Mwandishi wetu, Dar es Salaam
RAIS Jakaya Kikwete anatararajiwa kuongoza viongozi wenzake kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki katika mkutano wa siku mbili wa uwekezaji utakaohudhuriwa na mamia ya watu.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa kuhusu mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Uwekezaji nchini (TIC), Emmanuel Ole Naiko aliwashukuru Watanzania kwa kujiandikisha kwa wingi kuhudhuria mkutano huo.
“Tunawashukuru Watanzania kujitokeza kwa wingi na kuthibitisha kushiriki katika mkutano huu muhimu,” alisema Naiko.
Naiko pia aliwashukuru wafadhili wa mkutano huo kwa msaada wao mkubwa katika kufanikisha mkutano huo.
Alizitaja kampuni zilizofadhili mkutano huo mpaka sasa kuwa ni Vodacom Tanzania, IPP Media, BoA Bank, Twiga Cement na Tanzania Breweries Limited.
Aliwatka kampuni nyingine kufadhili mkutano huo unaotarajia kutoa fursa ya pekee kwa nchi za Afrika Mashariki kunadi maeneo muhimu ya uwekezaji.
Wafanyabiashara wengi kutoka nchi mbalimbali duniani na Jumuiya ya Madola watatumia mkutano huo kujionea fursa za uwekezaji zilizopo katika eneo la Afrika Mashariki ikiwamoTanzania.
“Ni fursa pekee kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuutumia mkutano huu kunadi vivutio na fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika ukanda huu,” alisema mkurugenzi huyo.
Katika meza ya duara, Tanzania itatangaza maeneo yote yanayohitaji zaidi uwekezaji, lakini itaweka mkazo zaidi katika kilimo na usindikaji na bila kusahau maeneo mengine yakiwamo ya utalii, miundombinu ili kupata wawekezaji kama njia ya kukuza uchumi.
Uganda itatangaza eneo la madini na nishati, Burundi Kilimo na chakula, Rwanda Afya na Elimu, wakati Kenya itatangaza Usafirishaji na huduma.
Akizungumza hivi karibuni na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Juma Mwapachu alisema mkutano huo ni muhimu sana kwa Tanzania kwani itapata fursa nzuri ya kujitangaza kwa wawekezaji.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment