SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, April 16, 2014

Upinzani wasusa kikao bunge la katiba Tanzania

 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgjideZe9jyM5esXCUTsGmMgSVvkjU1axFuttxG3MbSaO43fbQjdDGde3onTsozAQEIlpkfJwKpmajJ9e2z87Ijm0OwZmhaiow-IUhENQkPFEA7x3eRtzBJ6RASMBP87HxE1KXRg8AeogT7/s640/Picha-no-6.jpg
Baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameatoka nje ya kikao cha bunge hilo kinachoendelea mjini Dodoma kwa madai kwamba maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba Mpya yamekuwa yakipuuzwa.
Wajumbe wa bunge hilo ambao ni kutoka upande wa upinzani chini ya umoja unaojulikana kama UKAWA, yaani Umoja wa Katiba ya Wananchi, wameamua kutoka nje kupinga kile wanachosema ni kupuuzwa kwa makusudi maoni ya wananchi wanaotaka muungano wa muundo wa serikali tatu kama yalivyopendekezwa katika rasimu ya katiba hiyo.

Akichangia katika kikao cha bunge hilo Jumatano jioni, mmoja wa wajumbe Profesa Ibrahim Lipumba amelalamikia kauli za ubaguzi zinazotolewa na baadhi ya wajumbe, hususan wanaotaka muundo wa muungano wa serikali mbili, alieleza sababu za kutaka serikali tatu kuwa zitasaidia kutatua matatizo yaliyopo katika muundo wa sasa. Hata hivyo hakusita kupinga kile anachokiita kauli za ubaguzi kutoka kwa wajumbe wanaopinga mawazo ya wachache bungeni humoi. "Hatuwezi kuwa kundi la intarahamwe linalohamamisha ubaguzi ndani ya Tanzania, hili hatulikubali hatulikubali hatulikubali watu wote tunaotaka katiba ya wananchi tunawaachia intarahamwe waendelee na kikao chao. Ahsanteni sana". Mara baada ya kusema hivyo, wajumbe waliounga mkono kauli yake waliinuka na kutoka nje.

Hata hivyo, kikao cha bunge hilo kiliendelea baada ya makamu mwenyekiti wa bunge hilo kusema idadi ya wajumbe waliobaki walitosha kuendelea na kikao hicho.

Wanaounga mkono muundo wa serikali tatu, wanasema muundo wa sasa wa serikali mbili umeshindwa kutatua masuala yenye mgogoro katika muungano, maarufu kama kero za muungano, hivyo kudhoofisha muungano huo.

Hata hivyo wajumbe wanaounga mkono serikali mbili, yaani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanasema muundo wa serikali tatu ni kuvunja muungano wa Tanganyika na Zanzibar na pia itakuwa gharama kuiendesha serikali ya tatu.

Tangu kuanza kujadiliwa kwa vipengele viwili vya rasimu ya katiba mpya ya Tanzania, vijembe, kejeli na kurushiana na maneno makali miongoni mwa wajumbe yamekuwa mambo ya kawaida kuyasiki kutokana na mgawanyiko wa dhahiri wa misimamo, hasa kuhusu muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo ya kukusanya maoni ya wananchi.

Bunge hilo lenye zaidi ya wajumbe mia sita linaundwa na wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la wawakilishi Zanzibar na wajumbe 201 walioteuliwa na rais wa Tanzania kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.

Wajumbe 191 kutoka upinzani walitoka nje ya bunge kupinga mwenendo wa bunge hilo katika kujadili rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

HABARI NA BBC SWAHILI