Waziri wa Misaada ya Maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel.
Mwanzoni mwa karne hii,Umoja wa Mataifa
ulijiwajibisha kupunguza kwa nusu umasikini, kote ulimwenguni ifikapo
mwaka 2015. Lakini yadhihirika kuwa ni vigumu kulitekeleza lengo hilo.
Hata katika sekta za afya na elimu ni hali hiyo hiyo, kwani wakati huu
wa mizozo ya fedha na uchumi duniani, wafadhili wengi, ikiwemo pia
Ujerumani, hawatoweza kutimiza ahadi za kusaidia kifedha.
Mwaka huu wa 2010, serikali ya Ujerumani inatenga
takriban Euro bilioni sita kwa ajili ya misaada ya maendeleo. Hicho ni
kiwango kikubwa lakini ni dhahiri kuwa mwaka huu, serikali ya muungano
wa vyama vya kihafidhina na kiliberali haitoweza kutimiza ahadi ya
serikali iliyotangulia - yaani kutoa asilimia 0.51 ya pato jumla la
ndani. Msaada utakaotolewa huenda ukafikia asilimia 0.4 tu.
Hiyo haifurahishi lakini mtu anapaswa kufahamu kuwa
Ujerumani haina budi kurekebisha bajeti yake iliyoathirika kutokana na
msukosuko wa kiuchumi uliotokea kote duniani. Hayo alitamka Dagmar
Wöhrl, mwenyekiti wa kamati ya bunge inayohusika na masuala ya maendeleo
na ushirikiano wa kiuchumi. Katika mwaka huu wa 2010 pekee, Ujerumani
itakuwa na deni jipya la Euro bilioni 80.Akaongezea:
" Sisi wenyewe tukiwa katika hali ya udhaifu basi
hatuwezi tena kuwasaidia wengine."
Lakini, msemaji wa chama cha SPD Sascha Raabe,
anayeshughulikia masuala ya misaada ya maendeleo, amelalamika kuwa
waziri wa maendeleo Dirk Niebel wa chama cha kiliberali cha FDP anatenga
kifungu kidogo sana cha fedha kwa ajili ya miradi ya kimataifa.
Amesema:
" Yeye anataka kutoa theluthi mbili ya fedha hizo,
ili Ujerumani iweze kuweka muhuri wake katika kila mradi kote duniani.
Kwake, ufanisi si kuboresha hali ya walio masikini kabisa bali ni kupata
kandarasi zaidi kwa biashara ya Ujerumani."
Ukweli ni kwamba waziri wa maendeleo ameanzisha
mkondo mpya. Msingi ni kuwepo ushirikiano zaidi katika sekta ya uchumi -
yaani katika siku zijazo,serikali ishirikiane zaidi na makampuni ya
binafsi.
Kwa upande mwingine, Wöhrl anasema si wafadhili tu
wanaohimizwa. Hata nchi zinazoendelea yaani zile zinazopokea misaada ya
maendeleo, zinawajibishwa zaidi kuliko hapo awali, kwani sekta ya kilimo
haikushughulikiwa ipasavyo na nchi hizo, tangu miongo kadhaa.
Hata hivyo,rasmi serikali ya Ujerumani inaazimia kutimiza lengo la
kuongeza mchango wake wa msaada wa maendeleo hadi asilimia 0.7 ya pato
jumla la ndani, ifikapo mwaka 2015.
Mwandishi:Fürstenau,Marcel/ZPR/P.Martin
0 comments:
Post a Comment