MBUNGE wa Makunduchi Zanzibar, Abdisalaam Issa Khatib (70), amedai
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwamba Ikulu ilitoa ridhaa ya
kuendelea na mchakato wa kumpata mzabuni wa ukaguzi wa dhahabu.
Khatib, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Fedha 1995-2008, alidai hayo
jana alipokuwa akijibu swali la wakili wa upande wa utetezi, Herbert
Nyange, katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi inayowakabili mawaziri
wa zamani; wa Fedha, Basil Mramba, wa Nishati na Madini, Daniel Yona na
aliyekuwa Katibu Mkuu Hazina, Gray Mgonja.
Nyange alimhoji shahidi huyo wa saba wa upande wa Jamhuri ambaye
alidai alikaimu nafasi ya Waziri wa Fedha Mei 2003, baada ya kumwonesha
barua iliyoko mahakamani kama kielelezo, ambayo inadaiwa Yona
alimwandikia Rais akimwelezea mchakato wa kumpata mzabuni huyo na Rais
kujibu kwa kuandika kwa kalamu “nakubali endeleeni haraka”.
Baada ya kumwambia asome maneno hayo, alimuuliza kama Rais akipokea
ushauri wa Waziri Yona na kuufanyia kazi, uamuzi huo utakuwa ni wa nani
kati ya Rais na Waziri, Khatib alijibu kuwa utakuwa wa Rais.
Wakati huo Rais alikuwa Benjamin Mkapa. Hata hivyo, kulingana na
kauli hiyo, Mahakama ilihoji ili kujiridhisha kama kauli hiyo ilikuwa
ikimaanisha nini na kuna uthibitisho gani kwamba uamuzi unakuwa wa Rais,
Khatib alijibu kama Rais amekubali na amesaini, moja kwa moja ni uamuzi
wake Rais.
Khatib pia alijibu kwamba hakuwahi kuona barua iliyoandikwa na Yona
kwenda kwa Rais na jibu alilotoa Rais, hata hivyo alikiri hakuna shida
yoyote kama Waziri ataamua kufanya mawasiliano na Rais bila kupitia kwa
waziri mwingine.
Khatib awali alidai akiwa katika nafasi aliyokuwa akikaimu, Mei 17,
2003, alimwandikia barua Waziri Yona, akitoa ushauri kama wizara yake
ilivyoombwa na Wizara ya Nishati na Madini kuhusu mchakato wa kupata
mzabuni wa kufanya ukaguzi wa madini.
Katika kumjibu, Yona aliandika akitaka mchakato wa kuipata kampuni
itakayofanya kazi hiyo usimame mpaka watakapokwenda wataalamu katika
sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, kujifunza na kupata uzoefu kuhusu
ufanyaji kazi na gharama zake, ili watakaporudi waweze kupata kampuni
inayostahili.
Ushauri huo ulioandaliwa na Khatib baada ya kupata ushauri kutoka
jopo la wataalamu waliokuwa katika wizara hiyo ulipomfikia, Yona alijibu
Mei 20, 2003 akimfahamisha, kwamba kuna barua aliyoipata kutoka Ikulu
ikitoa maelekezo kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, kulingana na kielelezo kilichotolewa mahakamani hapo
kikidaiwa kuwa ni barua iliyokuwa ikitoka kwa Yona kwenda Ikulu, Yona
alijibiwa aendelee kabla hajaomba ushauri wa Wizara ya Fedha.
Nyange alimwuliza Khatib: “Ushauri wako kwa Yona ulikuwa na manufaa
yoyote wakati Rais ambaye ni bosi wenu alikuwa ameshaamua?” Khatib
alijibu kuwa hakujua hilo na kama angejua kama Rais alishaamua,
angewarejea wataalamu na kuwaeleza ili kujua wajibu ulikuwa nini, akadai
“nisingeweza kubadili uamuzi wa Rais.”
Shahidi wa nane katika kesi hiyo, Immanuel Mahendeka kutoka Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), alidai kuwa kampuni ya Alex Stewart
(Assayers) Government Business Corporation, haikulipa kodi katika
kipindi chote tangu iliposajiliwa na TRA Oktoba 3, 2003 na kama
ingelipa, Serikali ingepata Sh bilioni 11.7 kuanzia 2004 hadi 2007.
Kesi hiyo iliyoko mbele ya jopo la mahakimu wakiongozwa na Hakimu
John Utamwa; Mramba, Yona na Mgonja wanadaiwa kuruhusu kutolewa kibali
cha Serikali kilichoisaidia kampuni hiyo kutolipa kodi tofauti na
mapendekezo ya TRA, uamuzi ulioisababishia Serikali hasara ya Sh
11,752,350,148 kati ya mwaka 2002 na Mei 2005.
Kampuni hiyo inadaiwa kuidhinishwa kusimamia ukaguzi wa dhahabu
nchini kwa ‘kubebwa’ bila kuzingatia ushauri na kuisababishia Serikali
hasara ya mabilioni ya fedha. Kesi hiyo inaendelea leo.
Imeandikwa na Regina Kumba-Habari Leo.
Thursday, May 27, 2010
'Rais Mkapa alimruhusu Yona'
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Thursday, May 27, 2010
Email This
BlogThis!
Share to X
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment