwa wanataka nchi yao” alisema. 

Alisema juzi wamefanya maombi maalumu ya kumuombea Rais wa Zanzibar lengo likiwa ni kumjaaliwa kheri na awe na maamuzi sahihi juu ya wananchi wa Zanzibar sambamba na kuwaomba Makamu wa Kwanza na makamu wa Pili wa Zanzibar kusikia kilio cha wazanzibari wasiotaka Muungano.

“Tunamuomba Rais wetu Dk Shein, Makamu wa Kwanza Maalim Seif na Makamu wa Pili Balozi Seif kwamba sisi wazanzibari tunahitaji Zanzibar huru, tunahitaji heshima ya nchi yetu na tupo tayari kwa lolote kwa hivyo tunataka salamu hizi na ujumbe huu ukufikieni” alisema Sheikh Farid huku akiungwa mkono na maelfu waliohudhuria katika kongamano hilo ambalo awali liliandaliwa kwa lengo la kuzungumzia masuala la elimu na mfumo wake.

Akiendelea kutoa salamu hizo mara Sheikh Farid alisoma kifungu cha 16 cha katiba na kuwaleza wananchi kwamba haki ya kutembea ni haki ya kila mwananchi ambayo imeainishwa katika katiba na sheria za haki za binaadamu hivyo aliwageukiwa na kuwataka wasimame na kisha kumfuata yeye.

“Haki ya kutembea ni haki ya msingi kwa mujibu wa sheria na kifungu cha 16 kinatupa haki ya kutembea sasa mimi nataka kutembea jeee mpo tayari kutembea na mimi? Alihoji Sheikh huyo huku akijibiwa na umma mkubwa kwamba ndioooo”

Aliongeza kwamba “Tunaanza kutembea na tuone mtu atukamate tunakwenda njia ya kinazini, tunapita michenzani, tunapita barabara ya kwa biziredi na kisha tunarejea hapa hapa kuendelea na kongamano letu kwa amani kabisa mmesikia….akajibiwa ndiooooo”
baada ya kusema hivyo Sheikh Farid alitoa takbir na kuanza kukamatana mikono na viongozi wenzake na huku ummati mkubwa ukiwa umekamatana mikono nyuma na kuanza safari kwa pamoja na kutembea katika barabara ambazo walizitaja awali.

Waandamani hao walikamata mabango yenye maandishi mbali mbali ikiwemo hatutaki muungano, tunataka nchi yetu, zanzibar bila ya muungano inawezekana na wengine kadhalika huku wakitembea njiani na kupiga takbir ambapo walikuwa wakisema Mwenyeenzi Mungu Mkubwa, Mwenyeenzi Mungu Mkubwa sisi hatuna uwezo isipokuwa tunakutegemea wewe Mwenyeenzi Mungu.

Waandamanaji hao walianza kutembea kwa utaratibu maalumu huku magari yakisimama na kuwapisha bila ya kuwepo jeshi la polisi ambapo viongozi wa jumuiya hiyo na wananchi wengine waliongoza utaratibu huo na kutembea katika barabara kwa utaratibu mzuri hadi kumaliza maandamano yao waliyoyaita matembezi ya amani. 

Baadae jeshi la polisi lilifika katika eneo ambalo kumefanyika maandamano hayo na kufungua mabango yao ya kuwataka watu kuondoka lakini wakati magari hayo ya polisi matatu yanafika eneo hilo la Kariakoo tayari ummati mkubwa ulikuwa umeshapita katika eneo hilo na hivyo kuingia ndani ya magari yao na kuondoka kwa salama.

Awali akitoa mada katika kongamano hilo, Maalim Abdulhafidh Malelemba alisema sekta ya elimu imekuw aikidorora Zanzibar kutokana na kukandamizwa na mambo ya Muungano ambapo kila mwaka wanafunzi wanapofanya mitihani kufelishwa kwa makusudi huku idadi ya wanafunzi wanaokwenda katika vyuo vikuu wakiwa kidogo kutokana na kufelishwa katika mitihani ambapo husainiwa na baraza la mithani Tanzania (NECTA).

Wakizungumza katika nyakati tofauti katika kongamano hilo, baadhi ya walimu walisema kukosekana kwa baraza la mitihani Zanzibar kusimamia mitihani ya elimu ya juu ndio sababu ya wazanzibari kufelishwa kwa wingi na kushindwa kuingia katika vyuo vikuu kwa kuwa wanafunzi wengi wa Zanzibar hufelishwa.


Walimu hao walitoa ushahidi wa hivi karibuni wa kufelishwa wanafunzi wa kidatu cha nne ambapo walisema lile ni tukio la makusudia lililofanywa na baraza la mitihani ikiwa ni kuwadhoofishwa wanafunzi wa Zanzibar ili wasiendelee katika masomo kwa kuwafelisha.
----


JUMUIYA YA UAMSHO NA MIHADHARA YA KIISLAMU

(JUMIKI)

للجنة الدعوة الإسلامية

THE ASSOCIATION FOR ISLAMIC MOBILISATION AND PROPAGATION

P. O. BOX: 1266 -Tel:             +255-777-419473 begin_of_the_skype_highlighting            +255-777-419473      end_of_the_skype_highlighting       / 434145- FAX +255-024-2250022 E-Mail: jumiki@hotmail.com

MKUNAZINI ZANZIBAR


Tarehe 27MAY2012 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Kila sifa njema anastahiki ALLAH (S.W) na Rehma na Amani zimuendee Mtume Muhammad (S.A.W), ahli zake, Maswahaba zake na walio wema katika Uislamu.

Jumuia ya UAMSHO inatoa taarifa rasmi kwa umma wa Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla kwamba haihusiki na vitendo vyote vya uvunjaji wa amani vilivyotokea usiku wa tarehe 26 Mei 2012. Kama alivyosema Mtume (S.A.W) katika Hijatul Wadaa, kwamba ni haramu kumwaga damu zenu, kuharibiana mali zenu, kuvunjiana heshma zenu ila kwa haki ya Uislamu (maana yake pale mtu anapofanya kosa na likathibitika atahukumiwa kwa hukmu ya Kiislamu). Vile vile Uislamu unaheshimu nyumba za ibada (Makanisa, Mahekalu na n.k) zisivunjwe wala zisiharibiwe.

Jumuia inatoa wito kwa Waislamu na Wazanzibari wote kuendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi na kutoharibu mali za serikali, mali za wananchi, mali za taasisi za dini zenye imani tofauti, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu. Jumuiya inayachukulia matukio yaliyotokea usiku wa jana, na yanayoendelea tangu alfajiri leo, kama ni njama za makusudi za wale wasioipendelea amani nchi hii, pamoja na kutaka kuipaka matope jumuiya na kutaka kuzuia lengo la Wazanzibari kudai nchi yao.

Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na Vyombo vyote vya Dola wafanye kazi zao kama wanavyotakiwa kwa mujibu wa muongozo wa haki za binadamu kwa Polisi na vikosi vingine unaosema kwamba polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu. Kila mtu anayo haki ya kuwekewa mazingira muafaka ya kitaifa na kimataifa yatakayomuwezesha kupata haki zake za binadamu.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu isipokuwa tu kwa minajil ya kulinda haki za wengine.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kuheshimu, kulinda na kutetea haki za binadamu kwa watu wote.

WABILLLAH TAWFIQ .

0 comments:

Post a Comment