WAZIRI wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
Na Mary Victoria
Na Mary Victoria
WAZIRI wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema atahakikisha kampuni ya China National Gold Group Corporation (CNGGC) ambayo iko mbioni kununua hisa zaidi ya asilimia 30 za kampuni ya African Barrick Gold (ABG) kwamba haichimbi madini nchini hadi hapo ABG itakapolipa madeni yote inayodaiwa na Serikali ya Tanzania, Raia Mwema limeelezwa.
Msimamo huo wa Serikali umetokana na taarifa za hivi karibuni ambazo pia zilithibitishwa na Profesa Muhongo kwamba ABG imekuwa kwenye majadiliano ama tayari imeshajadiliana na kukubaliana na CNGGC juu ya kuuza hisa zake.
Profesa Muhongo amesema wameanza kuchunguza taarifa hizo na kwamba atahakikisha kampuni hiyo ya China haichimbi madini nchini hadi kampuni ya ABG ihakikishe imelipa madeni yote inayodaiwa kutokana na shughuli zake za uchimbaji madini nchini.
“Tutahakikisha kwamba kila kitu kinalipwa la sivyo atakayenunua hisa za kampuni ya ABG ndiye atakayelipa madeni yote kabla ya kuanza uchimbaji. Tunaendelela kufuatilia kila kitu kwa ukaribu sana, kwa kuwa wao wanatumia akili nyingi inatakiwa umakini kwelikweli,”alisema Profesa Muhongo na kuongeza:
“Ikiwa hawatalipa na wataamua kuwadanganya Wachina, basi Wachina hao uchimbaji wao utakuwa mgumu na hivyo nitamueleza pia Balozi wa China nchini Tanzania Lu Youqing kuhusu kampuni hiyo, ikiwa itanunua hisa za kampuni ya ABG iwe tayari kulipa gharama zote ambazo ABG imekwepa kuzilipa.”
Kauli hizo za Profesa Muhongo zinafuatia maoni kwamba Wizara yake inawachukua hatua gani kwa wamiliki wa kampuni za uchimbaji madini, gesi asilia na mafuta ambazo zimekuwa zikikwepa kulipa kodi kwa muda sasa na baadhi zimeamua kuuza hisa kwa kampuni nyingine ya kigeni kama ambavyo ABG inataka kufanya kwa sasa.
Maoni hayo yanatokana na taarifa ya ABG kupitia barua pepe kuwa imekuwa kwenye majadiliano ya kuuza baadhi ya hisa zake kwa kampuni hiyo ya Kichina.
Taarifa ya kuwa kuna majadiliano imethibitishwa pia na ofisi za ABG Dar es Salaam katika andiko lake kupitia kwa msemaji wake, Nector Foya, linalothibitisha kuwa kampuni hiyo iko katika hatua ya awali ya majadiliano na kampuni hiyo ya China.
“Wakati huu hakuna uhakika kwamba majadiliano hayo yanaweza kufikia muafaka kutokana na kwamba bado ni mapema kwamba majadiliano yanaweza kukamilika iwapo CNGGC itachukua zaidi ya asilimia 30 za ABG, kulingana na soko la hisa la London (London Stock Exchange) ABG inathibitisha kuwa ina hisa paundi bilioni 4.1 katika soko la hisa.’’
Wakati ABG ikitoa ufafanuzi huo ripoti ya Mpango wa Uhamasishaji Uwazi kwenye Mapato ya madini, gesi asilia na mafuta (TEITI) iliyo chini ya Mwenyekiti Jaji Mark Bomani imeweka wazi kuwa kuna uwezekano kuwa ABG inaweza kuwa inadaiwa.
Ofisa mmoja wa TEITI anasema: “ Katika ripoti ya pili ya TEITI ya Julai 2009 mpaka Juni 2010, mapato yote ya Serikali yalikuwa bilioni 419 kutoka katika makampuni ya uchimbaji madini na gesi asilia na mafuta, katika mgawanyo huo ulipaji wa kodi kwa makampuni yote si mzuri, yanalipa asilimia saba tu, madai yao ni kwamba hayapati faida.”
Ofisa huyo anasema takwimu hizo ni kwa mujibu wa ripoti ya pili, “ tu naposubiri kuandaa ripoti ya nne ya mwaka wa fedha 2012/ 2013 hatuna hakika ikiwa kampuni hiyo unayozungumzia ya ABG imelipa kodi ya mapato kwa mwaka wa fedha 2011/ 2012.”
ABG ina migodi kadhaa nchini katika maeneo ya Tulawaka, Biharamulo mkoani Kagera; Buzwagi na Bulyanhulu, Kahama, Shinyanga na North Mara, Tarime mkoani Mara.
CHANZO: BOFYA HAPA
0 comments:
Post a Comment