SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, July 24, 2012

Taarifa ya Serekali Ikitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU KUZAMA KWA
MELI YA MV. SKAGIT


Ndugu Waandishi wa Habari,
Ndugu Wananchi, kama tunavyofahamu kwamba Meli ya MV. SKAGIT iliyokuwa ikifanya safari kutoka Dar es Salaam kuja Zanzibar tarehe 18 Julai, 2012 ilipata ajali katika eneo la karibu na Kisiwa cha Chumbe na kupelekea meli hiyo kuzama. Meli hiyo ilitengenezwa nchini Marekani mwaka 1989 na imesajiliwa Zanzibar tarehe 25 Oktoba, 2011 na kupewa nambari ya Usajili 100144, yenye uzito wa GRT96. Kampuni inayomiliki meli hiyo ni Seagull Sea Transport Limited ya Zanzibar.


Meli hiyo kikawaida inafanya safari zake baina ya visiwa vya Unguja na Pemba na Dar es Salaam. Siku hiyo ya tarehe 18 Julai, 2012 meli hiyo iliondoka Dar es Salaam majira ya saa 6.00 mchana kuelekea Zanzibar. Kwa mujibu wa Manifest ya abiria iliowasilishwa na wenye meli kwa mamlaka husika (TPA na SUMATRA), meli hiyo ilikuwa imechukua watu 290 kwa mchanganuo ufuatao:-


1. Abiria watu wazima - 250


2. Watoto - 31


3. Mabaharia - 9



Mnamo saa 7.30 mchana meli hiyo ilizama karibu na eneo la Kisiwa cha Chumbe takriban umbali wa maili 7 za baharini kufikia kisiwa hicho.


Ndugu Wananchi, Serikali kupitia vyombo vyake vya Bandari, ZMA na Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Kampuni Binafsi vilianza kuchukua hatua ya kwenda katika eneo la tukio kwa ajili ya kutoa huduma za uokozi. Mnamo majira ya saa 9.15 harakati za uokozi zilianza kwa kuokoa wananchi waliokuwa hai na baadae kuanza zoezi la kutafuta maiti.


Vyombo vingi vilishiriki kikamilifu katika jitihada za uokozi, ikiwemo Kilimanjaro 3, Tagi ya Bandari, Flying Horse, Helikopta za Jeshi la Wananchi na Polisi, Zanzibar One, Boti za KMKM ambazo pia zilikuwa na wazamiaji (divers).


Ndugu Wananchi, katika jitihada hizo jumla ya watu 146 waliokolewa wakiwa hai. Hadi kufikia jana jioni maiti zilizopatikana zilifikia 73, wakiwa wanaume 19, watoto 17 na wanawake 37. Kwa ujumla maiti nyingi zilitambuliwa na kukabidhiwa jamaa zao kwa ajili ya mazishi. Serikali iligharamia mazishi hayo kwa kutoa vifaa vya kuzikia. Jumla ya maiti 23 hazikuweza kutambuliwa na jamaa zao na hivyo iliamuliwa kuzikwa na Serikali katika makaburi ya Kama nje kidogo ya mji wa Zanzibar ili kuepuka kukaa zaidi na maiti hizo kuharibika. Jitihada zaidi zinaendelea kuchukuliwa na Serikali kutafuta miili iliyokuwa haijaonekana. Hata hivyo, kwa wakati huu imeamulika maiti zitakazopatikana kuanzia sasa zitapelekwa moja kwa moja katika eneo la Kama kwa ajili ya mazishi. Kutokana na hali hiyo na baada ya Masheikh kutoa Fat-wa, iliamuliwa kufungwa kwa kambi ya Maisara iliyokuwa ikitumika kwa ajili ya utambuzi wa maiti.


Ndugu Wananchi, kwa taarifa tulizonazo, miongoni mwa abiria waliokuwa katika chombo hicho, walikuwemo raia wa kigeni 17 na waliookolewa wakiwa hai 15, mmoja amepatikana akiwa amefariki na mmoja hajapatikana hadi sasa. Wageni hao ni kutoka Ubelgiji, Marekani, Ujerumani, Uholanzi na Israel. Serikali ilitoa huduma kwa wageni hao na tayari wameondoka kurudi makwao kwa salama.


Ndugu Wananchi, jitihada za kukitafuta chombo kilichozama zilifanyika kwa kutumia wataalamu wa uzamiaji kutoka Kikosi cha KMKM, Jeshi la Wananchi, Polisi pamoja na wazamiaji wa kujitolea wa Ki-Israel ambao wapo Nungwi. Wazamiaji wetu hawa walifika umbali wa mita 48 chini ya bahari lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kuiona meli hiyo. Hata hivyo, jitihada zinaendelea.


Ndugu Wananchi, nachukua fursa hii kuwaomba wananchi wote wanaoishi katika maeneo ya mwambao na wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya baharini watoe taarifa kwa Serikali katika maeneo yao pale wanapoona miili ya watu wanaosadikiwa kuwa ni abiria wa meli iliyozama. Aidha, wananchi wote waliopotelewa na jamaa zao ambao wanadhani walikuwa katika chombo hicho kutoa taarifa kwa masheha na wakuu wa wilaya au Vituo vya Polisi vilivyo karibu nao.


Ndugu Wananchi, Kati ya majeruhi 138 waliopelekwa hospitali ya Mnazi Mmoja hadi kufikia leo hii wagonjwa wote walikwisha ruhusiwa baada ya kupata matibabu katika hospitali.


Ndugu Wananchi, Serikali imehuzunishwa sana na tukio hili na imekusidia kuchukua hatua mbali mbali, ikiwemo kutoa mkono wa pole kwa wahusika na kuunda Tume ya Uchunguzi wa ajali hii. Aidha, Serikali iliagiza Mikoa yote kusoma hitma na dua za kuwaombea marehemu na waliopatwa na ajali hii.


Katika hatua ya kudhibiti majanga ya aina hii, Serikali inakusudia kuzifanyia mapitio sheria zinazohusu usafiri wa baharini na kuweka viwango vya aina ya meli zitakazoruhusiwa kuingizwa nchini na kuchukua abiria. Aidha, Serikali inakusudia kuendelea na juhudi zake za kununua meli zake kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri wa hakika kwa wananchi katika maeneo ya mwambao.


Ndugu Wananchi, napenda kuchukua nafasi hii kuyashukuru sana Makampuni binafsi na vyombo vya usafiri wa baharini kwa msaada na ushirikiano mkubwa waliotupa kuanzia mwanzo wa zoezi hili hadi mwisho. Lakini pia napenda kuzipongeza Kamati zetu za Maafa za Tanzania Bara kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na ile ya Zanzibar kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa kufanya kazi kwa pamoja kusimamia zoezi hili la uokozi.


Ndugu Wananchi, napenda pia kuwashukuru wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla wakiwemo wafanyabiashara mbali mbali kwa misaada yao mbali mbali walioitoa na vyombo vya habari kwa ushirikiano wao wakati wote wa tukio hili ambapo walikuwa wanawajulisha wananchi wetu hali inavyoendelea.


Vile vile, napenda kuwashukuru Viongozi wetu wakuu kwa ushirikiano wao mkubwa waliotupa katika maafa haya. Ambao ni:- Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa namna alivyoliongoza zoezi zima la uokozi na kupata mafanikio katika zoezi hili. Tunawashukuru Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu kwa kuja binafsi kutoa pole zao na kuwafariji waliookolewa wakiwa hai kwa kuwatembelea vitandani mwao Hospitali ya Mnazi Mmoja na pia kuwafariji wafiwa kwa kuzitembelea maiti zilizookolewa pale uwanja wa Maisara.


Namshukuru Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa karibu nami kwani tangu ajali ilipotokea tulikuwa tunawasiliana kwa simu na kwa mchango mkubwa aliotoa kutoka Ofisi yake.


Ndugu Wananchi, aidha, nawashukuru Mabalozi wa nchi mbali mbali waliokuja binafsi kutufariji na pia wale waliotupigia simu. Kwa kipekee namshukuru Balozi Mdogo wa China hapa Zanzibar ambaye tumekuwa naye bandarini mara tu ajali ilipotokea.


Mwisho kabisa, nawashukuru Mawaziri wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Wawakilishi kwa umoja na mshikamano wao waliotuonyesha tangu mwanzo wa ajali mpaka sasa. Inshallah Mwenyezi Mungu atujaalie tuendelee na mshikamano wetu huu kwa maslahi ya wananchi wetu.


Ndugu Wananchi, nawashukuruni sana kwa kunisikiliza.


Balozi Seif Ali Iddi
MAKAMU WA PILI WA RAIS,
ZANZIBAR.
23 Julai, 2012:
Chanzo:ZanziNews Blog

0 comments:

Post a Comment