MTOTO Nassib Mpamka (15), anayetuhumiwa kufanya jaribio la kulipua
Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Mpamka alifikishwa mahakamani hapo saa mbili asubuhi na kuwekwa
chumba cha maulizo akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa Polisi.
Haikufahamika anakabiliwa na mashitaka gani kwa kuwa maofisa wa
mahakama walidai jalada lake lilihamishiwa mahakama ya watoto na
mashauri yake hayaruhusiwi kuripotiwa katika vyombo vya habari.
Kwa kawaida mahakama hiyo ya watoto hufanya shughuli zake asubuhi na
kumalizika kabla ya saa tatu ili kuruhusu watoto hao kuhudhuria masomo.
Ofisa mmoja wa Polisi aliyevaa nguo za kiraia, alionekana akimchukua
Mpamka kutoka chumba cha maulizo kilichopo katika mahakama ya kawaida
na kumpeleka katika chumba kimoja kilichopo katika jengo ambalo mahakama
ya watoto hufanyia shughuli zake.
Alipotoka katika chumba hicho, alirudishwa tena katika mahakama ya
kawaida na taarifa kutoka ndani ya mahakama hiyo zilidai kuwa, Mpamka
alikuwa akitafutiwa hakimu wa kusikiliza mashitaka yake baada ya kukosa
hakimu katika mahakama ya watoto ambako ndiko jalada lake liliko.
Haikuweza kufahamika mara moja kama alisomewa mashitaka hayo au la,
kwa kuwa hakuna aliyekuwa tayari kueleza kinachoendelea kuhusu mtuhumiwa
huyo.
Kwa kawaida kesi za watoto zinaendeshwa kwa usiri na si wazi kama
zilivyo kesi za kawaida. Taarifa kutoka chanzo chetu ndani ya Polisi
zilieleza kuwa alipelekwa katika mahabusu ya watoto iliyoko Upanga, Dar
es Salaam.
Kwa mujibu wa madai ya Polisi, Mpanga alifanya jaribio hilo baada ya
kuhamasika na mahubiri ya shehe wa msikiti wa Mtambani na kwamba wazo
la kulipua ubalozi huo alikuwa nalo tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna wa Polisi, Peter
Kivuyo alikaririwa na vyombo vya habari akisema mtuhumiwa huyo
alibainisha kuwa shehe huyo ambaye mpaka sasa hajatajwa jina, alikuwa
akihubiri mara kwa mara kuhusu vitendo vya majeshi ya Marekani kuwaua
Waislamu katika nchi mbalimbali duniani.
Kivuyo alisema wanahojiwa watuhumiwa wawili, yaani Mpamka na
mwenzake Amani Thomas (15), ambaye pia ni mwanafunzi wa kidato cha pili
katika shule ya sekondari Biafra.
Mei 16 saa 2:30 usiku, Mpamka alidaiwa kufika katika viunga vya
ubalozi huo katika eneo ambalo linaegeshwa magari ya kubebea maji na
kurusha chupa iliyokuwa imejazwa mafuta ya taa na kuwekwa utambi kwa
lengo la kulipua magari hayo.
Kutokana na juhudi za walinzi wa ubalozi huo waliokuwa kazini,
walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo na kumfikisha Polisi kwa mahojiano
zaidi.
habari Leo.
Thursday, May 27, 2010
Mtoto aliyetaka kulipua ubalozi afikishwa kortini
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Thursday, May 27, 2010
Email This
BlogThis!
Share to X
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment