Wapenzi wa jinsia moja hawateswi Cameroon
Serikali ya Cameroon imekana
madai ya mtu anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja anayetafuta hifadhi
Uingereza kuwa atateswa iwapo atarudi kwao.
Siku ya Jumatano, mahakama kuu ya London
ilimkubalia mtu huyo kubaki Uingereza pamoja na mwengine kutoka Iran.
Adhabu inayotolewa kwa wapenzi wa jinsia moja
nchini Cameroon ni hadi miaka mitatu jela.
Hata hivyo, waziri wa mawasiliano wa Cameroon
ameiambia BBC kuwa watu hao wanaruhusiwa kufanya vyovyote kwa faragha
bila kubughudhiwa na yeyote.
Waziri wa mawasiliano Issa Tchiroma amesema, "
Mapenzi ya jinsia moja yanakatazwa kwa mujibu wa sheria, hilo halina
shaka. Lakini naweza kusisitiza kwamba hakuna hata mmoja aliyefanya
mapenzi hayo akateswa hapa Cameroon."
Ameiambia BBC kwamba mtu huyo ametumia tu sheria
hiyo ili aweze kupata hifadhi Uingereza.
"Unadhani yeye ndiye mtu peke anayefanya mapenzi
ya jinsia moja Cameroon."
'Watu wenye hasira'
Watu hao wawili ambao sasa wameshinda kesi na
kupata hifadhi ya kubaki Uingereza walikataliwa ombi lao hilo na
serikali iliyopita ya Uingereza.
Uamuzi huo uliungwa mkono na mahakama ndogo, kwa
minajili ya kwamba wanaweza kuepuka kuteswa iwapo wataficha jinsia yao
au kufanya mapenzi hayo kwa siri.
Lakini mahakama kuu imeamua kuwa ni ukiukaji wa
haki za binadamu.
Mtu huyo kutoka Cameroon, ambaye anatambuliwa tu
kama HT, aliambiwa ahame eneo jingine nchini humo na afanye shughuli
zake kwa siri.
Alishambuliwa na watu wenye hasira huko nyumbani
baada ya kuonekana akimbusu mwenzake. Amekuwa akihangaika kubaki
Uingereza katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Awali HT aliiambia BBC, "Watu wengine
walinisimamisha na kusema "tunajua wewe unashiriki mapenzi ya jinsia
moja'.
" Siwezi kurudi na kujificha au kudanganya
kuhusu jinsia yangu. Nikirudi nyumbani nitaishi kwa hofu."
HT na mwenzake kutoka Iran, nchi ambayo hutoa
adhabu ya kifo kwa wapenzi wa jinsia moja, sasa kesi zao zitapitiwa na
mahakama za uhamiaji.
Mwandishi wa BBC Randy Joe Sa'ah huko Cameroon
amesema mbali na mawakili wachache na mwimbaji maarufu wa nchi hiyo
Petit Pays, hakuna makundi yeyote yanayotetea haki za watu wa jinsia
moja nchini humo. bbc swahili
0 comments:
Post a Comment