Baadhi
ya wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Dar es
salaam wakiwa na nyuso za furaha wakati wa mahafari ya 49 ya chuo hicho
yaliyofanyika katika ukumbi wa Blue Pearl jana jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Viwanda na Biashara Dkt. Abdallah Kigoda (kulia) ambaye alikuwa
mgeni rasmi katika mahafali ya 49 ya Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi
ya Dar es salaam akiimba wimbo wa Taifa wakati wa ufunguzi rasmi wa
mahafali hayo jijini Dar es salaam. Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Mathew Luhanga (katikati) na Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Emanuel Mjema.
Na. Aron Msigwa – Dar es salaam.
SERIKALI
imewataka watendaji na wamiliki wa makampuni mbalimbali kutoka ndani na
nje nchi kuacha tabia ya kutoa nafasi nyingi za ajira kwa wageni na
badala yake wawatumie vijana wa kitanzania wanaohitimu masomo katika
vyuo mbalimbali hapa nchini.
Kauli
hiyo imetolewa jana jijini Dar es salaam na Waziri wa Viwanda Biashara,
Dkt. Abdallah Kigoda wakati akizungumza na wahitimu 3363 wa fani
mbalimbali wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Dar es salaam
waliohudhuria mahafali ya 49 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es
salaam.
Amesema
Tanzania ina vijana wengi wenye kukidhi viwango na uwezo wa kutekeleza
majukumu ya Uhasibu,Udhibiti wa Biashara, Usimamizi wa Masoko,Manunuzi
na Ugavi , Mizani na Vipimo pamoja na Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano kwa ufanisi mkubwa kutokana na mafunzo waliyopewa katika
vyuo na taasisi mbalimbali hapa nchini.
Baadhi
ya wahitimu wa shahada ya Uhasibu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es
salaam mwaka 2014 wakisubiri kutunukiwa shahada zao wakati wa mahafali
ya 49 yaliyofanyika katika ukumbi wa Blue Pearl,Ubungo jijini Dar es
salaam.
“Tanzania
tunao vijana bora na wenye kukidhi viwango wanaohitimu kila mwaka,suala
la kutoa visingizio kuwa hatuna wataalam na makampuni haya kuajiri
wageni katika nafasi za kawaida na ngazi za utawala mimi sikubaliani
nalo ,nakemea tabia hii” Amesisitiza Dkt. Kigoda.
Amefafanua
kuwa Serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa tatizo la ukosefu wa
ajira lililopo hapa nchini kwa kujenga na kuandaa mazingira wezeshi ya
kukuza utengenezaji wa ajira za kujiajiri na kuajiriwa kwa kuendeleza
sekta binafsi katika eneo la Kilimo, Sekta ya Viwanda na Biashara
hususan ujasiriamali mdogo na wa kati.
Ameeleza
kuwa serikali inaendelea kujenga mazingira wezeshi na rafiki kwa
wahitimu hao kujiajiri wenyewe kwa kuratibu mfumo wake wa kodi na tozo
mbalimbali, kuangalia hatua za utoaji wa leseni na usajili wa biashara,
kushughulikia tatizo la uhaba wa mikopo na riba zinazotolewa kwa wale
wanaotumia mikopo kama mitaji pamoja na kushughulikia suala la mikataba
inayoandaliwa na makampuni ambayo mara nyingi inawakosesha vijana fursa
ya kupata ajira.
Waziri
wa Viwanda na Biashara Dkt. Abdallah Kigoda akizungumza na wahitimu wa
Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam waliohitimu masomo
yao kwa mwaka 2014. Takribani wahitimu 3459 wametunukiwa Astashahada,
Shahada na Stashahada za fani mbalimbali.
Ametoa
wito kwa wahitimu hao kuwa wajasiri na wenye moyo wa kuthubutu wa
kutumia taaluma na mafunzo waliyopata kuleta mabadiliko na maendeleo
nchini huku akiwataka wahitimu hao kuepuka tabia ya uzembe, uvivu na
Rushwa pindi watakapoingia kwenye ajira.
Kuhusu
uboreshaji chuo hicho Dkt. Kigoda amesema Serikali inaendelea
kukijengea uwezo chuo hicho kwa kuimarisha ubora wa mafunzo yanayotolewa
hususan matumizi ya mifumo ya kompyuta na mawasiliano (ICT) ili kiweze
kushindana na vyuo vya kigeni vilivyoanzisha kampasi zao hapa nchini.
Kwa
upande wake mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo hicho Prof. Mathew
Luhanga akizungumzia mahafali hayo ya 49 ya chuo hicho amesema kuwa
yanakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho.
Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Emanuel Mjema akizungumza na
wahitimu 3459 wa fani mbalimbali wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi
ya Dar es salaam waliohitimu masomo yao mwaka 2014.
Amesema
tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1965 mafanikio mbalimbali
yamepatikana yakiwemo ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa
kujiunga na masomo hadi kufikia kutoka 25 pindi chuo kinaanzishwa hadi
14000 wa sasa, ongezeko la kampasi kutoka 1 hadi kufikia 4.
Ameyataja
mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za
mafunzo kutoka 1iliyokuwepo mwaka 1965 hadi 6 zilizopo sasa na ongezeko
la wakufunzi wenye shahada ya uzamivu (PhD).
Prof.
Luhanga amefafanua kuwa chuo hicho sasa kimeanzisha ushirikiano wa
elimu na vyuo vikuu vingine vilivyo nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha
Maastricht cha Uholanzi, Chuo Kikuu cha Stockholm cha Sweeden na Chuo
Kikuu cha Eastern Finland ambacho kimeshirikiana na CBE kutoa mafunzo
ya shahada ya uzamivu kwa nchi za SADC.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Mathew Luhanga akizungumza na wahitimu hao.
Naye
Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema akiwakaribisha wahitimu, wadau
mbalimbali na Wanajumuiya wa Chuo hicho waliohudhuria mahafali hayo
amesema kuwa chuo chake kimepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa
kwake mwaka 1965 ikiwemo ongezeko la idadi ya wanafunzi wa kike
wanaohitimu chuoni hapo hadi kufikia asilimia 48 kwa mwaka 2014.
Amesema
tangu kuanzishwa kwa chuo hicho wataalam wengi katika fani za
Uhasibu,Udhibiti wa Biashara, Usimamizi wa Masoko,Manunuzi na Ugavi ,
Mizani na Vipimo pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wameweza
kuhitimu na kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Waziri
wa Viwanda na Biashara Dkt. Abdallah Kigoda akisoma tamko la kuwatunuku
wahitimu 3495 wa fani mbalimbali wa chuo cha CBE wakati wa mahafali ya
49 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Viwanda na Biashara Dkt. Abdallah Kigoda akiondoka ukumbini akiwa
ameambatana na viongozi wengine wa chuo cha Elimu ya Biashara CBE
kampasi ya Dar es salaam mara baada ya kufunga rasmi mahafali
hayo.(Picha na Aron Msigwa –MAELEZO).
0 comments:
Post a Comment