SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Monday, April 23, 2012

WANAHARAKATI WATAKA MJADALA KUHUSU ULEVI UNAVYOCHANGIA UKATILI




Ananilea Nkya Mkurugenzi Mtendaji Tamwa
****
Viongozi wa mashiriki matatu  yanayotetea  haki za wanawake na watoto wamesema ni muhimu  wananchi mijini na vijijini wakaanza kujadili madhara ya ulevi na kuchukua hatua  kuepusha  vitendo vya ukatili vinavyosababishwa na ulevi.
 Wamesema bila jamii kuchukua hatua madhubuti kupambana na ulevi nchi itaendelea kushuhudia vitendo vya ukatili wa kijinsia  vinavyokosesha familia  amani  ambayo ni msingi  muhimu wa maendeleo ya familia na taifa.
Wamesema wanaume wanaokunywa pombe na kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wanaweza kubadilika endapo wananchi  katika ngazi za  vijiji, mitaa na kwenye  taasisi wangeanzisha mjadala kuhusu namna bora ya kupambana na ulevi.
 Viongozi hao  kutoka  Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC), Shirika la Haki za  Wanawake – KIVULINI na  Kituo cha Usuluishi (CRC) walisema hayo walipokuwa wakizungumza na TAMWA kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki.
 Wamesema  kwa mfano matukio mengi ya wanawaume kuwapiga wake zao, ubakaji, lugha za  kudhalilisha utu,  na wazazi kutohudumia watoto kwa kuwapatia  chakula, mavazi  na elimu  yanachangiwa na ulevi.
 Maimuna Kanyamala, Mkurugenzi wa  shirika la KIVULINI ambalo linaendesha kampeni ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake katika kanda ya Ziwa  amesema kupitia sinema na mijadala ya umma wanaume zaidi ya 350,000 katika kanda hiyo wamebadilika  na familia zao zinaishi kwa amani.
 Amesema watu hao waliweza kuacha pombe baada ya kuona sinema iliyoonyesha mambo maovu ambayo mtu anaweza kufanya kutokana na kunywa pombe.
 Mkurugenzi wa WLAC  Theodosia Muhulo Nshala na  Mratibu wa CRC  Elizabeth  Muhangwa wamesema  wanawake wengi   na watoto wanaofika katika mashirika  yao kutaka msaada wa ushauri na wa kisheria   ni wale ambao wamefanyiwa ukatili ambao kwa namna moja au nyingine umechochewa na  unywaji wa pombe. Viongozi wa mashirika hayo wameyataka mashirika yote ya kijamii yanayotoa msaada wa kisheria na ushauri kwa wanawake na watoto kuchunguza kwa kina mashauri wanayopokea ili kufahamu ni yepi yana uhusiano na pombe.
 Wamesema kwa kufanya hivyo nchi itaweza kupata takwimu sahihi kuhusu ni kwa kiasi gani unywaji pombe unavyochangia ukubwa wa tatizo la ukatili wa kijinsia.
       Imetolewa na: 
Ananilea Nkya
Mkurugenzi Mtendaji Tamwa

0 comments:

Post a Comment