Na maggid mjengwa
Nimeiona habari kubwa kwenye ITV usiku wa leo; Aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw. Iddi Simba amefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Ni Iddi Simba ambaye alilazimika kujiuzuru uwaziri kwa kashfa ya sukari. Ni Iddi Simba ambaye huko nyuma aliipigania sana sera ya Uzawa.
Na kadhia iliyomkumba sasa inahusu kafsha ya UDA. Ni lililokuwa Shirika la Usafiri Dar Es Salaam. Iddi Simba amesomewa mashtaka 8 ikituhumiwa kudanganya, kughushi na kulitia hasara ya shilingi milioni 320 Shirika la Usafiri Dar es Salaam ( UDA).
Tafsiri yangu;
Huu ni mwendelezo wa mwanzo uliotiliwa mashaka. Kuna watakaoanza kuamini, kuwa zama za kulindana zimeanza kufikia ukingoni.
Iddi Simba ni kigogo. Ni Mzee wa Dar es Salaam. Ni Mwenyekiti wa Wazee wa Dar es Salaam. Leo amefikishwa kwenye Mahakama ya katikati ya Jiji la Dar. Bila shaka, kuna ambao hawakuamini kumwona Idi Simba kwenye runinga akikalia kwenye benchi la Mahakamani.
Naam, tunaziona ishara la wimbi kubwa linalokuja, si dogo hata kidogo. Yumkini naye anasafisha njia ya wengine kufuatia. Na tusubiri tuone.
0 comments:
Post a Comment