Mwenyekiti wa Kamati Ya Bunge Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Mbunge wa Monduli(CCM) Edward Lowassa
**==**
KAMATI ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imesema Tanzania imejiandaa kiakili na kivifaa kuingia vitani na Malawi kama italazimika kufanya hivyo.Akizungumza mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Edward Lowassa alisema kamati yake imeridhishwa na maandalizi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Tumepewa maelezo na jeshi letu na tumeridhika kuwa ikibidi kuingia vitani jeshi letu liko vizuri sana na limejipanga vizuri sana kwa uhakika, kiakili na kivifaa,” alisema Lowassa.
Kabla ya Lowassa kuzungumza na waandishi wa habari, alifanya kikao cha faragha kilichohusisha pia wajumbe wa kamati hiyo na makamanda wa JWTZ walipofika bungeni kutoa taarifa kwa kamati hiyo.
Hata hivyo, katika tamko hilo Lowassa alisema Tanzania inatarajia mgogoro huo utamalizika kwa njia za kidiplomasia kwa sababu Watanzania na Wamalawi ni ndugu wa muda mrefu.
“Ikibidi kuingia vitani jeshi letu liko vizuri sana na kama ilivyo ahadi yao (JWTZ), wako tayari kulinda mipaka ya nchi yetu hadi tone la mwisho. Tunasali sana tusifike hapo,” alisema Lowassa na kuongeza: “Tunategemea hatutafika huko, lakini kwa heshima ya nchi yetu kama ikibidi kufika huko (vitani) tutafika kulinda mipaka yetu”.
Mwenyekiti huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu, alisema kama Tanzania itafikishwa mahali itabidi damu ya Watanzania imwagike, nchi iko tayari kulinda mipaka yake kwa nguvu.Alisema kama itabidi kuingia vitani, itatumia umoja na mshikamano wa Watanzania wa mwaka 1978 wakati wa Vita na Uganda kulinda mipaka ili kulinda heshima ya nchi.
Alisema mwaka 1978 wakati Rais wa Uganda, Idd Amin na majeshi yake walipochukua sehemu ya Tanzania na kujitangazia ni mali yake, ilichukua hatua kumfukuza Amin.
“Alijitangazia sehemu ile ni mali ya Uganda hutegemei nchi ikae kimya, hutegemei Watanzania wanyamaze wakati nchi yao imetekwa, tulichukua hatua tukamfukuza hadi nchini kwake.”
Lowassa alisema Kamati ya Bunge inajua madhara ya kiuchumi yaliyotokana na Vita ya Idd Amin na kwamba vita yoyote ikipiganwa lazima kunakuwa na madhara ya kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment