SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, May 27, 2011

VIASHIRIA VYAONYESHA TANZANIA KUTIMIZA LENGO LA 4 LA MILENIA IFIKAPO 2015!!

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Mh. Dk. Haji Hussein Mponda akiwaelezea waandishi wa habari kuhusu moja ya malengo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa 2010 ambao amezindua rasmi ripoti yake leo; ambapo amesema ni kutoa taarifa zitakazo wezesha kufuatilia na kutathmini mahitaji ya huduma za afya, uzazi wa mpango na mikakati ya kupambana na virusi vya ukimwi na ukimwi.
Mfululizo wa picha ni baadhi ya wadau wa maendeleo ya afya ya uzazi na mtoto pamoja wawakilishi wa mashirika ya misaada ya maendeleo ya Marekani (USAID) na Uingereza (DFID) katika uzinduzi wa ripoti hiyo.
Mh. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Mh. Dk. Haji Hussein Mponda (waliokaa mstari wa mbele katikati) katika picha ya pamoja na maofisa wa serikali, wawakilishi kutoka USAID na DFID, mashirika ya Umoja wa mataifa, Benki ya Dunia, Macro international na wadau wengine wa maendeleo waliohudhuria uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa 2010 uliofanywa leo jijini Dar es Salaam.
*************
 Matokeo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa Mwaka 2010 nchini Tanzania pamoja na kutoa viashiria kadhaa kikubwa zaidi yanaonyesha kuwa lengo la Milenia namba nne(4) la kupunguza vifo vya watoto, sekta ya Afya litatimia ifikapo mwaka 2015.
Akizindua Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa Mwaka 2010 jijini Dar es Salaam leo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Mh. Dk. Haji Hussein Mponda (Mb) amesema katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2006/2010 kiwango cha vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano kimepungua kwa asilimia 40.
Kiwango hicho kimepungua kutoka vifo vya watoto 137 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai hadi kufikia vifo vya watoto 81 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai na katika kipindi hicho pia kiwango cha vifo vya watoto wachanga kimepungua kutoka vifo vya watoto 88 hadi kufikia vifo 51 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai.
Kwa mujibu wa lengo namba 4 la Milenia ifikapo mwaka 2015 Tanzania inatakiwa ipunguze vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kufikia 64 kwa kila hai 1,000 na waliochini ya mwaka mmoja lengo ni vifo 38 kwa kila waliozaliwa hai 1,000.
Mh. Dk. Mponda amesema utafiti huo ulikuwa na malengo mengi, lakini lengo kuu lilikuwa kukusanya takwimu zenye ubora wa hali ya juu kuhusiana na viwango vya uzazi; upendeleo wa jinsia na idadi ya watoto; matumizi ya uzazi wa mpango; afya ya uzazi na ahya ya mama na mtoto.
Amefafanua kuwa malengo mengine ni kukusanya takwimu za hali ya lishe kwa watoto na akina mama; kiwango cha vifo vya watoto; umiliki na utumiaji wa vyandarua; magonjwa ya watoto na tiba; ufahamu na tabia kuhusiana na virusi vya Ukimwi na Ukimwi; vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi; kiwango cha damu; kiwango cha madini joto na madini chuma; vitamin A na ukatili wa kijinsia.
Mfululizo wa picha ni baadhi ya wadau wa maendeleo ya afya ya uzazi na mtoto pamoja wawakilishi wa mashirika ya misaada ya maendeleo ya Marekani (USAID) na Uingereza (DFID) katika uzinduzi wa ripoti hiyo. 
Na Mo Blog. 

0 comments:

Post a Comment