Bwana Christopher Mush Smith wa Hoteli ya La Gema akikata Keki Maalum yenye Bendera za Tanzania na China iliyoandaliwa na Hoteli hiyo kwa ajili ya Mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Li Yuanchao aliyepo pembeni yake akiwa sambamba na Mwenyeji wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China imekusudia kuongeza nguvu za ziada katika kusaidia kuimarisha miundo mbinu ndani ya Bara la Afrika kwa lengo la kuyajengea uwezo wa uzalishaji wa kiuchumi Mataifa mbali mbali yaliyomo ndani ya Bara hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa China Bwana Li Yuanchao wakati yeye na ujumbe wake alipofanya mazungumzo Rasmi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiuongoza Ujumbe wa Zanzibar kwa Niaba ya Rais wa Zanzibarna Mwenyekiti wa Bararaza la Mapinduzi Dr. Ali Moh’d Shein hapo hoteli ya La gema Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Bwana Li Yanchao akiwa Zanzibar kwa siku moja akiendelea na ziara yake ya siku sita Nchini Tanzania alisema katika utekelezaji wa azma hiyo China imejipangia kutumia Yuan Bilioni 2.2 katika mipango yake ya kuimarisha miundo mbinu hiyo ya uwekezaji kwenye sekta ya biashara.
Aliishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuitumia fursa hiyo adhimu kwa kuchagua miradi yake itakayoipa kipaumbele cha kwanza kwa kuwasiliana na Ofisi ya Ubalozi mdogo wa Nchi hiyo uliopo Zanzibar ili kuratibu miradi hiyo na hatimae hatua za utekelezaji zianze mara moja.
Bwana Li Yuachao alifahamisha kwamba China kupitia wataalamu wake itaangalia mfumo wa uwekezaji uliopo hapa nchini na kuwashawishi wafanya biashara wa nchi hiyo iliyopiga hatua kubwa kiuchumi kuwekeza miradi yao katika visiwa vya Zanzibar.
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Watu wa China alipongeza uhusiano wa muda mrefu uliopo kati yaJamuhuri ya Watu wa China na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla na unastahiki uimarishwe zaidi kwa ustawi wa baadaye wa pande zote mbili.
Alisema miaka mingi iliyopita ya ushirikiano wa kindugu uliofikiwa kati ya pande hizo mbili imeipa faraja kubwa Tanzania kutokana na nguvu kubwa iliyopata ya uimarishaji wa uchumi kupitia misaada mbali mbali inayotolewa na China.
“ Tumeshuhudia ziara za Viongozi wetu wakuu wa pande zote mbili jinsi wanavyotembeleana ikionyesha wazi uthibitisho wa uhusiano huo mkubwa unaopaswa kulindwa kwa nguvu zote “ . Alisema Bwana Li Yanchao.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa shukrani zake alisema Zanzibar itaendelea kuiheshimu na kuithamini China kutokana na msimamo wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati za kuimarisha uchumi.
Balozi Seif alieleza kwamba Jamuhuri ya Watu wa China inastahiki kupongezwa kwa misaada yake mikubwa inayotoa kwa Zanzibar ambayo haijawahi kutokea katika Historia ya Zanzibar tokea Mapinduzi ya Mwaka 1964.
Alisema Wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakishuhudia misaada tofauti inayotolewa na China ndani ya kipindi cha miaka 50 tokea Mapinduzi iliyolenga katika sekta za afya, elimu, maji, miundo mbinu, kilimo pamoja na mawasiliano.
Balozi Seif alieleza kwamba ujenzi wa maegesho ya ndege katika uwanja wa ndege wa Zanzibar, uwepo wa Madaktari wa Kichina wanaofanyakazi katika hospitali mbali mbali nchini, ujenzi wa hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani Pembapamoja na ujenzi wa skuli ya Sekondari za Wilaya ni ushahidi wa misaada hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza ujumbe huo wa China unaoongozwa na Makamu wa Rais wake kwamba wawekezaji wa nchi hiyo wako huru kuitumia fursa iliyotolewa na Zanzibar katika uwekezaji vitega uchumi ndani ya sekta ya Utalii.
Balozi Seif alisema Zanzibar inahitaji kuwa na ukumbi mkubwa wa kimataifa utakaoweza kutoa huduma za mikutano ya kimataifa sambamba na watalii wa China kuombwa kupanga safari za kuitembelea Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Li Yanchao alifuatana na Mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bwana Qian Hongshan, Naibu Waziri wa Taasisi ya IDCC ya Chama cha Kikoministi cha China Bwana Yu Hongjuu, Katibu Mkuu wa Vijana wa Chama cha Kikoministi cha China Bwana Qin Yizhi, Balozi Mdogo wa China Bwana Lu Yunliang pamoja na Naibu Waziri wa Fedha wa China Bwana Li Junzao.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika mazungumzo hayo aliambatana na Balozi wa Tanzania Nchini China Balozi Abdullrahman Shimbo. Waziri wa Fedha Zanzibar Mh. Omar Yussuf Mzee pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dr. Mwinyihaji Makame.
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofiri ya Rais Utawala bora wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kepteni George Mkuchika, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Mh. Nassor Ahmed Mazrui pamoja na mshauri wa Rais wa Zanzibar Balozi Mohd Ramia.