KUNA taarifa kwamba, polisi wamemkamata mlinzi wa sekondari ya Aboud
Jumbe, Kigamboni, Shemsa Mpelela (22), anayetuhumiwa kuchoma moto nyumba
na kuua watu watano wa familia moja.
Sambamba na kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo wa mauaji, jana vilio
vilitawala kutoka kwa mamia ya watu waliohudhuria maziko ya watu hao
watano yaliyofanyika Tungi, Kigamboni, Dar es Salaam.
Walioteketea kwa moto wakiwa katika nyumba yao yenye chumba kimoja
ni baba mwenye nyumba John Onesmo (32) ambaye ni mfanyabiashara wa
samaki eneo la Feri, Catherine Jackson (25) anayefanya biashara ndogo,
watoto wao Oliver (2) na Joyce John (5) na Esther Mugulu (20) ambaye ni
mdogo wa Catherine, aliyekuwa na uhusiano wa kimapenzi na Shemsa na
kutokana na ugomvi baina yao, alidaiwa kuchoma nyumba hiyo ya chumba
kimoja.
Taarifa zilizopatikana jana eneo la msiba zilidai kuwa juzi Shemsa
alikwenda kwa kaka yake eneo la Kigamboni, Kisiwani, kuomba nauli ili
aondoke Dar es Salaam ndipo watu walipomwona na kutoa taarifa Polisi
ambao walimkamata huku umati wa watu ukishuhudia.
“Watu walimwona mtuhumiwa na kutoa taarifa Polisi na wao kwenda
kumkamata na polisi waliwahi na kumkuta eneo la Sido Kigamboni saa 4
asubuhi huku wananchi tukishuhudia,” alisema binamu wa John, Majuto
Daudi.
Habari hizo zilizozagaa eneo hilo la msiba, zilibainisha kuwa mbali
na kukamatwa kwa Shemsa, pia Polisi iliwakamata marafiki wawili wa
mtuhumiwa huyo, akiwamo anayedaiwa kushirikiana naye kuchoma moto nyumba
hiyo na kusababisha vifo.
Inadaiwa Jumatatu rafiki wa mtuhumiwa ambaye jina lake
halikufahamika, aliropokwa kijiweni kuwa mtuhumiwa huyo siku ya tukio
alikwenda nyumbani kwa John na kumtaka amtoe mpenzi wake, lakini John
licha ya kukubali kuwapatanisha alikataa kumtoa akidai kesi
imeshafikishwa polisi na ndipo Shemsa alipokasirishwa na usiku wake
kuamua kuchoma nyumba.
“Rafiki yake alisema mtuhumiwa alikuwa akinunua lita moja moja za
petroli na zilipofika lita 10 alimwomba rafiki yake amsindikize, lakini
rafiki huyo hakujua tendo alilokuwa anakwenda kufanya na ndipo
aliposhangazwa kuona mwenzake akichoma nyumba na wakaondoka eneo la
tukio haraka na kukaa mbali huku wakishuhudia nyumba inavyoteketea
aliposema hivyo, polisi jamii walimkamata na kuita askari Polisi,”
alidai Daudi.
Mwenzake mwingine aliyekamatwa na Polisi ambaye ni mchunga ng’ombe
anadaiwa kumficha Shemsa sehemu anakoishi Kigamboni tangu Ijumaa
alivyomchoma kisu mchumba wake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime, alipoulizwa,
hakupinga wala kukubali kama mtuhumiwa huyo amekamatwa.
“Siwezi kuzungumza na mwandishi kwa njia ya simu, taarifa zangu
nazitoa kwa maandishi tu ukitaka taarifa zangu njoo ofisini nikupe kwa
maandishi,” alisema.
Hata alipoombwa na mwandishi kutokana na muda ulivyokuwa umekwenda
na foleni barabarani kuwa kubwa, hivyo mwandishi angechelewa kufika
ofisini kwake, Kamanda huyo alikataa na kukata simu.
Gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu,
Suleiman Kova, hakupatikana hadi tunakwenda mitamboni.
Katika hatua nyingine, vilio vya umati wa waombolezaji jana
waliofurika nyumbani kwa baba yake John, Onesmo Magandu, kulipofanyika
maziko, vilisikika na kulifanya eneo la mtaa huo kuzizima huku watu
wakimlaani mtuhumiwa aliyefanya mauaji hayo.
Miili ya marehemu iliwasili nyumbani kwa Onesmo saa 9 alasiri na
sala ya kuwaombea iliongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Anglikana wa
Tungi, Obed Ntigogozwa na baadaye majeneza yote matano yalipelekwa
kuzikwa eneo la makaburi la Vijibweni.
Hata hivyo miili ya marehemu hao haikuoneshwa, kutokana na
kuharibika kwa moto na watu kutopita mbele ya majeneza hayo kutoa
heshima za mwisho.
Akitoa mahubiri wakati wa sala ya kuwaombea marehemu, Mchungaji
Ntigogozwa, alisema tukio hilo linaonesha watu walivyobadilika na
kugeuka wanyama, matukio ambayo hutokea siku za mwisho wa Dunia.
“Tukio hili litufanye tuone tunaishi siku za mwisho, tunaishi na
watu ambao si watu ingawa kwa mwonekano utafikiri ni watu … viongozi nao
wanapotaka uongozi wanakwenda kwa waganga na kuua albino, sasa hivi
waganga wanaharibu Taifa na tunakuwa na viongozi mbumbumbu. Waganga
wakamatwe kama majambazi,” alisema.
Katibu wa CCM wa Wilaya ya Temeke, Saad Kusilawe, aliyehudhuria
maziko hayo akifuatana na Mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo na
Diwani wa Vijibweni, Lucy Kanyopa, aliwataka wananchi kuepuka dhana ya
kujichukulia sheria mkononi. Chama hicho kilitoa rambirambi ya Sh
100,000.
Shemsa anadaiwa kuchoma nyumba ya John na familia yake usiku wa
kuamkia Jumatatu wiki hii na kuua watu wote
Na Maulid Ahmed-Habari Leo
****************************
Waombolezaji wakiwa kwenye ibada Tungi Kigamboni kuwaombea
watu watano wa familia moja waliokufa kwa kuchomwa moto ndani ya nyumba,
Kigamboni, Dar es Salaam. (Picha na Mroki Mroki).
Thursday, May 27, 2010
'Muuaji' aomba nauli atoroke Dar es Salaam
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Thursday, May 27, 2010
Email This
BlogThis!
Share to X
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment