TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA KUHUSU SAKATA LA MGOMO WA MADAKTARI WANAOFANYA KAZI CHINI YA USIMAMIZI (INTERN DOCTORS).
Chama cha Madaktari Tanzania kimesikitishwa sana na mgogoro na migomo inayoendelea katika hospitali mbalimbali nchini kwa Madaktari wanaofanya kazi chini ya usimamizi yaani “interns”.
Tatizo kubwa ni kwamba Serikali haijawalipa malipo yao kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi mitatu hali ambayo imewafanya washindwe kuendelea na kazi yao ya kuokoa maisha ya Watanzania wasiokuwa na hatia
Ikumbukwe kwamba Madaktari hawa walio chini ya uangalizi ndiyo uti wa mgongo wa utoaji huduma katika hospitali wanazofanya kazi hasa ikichukuliwa kuwa wao ndio wa kwanza kumwona mgonjwa na kumpa matibabu kabla ya kuonwa na Madaktari Bingwa walio wachache.
Hivyo, kutokuwepo kwao kazini kunafanya utoaji wahuduma kwa wananchi kudorora katika hospitali husika.
Baada ya kufanya utafiti wa kina, chama kimebaini kuwa hospitali tano za rufaa nchini tayari Madaktari hawa wameshindwa kufanya kazi zikiwemo:
1. Hospitali ya Taifa Muhimbili
2. Hospitali ya mkoa wa Tanga Bombo
3. Hospitali ya Mount Meru Arusha
4. Hospitali ya Mkoa wa Dodoma
5. Hospitali ya Manispaa ya Temeke
Katika vituo ambavyo Madaktari wameendelea kufanya kazi, imebainika kuwa ni kutokana na vituo, hospitali au halmashauri husika kuamua kuwakopesha wataalam hao ili kuwawezesha wataalam hao kuweza kuendelea na maisha yao ya kila siku huku wakitoa huduma wakati ufuatiliaji ukiendelea kwenye serikali kuu.
Aidha Chama kimebaini kuwa hali hii inaenea katika hospitali nyingine zenye Madaktari hawa na pia inaleta mzigo mkubwa kwa wale madaktari mabingwa na waandamizi na hii inaweza kuleta mgogoro katika fani yote ya udaktari nchi nzima.
Pia Chama kinakitafsiri kitendo cha kutowalipa Madaktari malipo yao na kuwafanya waishi kwa shida kwa muda huo wote kuwa ni kitendo cha dharau kwa fani ya udaktari na huduma wanazotoa kwa wananchi. Pia ni udhalilishaji wa hali ya juu kuwaacha madaktari waishi kwa kuomba omba huku wakitoa huduma kwa wananchi. Pia inatafsiriwa kuwa ni jinsi gani serikali isivyojali huduma za afya kwa wananchi inaowaongoza.
Kutokana na hayo:
1. Chama kinalaani kitendo cha Serikali kupitia Wizara ya Afya kutowalipa Madaktari malipo yao halali hadi kufikia mgomo unaopelekea wananchi kukosa huduma stahili za matibabu
2. Chama kinaitaka jamii na Serikali ielewe wazi kuwa madaktari kuwepo kazini bila malipo kwa muda mrefu ni uvunjifu wa haki za binaadamu, kinyume na kiapo cha udaktari na inapelekea utoaji wa huduma hafifu na vitendo vya uvunjifu wa sheria kama kukaribisha mazingira ya rushwa.{Sehemu ya kiapo inayozungumziwa inasema hivi “...Wakati nikikishika kiapo hiki na ijaliwe kwangu kufurahia maisha na kazi yangu, jamii inikumbuke na kuniheshimu nikiwa hai au nimekufa..."
3. Chama kinaitaka Serikali kuwalipa Madaktari wote malipo yao mara moja ndani ya kipindi cha masaa 48 ili waweze kuendelea kufanya kazi ya kuwahudumia Watanzania
4. Chama kinaitaka Serikali kuheshimu kazi ya udaktari na huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi na iepuke kuwa chanzo cha migogoro ya mara kwa mara katika sekta ya afya.
5. Chama kinaitaka Serikali yaani viongozi wa Wizara na taasisi kuacha kutumia lugha za vitisho wakati tete kama huu hasa baada ya kushindwa kuwalipa Madaktari stahili zao
6. Chama kinaitaka Serikali kuwa na mipango endelevu na ya muda mrefu katika kulipa stahili za wafanyakazi ili kuepuka kufanya kazi kwa zimamoto kama inavyofanya sasa
7. Chama kinaialika Wizara ya Afya kushirikiana nacho katika utendaji wake ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima kama hii inayopelekea mateso kwa wananchi wasio na hatia.
Kwa kumalizia, chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kinapinga unyanyasaji unaofanywa na Wizara ya Afya kwa wataalamu wake, pia chama kinaona wataalam hawa hawana hatia ya uvunjifu wa kiapo chao katika kutoa huduma kwa watanzania kutokana na serikali kutokutimiza wajibu wake kama inavo elekeza kwenye kiapo na makubaliano ya kazi.
Chama pia kinasikitishwa na matokeo yanayotokana na mgogoro huu kwa wananchi wasio na hatia na taifa kwa jumla.
Pia chama kinazipongeza hospitali, na halmashauri zote zilizoamua kuwakopesha madaktari malipo yao ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Chama kinapenda kuweka wazi kwamba iwapo Wizara itashindwa kushughulikia malipo haya ndani ya saa 48 basi itatulazimu kuitisha mkutano wa dharura kwa Madaktari nchini ili kutafakari mstakabali wa jambo hili nyeti na yote yanayohusu fani ya udaktari katika Taifa letu.
Taarifa hii imetolewa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT)
Dr. Namala mkopi
Rais - MAT
Na www.wavuti.com/
0 comments:
Post a Comment