SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, October 7, 2011

RAIS JK AKAGUA UZALISHAJI WA UMEME KIDATU

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikagua mitambo ya kuzalisha umeme katika bwawa la Kidatu,mkoani Morogoro jana .Kushoto ni meneja wa TANESCO wa mkoa na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera Picha na Freddy Maro wa Ikulu.
Mwandishi Wetu, 
Kidatu Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ametembelea bwawa la uzalishaji umeme wa gridi ya Taifa la Kidatu, mkoani Morogoro kujionea mwenyewe kina cha maji katika bwawa hilo, moja ya vianzio vikubwa vya umeme nchini. 
Rais Kikwete alisimama na kuangalia bwawa hilo kwa muda mfupi tu baada ya kuwa amefunga Mafunzo ya Uchunguzi na Upelelezi wa Maofisa wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi kwenye Chuo cha Polisi kilichoko hapo hapo Kidatu. Kwenye bwawa hilo, Rais aliambiwa na Kaimu Meneja wa Uzalishaji Umeme Kidatu, Mhandisi Joseph Lyaruu kuwa hali ya uzalishaji umeme kutoka Kidatu bado ni mbaya kwa sababu ni megawati 40 tu za umeme zinazozalishwa kwenye bwawa hilo kwa sasa kulinganisha na uwezo wa uzalishaji wa megawati 200 kwa sababu ya kupungua kwa kina cha maji kwenye bwawa hilo. 
Mhandisi Lyaruu pia alimweleza Rais Kikwete kuwa hata uzalishaji umeme katika bwawa jingine la Mtera lililoko mkoani Iringa bado ni mdogo sana kwa sababu bwawa hilo linazalisha kiasi cha megawati 30 tu kati ya megawati 80 zinazoweza kuzalishwa kwenye bwawa hilo kama yapo maji ya kutosha. “Hali bado mbaya,” Rais alisema baada ya kuwa ameelezwa na Mhandisi Lyaruu kuhusu hali hiyo ambayo imesababisha mgawo mkubwa wa umeme nchini kwa miezi kadhaa sasa na kusababisha Serikali kuchukua hatua za dharura za kuzalisha umeme kutokana na vyanzo vingine. 
Akiwa njiani kuelekea Ifakara kutoka Kidatu, Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya siku tatu ya Mkoa wa Mogororo alisimama kwa muda katika Kijiji cha Mkula kupata maelezo kuhusu skimu ya umwagiliaji ya kilimo cha mpunga, ambayo aliifungua mwaka 2008 wakati wa ziara nyingine ya mkoa huo. 
Kwenye kijiji hicho, Rais Kikwete aliambiwa kuwa kutokana na skimu hiyo ya umwagiliaji ambayo ilijengwa kwa kiasi cha Sh276 milioni za Serikali, wananchi wa kijiji hicho sasa wameongeza uzalishaji wa mpunga hadi kufikia tani 7.6 kwa ekari moja kutoka tani 1.5 iliyokuwa inavunwa kabla ya kuanza umwagiliaji. Wanakijiji hao walimwambia Rais: “Tumesikia unapita na tukaamua kujikusanya kukushukuru kwa msaada wako. 
Uliahidi kutupatia power tillers tano na tayari tumekwishakupokea nne. Tulikuwa tunalina ekari 12 tu kabla ya skimu ya umwagiliaji kujengwa na sasa tunalipa ekari 100 kati ya eneo la ekari 254 za eneo hili. Tunakushukuru sana kwa sababu yote uliyotuahidi ulipofika hapa mwaka 2008 yametimizwa.” Waliongeza wanakijiji katika risala yao: “Kipato chetu kimeongezeka kiasi cha kutosha Mheshimiwa.
Tunacho chakula cha kutosha na ziada kubwa ya kuuza. Tunaweza sasa kulipa ada ya wanafunzi wa shule yetu, tuna chakula mwaka mzima, tunazo pesa za matibabu na tuna uwezo wa kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo.” Walisema wana-kijiji hao: “Ni viongozi wachache sana wanaoahidi kuwatembelea tena wanavijiji na wakafanya hivyo, tena kututembelea sisi kwenye hii vumbi. Kama ungekuwa mchezaji wa mpira hakuna shaka kuwa ungenunuliwa kwa bei mbaya.”
CHANZO: CLICK

0 comments:

Post a Comment