SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Saturday, September 15, 2012

WAOMBAJI KAZI WAMETAKIWA KUJIANDAA WANAPOENDA KWENYE USAILI


Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Bw. Xavier Daudi (kushoto) akifafanua jambo kwa Waandishi wa habari (hawapo pichani) na kulia ni Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Ajira, Bw. Bakari Mahiza.
****
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amesema ofisi yake hivi sasa itakuwa ikitoa ratiba ya usaili mapema kila mara ili kuwawezesha wasailiwa kuwa na muda wa kutosha kujiandaa kabla ya kwenda kwenye usaili husika.
Amesema hayo leo wakati akiongea na mwandishi wa habari ofisini kwake alipokuwa akitoa ratiba ya usaili kwa mwezi Septemba, 2012 pamoja na tangazo la kuita kazini waombaji waliofaulu usaili uliopita. Aliongeza kuwa ili msailiwa aweze kufanya vizuri katika usaili pamoja na vigezo vya kitaaluma alivyonavyo bado anatakiwa kujiandaa vyema na kujiamini anapojibu maswali wakati anapokuwa kwenye usaili.
Daudi amesema hivi sasa dunia imekuwa ya utandawazi na fursa za ajira ni za ushindani zaidi, maana wahitimu hivi sasa ni wengi na hawana ajira hivyo ni vyema kwa wahitimu wanapoomba nafasi za kazi na kuitwa kwenye usaili wawe wamejiandaa vya kutosha ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata ajira.
Katibu amesema usaili kwa mwezi Septemba, utaanza tarehe 18 Septemba hadi 5 Oktoba, 2012 kwa taasisi zifuatazo; Wakala wa Barabara (TANROADS), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), TEMESA, ADEM, CARMATECH, NEEC (UWEZESHAJI), Chuo cha Utalii, Chuo cha Diplomasia, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Wizara ya Fedha (PFMRP) EPZA, na Maafisa Tarafa.
Amesema kwa maelezo zaidi ya nafasi hizo na wapi usaili utafanyika ni vyema waombaji wakaperuzi tovuti ya Sekretarieti ya Ajira pamoja na tovuti za Taasisi husika na kufungua tangazo la kuitwa kwenye usaili ili kuiona ratiba nzima ya tarehe ya mchujo na usaili kama zinavyoonekana katika tangazo lenye orodha ya majina ya kuitwa kwenye usaili.
Aidha, amesisitiza ni muhimu kwa waombaji kuzingatia masharti ya tangazo pindi wanapoenda kwenye usaili kwani ni njia mojawapo ya kujua msailiwa amejiandaa kwa kiasi gani.
Wakati huohuo, Katibu amewataka waombaji wa nafasi za kazi waliofanya usaili kuanzia tarehe 7 hadi 31, Agosti, 2012 katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Biashara (CBE), Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo cha Maji (WDMI), Chuo cha Mipango Dodoma (IRDP), Chuo cha Serikali za Mitaa- Hombolo, COASCO, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Tume ya Mionzi (TAEC), Taasisi ya Utafiti wa Samaki (TAFIRI), Wakala wa Mbegu (TOSCI), Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) kuangalia majina yao katika tovuti ya Sekretarieti ya Ajira pamoja na taasisi husika ili kujua waliofaulu.
Amesema kwa waliofaulu usaili wanatakiwa kuripoti kwa Mwajiri katika muda ambao umeainishwa kwenye barua zao za kupangiwa vituo vya kazi wakiwa na vyeti halisi (Originals) vya masomo kuanzia kidato cha nne na kuendelea ili vihakikiwe na mwajiri kabla ya kupewa barua ya ajira. Aidha, barua za kuwapangia vituo vya kazi zimetumwa kupitia anuani zao za posta.
Alimalizia kwa kusema kuwa, kwa wale ambao hawataona majina yao katika tangazo husika watambue kuwa maombi yao hayakufanikiwa na wasisite kuendelea kuomba mara nafasi za kazi zitakapotangazwa tena.
CHANZO: BOFYA HAPA

0 comments:

Post a Comment