SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, January 20, 2012

Rais Jakaya Kikwete Atuma Salaam Za Rambimrambi Kufwatia Kifo Cha cha Mhe. Jeremia Solomon Sumari,Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa Tiketi ya CCM na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
-------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda (Mb.,) kutokana na kifo cha Mhe. Jeremia Solomon Sumari, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la
Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CCM na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 19 Januari, 2012 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa
matibabu.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Jeremia Solomon Sumari kwani alikuwa kiongozi aliyewatumikia vema wananchi wa Jimbo lake la Uchaguzi la Arumeru Mashariki na Taifa kwa ujumla katika wadhfa wake wa Waziri kwa umahiri na uhodari mkubwa”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake.
Rais Kikwete amesema kutokana na kifo chake, wananchi wa Arumeru Mashariki
wamepoteza kiongozi wa kutegemewa sana huku Taifa likiachwa na pengo kubwa ambalo si rahisi kuzibika ikizingatiwa kwamba alikuwa kiongozi katika Wizara ambayo ni mhimili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
“Kwa dhati ya moyo wangu, natuma salamu za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya Marehemu Jeremia Sumari kwa kumpoteza kiongozi na mhimili madhubuti wa familia. Ninawahakikishia kwamba nipo pamoja
nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa, na namuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema aipumzishe roho ya Marehemu Jeremia Solomon Sumari mahali pema peponi, Amina”, ameongeza kusema Rais Kikwete.
Ameiomba familia ya Marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni mapenzi yake mola.
Imetolewa na
Kurugenzi Ya Mawasiliano
IKULU
19 Jan 2012

0 comments:

Post a Comment