SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, July 4, 2014

BALOZI IDDI AUAGIZA UONGOZI WA UWANJA WA NDEGE ZANZIBAR KUWA WABUNIFU ILI KUTOA HUDUMA ZA KIMATAIFA

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza kutoa maagizo kwa Uongozi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanziba  { ZIA } kuwa wabunifu katika kutoa huduma zinazokwenda kimataifa baada ya kufanya ziara ya ghafla katika uwanja huo. Wa pili (kulia) ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwnja wa Ndege wa Zanzibar Nd. Said Iddi Ndombogani na Katibu Mkuu Wizara ya Maiundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akili.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar Nd. Said Iddi ndombogani  kulia akimpatia maelezo Balozi Seif aliyepo kati kati wakati alipofanya nziara ya ghafla kiwanjani hapo. Kulia yao ni Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akili.
 Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akili akimfafanulia jambo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipofanya ziara fupi kwenye uwanja wa ndege wa Zanzibar.
 Baadhi ya abiria wa Kimataifa walioingia Zanzibar kwa usafiri wa anga wakipata huduma zitakazowapa fursa za kuwepo nchini kwa taratibu zilizowekwa kisheria.
Balozi Seif akiagizwa kuandaliwa utaratibu wa utoaji huduma wa ubia kwa watendahji wa uwanja wa ndege wa Zanzibar ili kupunguza msongamano wa abiria kiwanjani hapo.Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ. 
******************************
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi pamoja na Watendaji wa Mamlaka ya uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar { ZIA } kuwa wabunifu katika kuandaa utaratibu mzuri unaokwenda na wakati ambao utaondoa usumbufu kwa wasafiri wanaotumia uwanja huo.
Alisema watendaji hao pia wanapaswa kubadilika na kwenda na wakati kulingana na huduma wanazotoa kwa  wasafiri hasa wakizingatia kwamba  uwanja huo hivi sasa unaendelea kuimarishwa  katika hadhi na kiwango cha Kinachokubalika  kimataifa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara fupi ya ghafla kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kufuatia malalamiko mbali mbali aliyokuwa akiyasikia kutoka kwa baadhi ya abiria kutokana na huduma zinazotolewa  uwanjani hapo .
Matatizo yanayolalamikiwa zaidi na abiria hao ni pamoja na umbali wa masafa kati ya eneo la maegesho ya gari na lilipo jengo la wafafiri ambapo hujitokeza usumbufu kwa wale  wasafiri wenye mizigo mikubwa pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa hasa wakati wa mvua.
Balozi Seif alisema utaratibu uliopo hivi sasa  ni vyema ukaimarishwa zaidi ili  kupunguza bughdha pamoja na kuwapa faraja abiria  ambao wengi kati yao huwa tayari wameshachoka kutokana na uchovu wa safari zao za Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwatahadharisha watendaji hao kuwa makini na kauli zao wakati wanapotoa huduma kwa wasafiri wao ili kuwaondolea shaka na dhana wakati wanapoamua kutembelea hapa Zanzibar.
“ Zipo taarifa kwamba baadhi ya watendaji wamekuwa na kauli za makaripio. Sasa umefika wakati kwao kuwapunguzia bughdha wateja wao ili isionekane msafiri anayetembelea Zanzibar akaanza kuweka simanzi “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar uliutaka uongozi huo wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Zanzibar kukaa pamoja na Idara ya Uhamiaji pamoja na taasisi nyengine zinazokusanya mapato kiwanjani hapo katika kulitafutia ufumbuzi wa haraka tatizo la urasimu unaosababisha msongamano mkubwa wa wasafiri.
Alisema msongamano huo unaweza kuepukwa kwa taasisi hizo kuweka utaratibu utakaotoa huduma kwa ubia badala ya ule uliopo hivi sasa wa msafiri kupanga foleni ya kupata huduma kwa kila Taasisi.
Balozi Seif aliuhakikishia uongozi wa Mamlaka hiyo kwamba Serikali itajitahidi kuona yale mapungufu yanayokwaza uwajibikaji wa watendaji wa taasisi hiyo ambayo husimamiwa na taasisi nyengine yatapatia ufumbuzi.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Zanzibar Nd. Said Iddi Ndombogani alisema mamlaka hiyo inaendelea na juhudi za kukamilisha matengenezo ya banda la wasafiri litakalokidhi mahitaji hasa wakati wa msimu wa masika.
Nd. Said alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba malalamiko ya abiria kuteremka mbali na eneo la kupata huduma za wasafiri litakamilika baada ya kumalizika kwa matengenezo hayo.
Alisema utaratibu utawekwa kwa abiria hao kujihudumia wenyewe kwa kutumia vigari maalum ili kuondosha usumbufu kwa wale wasafiri watakaokuwa na mizigo mizito au mingi katika safari zao.
“  Kama tutaruhusu magari ya abiria na yale ya wasafiri kuingia na kusimama kwa ajili ya kuteremsha wateja wao mbele ya jengo la huduma za wasafiri ni kusema kwamba foleni ya gari hizo itaongeza usumbufu na kuwachanganya zaidi wasafiri wanaotaka kuwahi kwa mujibu wa tiketi zao “. Alisema Nd. Said Iddi Ndombogani.
Alifahamisha kwamba Mamlaka inaendelea kuzingatia vigezo vya Kimataifa katika kutoa huduma kwa wasafiri wanaotumia usafiri wa anga ambao humtaka abiria anayesafiri ateremke kwenye gari masafa ya mita mia Moja na eneo analotakiwa kupata huduma kwa ajili ya safari yake.

0 comments:

Post a Comment