Kamanda Kanda Maalum, Seleman Kova akiwa ameshika meno ya tembo.
=====
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu raia wa China, Yu Bo (45), kulipa
faini ya Shilingi bilioni tisa au kwenda jela miaka 20 baada ya kukiri
kukutwa na nyara za serikali.
Yu,
alikamatwa akiwa na kilo 303 za nyara hizo ikiwamo ngozi za vinyonga
wawili vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 975 mali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Devota Kisoka, baada ya upande wa Jamhuri kumsomea mshtakiwa mashitaka na kukiri.
Alisema
baada ya mshtakiwa kukiri makosa yake, mahakama imemtia hatiani na
kumhukumu kulipa faini ya Shilingi bilioni tisa na akishindwa aende jela
miaka 20.
Hata hivyo, hadi NIPASHE inaondoka mahakamani hapo jana saa 9:00 alasiri Yu alikuwa hajafanikiwa kulipa faini hiyo.
Kabla ya
hukumu hiyo kusomwa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi,
alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na alimkumbusha mshtakiwa
mashitaka yake.
Nchimbi
alidai kuwa Desemba 30, mwaka 2013, katika Bandari ya Dar es Salaam,
mshtakiwa alikutwa na nyara hizo bila kuwa na leseni ya Mkurugenzi wa
Wanyamapori.
Alidai
kuwa mshtakiwa alikutwa akiwa na vipande 81 vya pembe za ndovu ambazo
zimetokana na kuwaua tembo 40 zenye thamani ya Sh. 975,076,350 na ngozi
mbili za vinyonga wawili zenye thamani ya Sh. 3,044,140 vyote vikiwa na
jumla ya thamani ya Sh. 978,120,490 mali ya Serikali ya Tanzania.
Mshtakiwa baada ya kusomewa maelezo hayo alikiri na mahakama ikamhuku adhabu hiyo.
CHANZO: NIPASHE