SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, October 13, 2010


Kambi ya Simba hofu tupu
Na Erasto Stanslaus
HALI si shwari ndani ya kambi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom, Simba baada ya kutokuwa na uhakika wa kuwatumia wachezaji wake muhimu katika mchezo wao dhidi ya watani wao wa jadi Yanga, utakaochezwa Jumamosi hii, Oktoba 16 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Daktari wa timu hiyo, Cosmas Kapinga, aliliambia Championi Jumatano kuwa, kuna uwezekano mkubwa katika mchezo huo kuwakosa baadhi ya wachezaji kutokana na kuwa majeruhi.
Kapinga aliwataja wachezaji ambao wana hatihati ya kucheza katika mchezo huo kuwa ni Mussa Hassan Mgosi, Hilary Echessa, Ali Mustapha ‘Bathez’ na Patrick Ochan.
Mgosi na Echessa waliokuwa majeruhi walipata nafuu lakini waliumia tena katika mechi za kirafiki mwanzoni mwa wiki hii. Kapinga alisema wametonesha magoti yao ambayo yalikuwa yanawasumbua kwa muda mrefu huku Ochang akiumia juzi asubuhi alipokuwa mazoezini wakati Bathez anasumbuliwa na malaria.
Kapinga alisema kikosi hicho kimekuwa kikiandamwa na majeruhi lakini wachezaji wengine wanaweza kucheza mchezo huo muhimu kutokana na hali zao kutokuwa mbaya.
Aliwataja wachezaji wengine majeruhi lakini wana uwezo wa kucheza ambao ni Juma Kaseja na Mohamed Banka, waliojiunga na timu baada ya kumaliza mchezo dhidi ya Morocco.
“Tunafanya jitihada za dhati kuhakikisha wachezaji hao wanakuwa vizuri katika mchezo huo kutokana na umuhimu wao katika kikosi hicho,” alisena Kapinga.

0 comments:

Post a Comment