SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, June 17, 2011

RAIS KIKWETE AGUSWA NA UPUNGUFU WA AJIRA MIONGONI MWA VIJANA BARANI AFRIKA!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa kwenye mkutano wa ILO Geneva, Uswiss.
*************************************
Upungufu wa ajira hususan miongoni mwa vijana ni changamoto kubwa kwa nchi zinazoendelea kwa sababu ya uchumi wake kuwa mdogo na kukua polepole.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameyasema hayo Jumatano wiki hii (15 Juni, 2011) wakati wa hotuba yake katika kikao cha 100 cha Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika makao makuu ya shirika hilo mjini Geneva, Uswiss.
Tunahitaji kutatua tatizo la ajira ambalo linaongezeka, hasa kwa vijana katika nchi zinazoendelea,ili kulitatua kwa umakini zaidi juhudi za pamoja  zinahitajika baina ya  serikali, jumuiya za wafanyabiashara wa kitaifa na kimataifa, mashirika ya kiraia na washirika wetu wa kimaendeleo”, Amesisitiza na kufafanua kuwa  “ Kwa ushirikiano baina ya pande zote kasi ya kuongeza na kutengeneza ajira  inahitajika katika nchi zinazoendelea”.  Rais Amesema.
Mara baada ya kuhutubia mkutano huo, Rais pia alipata nafasi ya kuzungumza na viongozi na wawakilishi wa nchi za Afrika waliohudhuria Mkutano huo.
Alisisitiza kuwa nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto ya ajira na kwamba kwa pamoja ushirikiano wa kikanda unahitajika kupitia jumuiya mbalimbali za kiuchumi barani Afrika kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Soko la pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA), Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na nyingine ambazo kwa pamoja zinaweza kupanua ajira na kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi kwa bara la Afrika.
Shirika la Kazi Duniani ni shirika ambalo huendesha shughuli zake kwa kanuni ya utatu ambapo hujumuisha viongozi wa kiserikali, viongozi wa vyama vya waajiri na vyama vya wafanyakazi duniani na ujumbe wa kila nchi huhudhuria vikao hivi kwa kuzingatia utatu huu.
Katika hatua nyingine Rais Kikwete amewaeleza mabalozi, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na waajiri barani Afrika juu ya makubaliano makuu matatu ya  jumuiya tatu za EAC, COMESA na SADC katika kikao chao kilichofanyika mwishoni mwa juma lililopita nchini Afrika ya Kusini, kuwa viongozi hao waliazimia kwa pamoja kuunda muungano mkubwa wa soko huru (Free Trade Area) kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Maeneo hayo ni kukuza masoko baina ya nchi hizi, miundo mbinu na nishati.
Rais amesema maendeleo haya yanalenga katika kukuza uchumi na hatimaye kuongeza na kutengeneza ajira zaidi.
Rais Kikwete pia ametoa changamoto kwa wananchi wa Afrika kuacha kuwa wanyonge na kudharau maendeleo yaliyokwisha patikana katika nchi zao, amesema inasikitisha kuona  Waafrika wanaongea kwa kujidharau na kujidhalilisha wenyewe bila hata kuona kufanya hivyo ni kujikosea binafsi.
Tunahitaji kuwa wazalendo na pia kuwa na matumaini na bara letu na juhudi zetu katika kujiletea maendeleo na sio kujidharau wenyewe” Rais amewaasa wawakilishi wa Afrika.
Rais Kikwete amerejea jijini Dar-Es-Salaam jana (16 Juni 2011) jioni.
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi.
Geneva-Uswiss.
17 Juni, 2011

0 comments:

Post a Comment