Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akimkaribisha Balozi mpya wa Marekani nchini Tanzani, Mark Childres, wakati
alipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Juni 9, 2014 kwa
mazungumzo na utambulisho wa balozi huyo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa
katika mazungumzo na Balozi mpya wa Marekani nchini Tanzania, Mark Childres,
wakati alipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Juni 9, 2014 kwa
mazungumzo na utambulisho wa balozi huyo.
********
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MAKAMU WA RAIS-IKULU
=====
BALOZI MPYA WA MAREKANI AJITAMBULISHA KWA MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS
Ikulu, Dar es Salaam: 2014-06-09
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal
leo amekutana na Balozi mpya wa Marekani, Mheshimiwa Balozi Mark
Childress ambaye amefika ofisini kwa mheshimiwa Makamu wa Rais kwa ajili
ya kujitambulisha.
Balozi
Childress alimueleza Mheshimiwa Mkamu wa Rais kuwa, Tanzania ni nchi
yenye uhusiano maridhawa na Marekani na kwamba katika kipindi chake kama
Balozi atahakikisha uhusiano huu mzuri uliojengwa unadumishwa na
kwamba, nchi hizi mbili zinazidi kuwa na maeneo ya kushirikiana hasa
yanayolenga kuboresha maisha ya watu na kuwapatia maendeleo.
Balozi
Childress pia alisema kuwa Tanzania imekuwa ikitumia kama mfano
kufuatia kuonesha mabadiliko ya haraka katika miradi mbalimbali
inayoendeshwa hapa nchini kwa ushirikiano na watu wa Marekani na
akafafanua kuwa, kazi iliyoko mbele ni kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga
hatua zaidi na sio kurudi nyuma.
“Mheshimiwa
Makamu wa Rais, kila nikipata fursa ya kukutana na wenzangu tumekuwa
tukizungumzia suala la Tanzania kupiga hatua kwa haraka. Mna mambo mengi
yaliyofanyika na kazi iliyopo ni kuendelea kupiga hatua pasipo kurudi
nyuma,” alisema.
Kwa
upande wake Mheshimiwa Makamu wa Rais alimueleza Balozi Childress kuwa,
Tanzania ipo katika kipindi ambacho kinaonesha mabadiliko makubwa ya
kiuchumi na kwamba kazi ya serikali ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa
uchumi unakuwa na unasaidia vizazi vya sasa na vijavyo.
“Mtazamo
wetu katika serikali ni kuwa Tanzania itapiga hatua kubwa katika miaka
michache ijayo. Lengo letu ni kutazama kuwa ukuaji wa uchumi hauwi wa
muda mfupi, tunatazama pia maendeleo kwa vizazi vijavyo.
Kuhusu
suala la utunzaji mazingira, Balozi Childress alisifu hatua za
Mheshimiwa Makamu wa Rais hasa katika kazi ya uhamasishaji upandaji miti
na akasema, utunzaji wa mazingira ni jambo la muhimu ili kuifanya nchi
yetu iweze kuendelea na isikabiliane na matatizo yanayotokana na
mazingira kuharibiwa.
“Nakupongeza
Mheshimiwa Makamu kwa kazi yako ya uhamasishaji utunzaji wa Mazingira.
Usichoke kufanya hivyo maana unasaidia dunia,” Balozi Childress alisema.
Imetolewa na : Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam