Na Edson Kamukara
SIKU moja baada ya gazeti hili kuchapisha habari za baadhi ya wafanyakazi wa kigeni kuajiriwa katika hoteli kubwa za kitalii jijini Dar es Salaam kwa kazi ambazo zinapaswa kufanywa na wazawa, siri nzito zimeendelea kutobolewa jinsi wanavyopatiwa vibali kiaina.
Katika taarifa iliyochapishwa jana, ni kwamba wafanyakazi hao huletwa na ndugu zao wenye madaraka makubwa katika hoteli hizo bila kujali taaluma zao.
Katika orodha ya hoteli moja kubwa na maarufu iliyoko eneo la Kunduchi jijini hapa, inaonyesha kuwa na wafanyakazi wa kigeni 29 ambao takriban ni raia wa India ukiacha watendaji wachache wa juu kabisa.
Taarifa hiyo imewaibua wafanyakazi kadhaa kwenye kampuni na hoteli mbalimbali ambapo walipiga simu na wengine kufika chumba cha habari kuelezea kwa undani jinsi wageni hao wanavyoendelea kumiminika na kufanya kazi nchini kiujanjaujanja.
Mmoja wa viongozi wa juu wa hoteli ya kitalii iliyoko eneo la Kunduchi, alikiri kuwa madai hayo ni ya kweli lakini akasisitiza kuwa chimbuko la matatizo yote ni watendaji wa serikali walioko ndani ya Wizara mbili za Mambo ya Ndani na Kazi na Ajira.
“Mimi si msemaji wa hoteli kuhusu jambo hilo unaloliuliza lakini nikwambie kuwa anayeidhinisha sifa za wageni hao kama wana sifa au la ni mwajiri.
Pili watu hawa wako nchini kihalali wakiwa wameidhinishwa na serikali.
Mtoa taarifa huyo alipoulizwa kuhusu madai ya uongozi wa hoteli hiyo kutoa rushwa kwa maofisa wa serikali ili kuwalainisha wasiwasumbue wageni hao, alikiri ni kweli na kutamba: “Kama tunao uwezo huo wa kufanya hivyo kwa nini tusifanye?
“Hawa wafanyakazi wazalendo wanaolalamika kunyimwa haki madai yao ni ya kweli, lakini mfumo wa serikali yetu umevurugika kila vinapokuja vyombo vya dola hotelini tunamalizana,” alisema.
Chanzao hicho kilisisitiza kuwa wageni hao vihiyo wanaletwa nchini kwa maslahi ya wenye hoteli na kwamba serikali nayo ina maslahi yake ndiyo maana watendaji wake wanakuwa wepesi kumalizana nao.
“Mathalami wakaguzi wa Idara ya Uhamiaji walifika hotelini kwetu na nilifanikiwa kuwaeleza waziwazi kuwa udhaifu uko upande wao, lakini nao walipoingia ndani walipewa ‘chochote’ wakaondoka zao.”
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, wageni wanapaswa kufanya kazi ya kuhamisha teknolojia kwa wafanyakazi wazawa yaani kuwafundisha na wakiishamudu wao wanarudi kwao.
Wakati hali ikiwa hivyo kwenye hoteli, nao baadhi ya wafanyakazi wa kampuni moja ya Kichina iliyoko maeneo ya Shekilango, walifika ofisi za gazeti hili na kueleza namna wageni hao walivyojazana na kufanya kazi za kawaida zinazoweza kufanywa na Watanzania.
“Nafasi zote za utawala kwenye kampuni yetu ni Wachina na utashangaa kuona kwenye nafasi moja kuwa watu watatu hadi wanne. Sisi tumefanya hapo kwa muda mrefu sana, tuna elimu ya shahada hadi uzamivu lakini kila mara wanaletwa Wachina wenye elimu za kawadia na wanapewa nafasi kubwa za umemeja,” walisema.
Waliongeza kuwa wageni wanapewa ajira za muda mrefu halafu wazawa wanapewa mikataba ya mwaka mmoja.
Wafanyakazi hao walisema kuwa chanzo cha kujazana kwa Wachina hao nchini, ni udhaifu uliopo kwenye Wizara ya Kazi kiengo cha utoaji vibali, Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), kwamba hata viongozi wao hao wamekuwa wakijivuna jinsi wanavyowapa rushwa.
“Pale Wizara ya Kazi kuna mtu (wanamtaja) amekuwa tatizo, huyu ndiye anatoa vibali kiholela kwa rushwa, Wachina wanajivuna kwa hilo ndiyo maana wanawakusanya ndugu zao na kuwajaza hapa nchini,” walisisitiza.
Mfanyakazi huyo alipotafutwa kwa njia ya simu jana, alikanusha kuhusika na kuahidi kutoa taarifa kamili baadaye, akidai wafanyakazi hao wamekuwa wakichanganya mambo na kumhusisha kwenye tuhuma zisizomhusu.
Juhudi za kumpata Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emnamuel Nchimbi, na mwenzake wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, hazikuzaa matunda jana kutokana na simu zao kuita bila kupokelewa.
Vyanzo vyetu vilidokeza kuwa ili kukwepa mkono wa sheria za nchi kuhusu wageni kufanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania, baadhi ya wageni hao wamekuwa wakitumia majina tofauti badala ya yale yaliyoko kwenye pasi zao za kusafiria au nyaraka za Idara ya Uhamiaji.
CHANZO: BOFYA HAPA
CHANZO: BOFYA HAPA
0 comments:
Post a Comment