Nasra akiwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro.
MTOTO mwenye umri wa miaka minne aliyefungiwa ndani ya boksi kwa zaidi na miaka mitatu mkoani Morogoro, amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi na tiba zaidi huku wataalamu wakikuna vichwa namna ya kumrudishia afya yake. Imeelezwa jopo la madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali ya binadamu wakiwemo wataalamu wa saikolojia, wanahitajika kwa ajili ya kumwezesha mtoto huyo mwenye ulemavu kuwa katika hali ya kawaida.
Aidha, pamoja na uhitaji wa jopo la wataalamu hao, mtoto huyo ambaye amelazwa katika wadi ya watoto, atahamishiwa katika wadi maalumu ya watoto wenye utapiamlo awe karibu na uangalizi wa lishe baada ya kubainika ana udhaifu mkubwa wa lishe.
Wakizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti hospitalini hapo, Daktari Bingwa wa Watoto wa MNH, Dk Mwajuma Ah- mada alisema mtoto huyo hajazidiwa kuumwa.
Alisema walimpokea juzi usiku na hatua za awali zilizofanywa ni pamoja na kuchukua baadhi ya vipimo kwa ajili ya uchunguzi.
“Mtoto aliletwa hapa jana (juzi) usiku, baadhi ya vipimo vimechuku- liwa, vingine atafanyiwa leo (jana) ikiwa ni pamoja na kumfanyia huduma ya kum scan (kumwingiza kwenye mashine maalumu) mwili mzima ili tufahamu tatizo na tiba sahihi,” alisema Dk Ahmada.
Alisema huduma ya tiba kwa mtoto huyo siyo ya daktari bingwa mmoja bali inahitaji jopo la wataalamu waki- wemo wa mifupa, saikolojia, viungo na magonjwa mbalimbali ya binadamu kumsaidia mtoto huyo.
“Kwa sasa hatuwezi kusema lolote kubwa kuhusu mtoto huyo ndio kwanza kafika na ndiyo tuko kwenye hatua ya awali ya kuchukua vipimo, na leo atafanyiwa huduma ya kumulikwa mwili mzima ili tujue tunaanzia wapi”, alisema Dk Ahmada.
Alisema pamoja na kusubiri majibu ya vipimo, hatua wanayochukua ni ya kumhamishia kwenye wadi ya watoto wenye utapiamlo, ili kutibu maradhi hayo ambayo ndio yameonekana awali, kwani mtoto amekosa lishe na viru- tubisho muhimu vya awali.
Alifafanua, katika hatua hiyo ya awali, mtoto huyo atakuwa akipewa maziwa ya lishe na kuendelea na tiba ya dawa za kuua vijasumu kutokana na kusumbuliwa na vichomi.
Akizungumzia kwa ufupi ikiwa mtoto huyo anaweza kurejea katika hali ya kawaida kwa viungo kunyooka na kutembea, Dk Ahmada alisema pamoja na kusubiri majibu ya vipimo, lakini pia tiba ya mtoto inategemea zaidi historia ya mtoto mwenyewe.
Mlezi azungumza Kwa upande wake, mlezi wa mtoto huyo , Josephina Joel akizungumza na gazeti hili wadini hapo alisema mtoto anaendelea vizuri ingawa juzi alikuwa na homa.
Hata hivyo alisema imeshuka, na kwamba kadri siku zinavyosonga, anaona uchangamfu wa mtoto.