Mwanariadha wa Afrika Kusini Castor Semenya
amepata idhini kutoka shirikisho la riadha duniani IAAF kurejea
kushiriki mashindano ya riadha kama mwanamke.
Semenya mwenye umri wa miaka 19, hajashiriki
mashindano yoyote katika muda wa karibu mwaka mmoja kutokana na utata
kuhusu jinsia yake, na amekuwa akisubiri matokeo ya kubaini ikiwa ni
mwanamme au ni mwanamke.
Utata huo ulizuka Agosti mwaka uliopita kwenye
mashindano ya mbio za ulimwengu mjini Berlin wakati Semenya aliposhinda
mbio za mita 800 kwa wanawake huku akimwacha mpinzani wa karibu kwa
zaidi ya mita 20.
Kufuatia utata huo ambao pia ulikuwa umejitokeza
kwenye mashindano ya riadha kwa vijana barani Afrika, IAAF iliagiza
uchunguzi kufanyika kubaini jinsia ya Semenya ili kuamua ikiwa
ataruhusiwa kuendelea kushindana kama mwanamke.
Taarifa kutoka IAAF imethibitisha uamuzi huo wa
kumpa idhini Semenya kuendelea kushiriki katika mashindano ya riadha
kama mwanamke, baada ya kamati ya wataalamu wa afya kukamilisha
uchunguzi wake.
Taarifa hiyo imesema, ''Mchakato ulioanzishwa
mwaka 2009 kuhusu Castor Semenya umekamilika. IAAF inakubali kauli ya
kamati ya wataalamu wa afya kwamba anaweza kuanza kushiriki mashindano
ya riadha mara moja.''
Hata hivyo taarifa hiyo imesema maelezo ya afya
kuhusu jinsia ya Semenya yatabakia kuwa siri, na IAAF haitasema chochote
kuhusu swala hilo.
Kufuatia idhini hiyo Semenya anaweza kuamua
kushiriki mashindano ya kimataifa ya vijana nchini Canada baadaye mwezi
huu, lakini huenda akapendelea kuanza kujiandaa kwa michezo ya Jumuiya
ya Madola itakayofanyika mjini New Delhi, India mwezi Oktoba.
Mjini Berlin Semenya alishinda mbio za mita 800
kwa muda wa dakika moja sekunde 55.45, na kumwacha kwa karibu mita 20
aliyekuwa bingwa wa dunia wakati huo Janeth Jepkosgei kutoka Kenya.
Rekodi ya dunia ya mbio za mita 800 ni dakika
moja sekunde 53.28 iliyowekwa na Jarmila Kratochvilova wa Jamhuri ya
Czech mwaka 1983 na haijapata kuvunjwa tangu wakati huo.
Kuidhinishwa kwa Semenya kuendelea kushiriki
mbio za mita mia nane kama mwanamke huenda kukatoa fursa ya rekodi hiyo
kuvunjwa. bbc swahili.
0 comments:
Post a Comment