Maafisa wa usalama nchini Thailand wametumia risasi kutawanya waandamanaji waliokuwa wamepiga kambi katikati mwa mji mkuu Bangkok.
Waandamanaji hao wanataka waziri mkuu ajuhuzulu na uchaguzi wa mapema ufanyike.
Waziri mkuu aliahidi kuvunja bunge la nchi hiyo lakini pande zote mbili zikashindwa kuelewana kuhusu ni nani anapaswa kulaumiwa kwa kusababisha machafuko ya mwezi jana.
Idadi kubwa ya waandamanaji hao inaunga mkono waziri mkuu Thaksin Shinawatra ambaye aling'olewa mamlakani mwaka 2006 baada ya mapinduzi kufanyika.
Makabiliano makali
Mwandishi wa BBC mjini Bangkok anasema mji sasa ni uwanja wa vita na kuna ripoti kuwa waandishi wawili wa habari wa Televisheni ya Ufaransa na mmoja kutoka gazeti la Thailand la Matichon wamepigwa risasi miguuni.
Msemaji wa serikali Panitan Wattanayagorn ameiambia BBC kuwa maafisa wa usalama wanataka kuzingira eneo hilo na wala sio kusababisha machafuko.
Maelfu ya waandamanaji wakiwemo wanawake na watoto wameapa kuendelea kupiga kambi katikati mwa mji huo wa Bangkok.
Msemaji wa waandamanaji hao amewalaumu maafisa wa usalama kwa kusababisha machafuko hayo lakini maafisa hao wanasema wana ruhusa kushambulia kwa nia ya kujilinda.
Haya ndiyo machafuko mabaya zaidi ya kisiasa kuwahi kutokea nchini Thailand kwa muda wa miongo miwili na tayari watu 30 wameuawa na zaidi ya 1,400 kujeruhiwa.
0 comments:
Post a Comment