Waziri
wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (aliyenyoosha mikono) akitoa
taarifa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara za
kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam wakati alipokutana na
Kamati ya Bunge ya Miundombinu. Kulia kwa Waziri Magufuli ni Naibu
Waziri wa Wizara ya Ujenzi Eng. Gerson Lwenge na anayefuata ni Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga. Kushoto kwa
Waziri ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Peter
Serukamba na wengine ni Wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na Wataalam kutoka
Wizara ya Ujenzi.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Peter Serukamba (mbele mwenye
koti) akiwaongoza Wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge kukagua maendeleo ya
ujenzi wa Daraja la Segerea Jijini Dar es Salaam.
Naibu
Waziri wa Ujenzi Mhe. Eng. Gerson Lwenge akitoa maelezo kwa Wajumbe wa
Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu ujenzi wa barabara ya Mbezi
kupitia Malambamawili kuelekea Kifuru hadi Kinyerezi.
Wajumbe
wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakiwa na Naibu Waziri wa Wizara ya
Ujenzi Eng. Gerson Lwenge na Watendaji wengine kutoka Wizani na Tanroads
wakikagua barabara ya Tegeta – Wazo Hill ambayo iko katika ratiba ya
kufanyiwa matengenezo kama sehemu ya mradi wa kupunguza msongamano wa
magari Jijini Dar es Salaam.
Mhe.
Halima James Mdee (kulia) Mbunge wa Jimbo la Kawe, akimsikiliza Naibu wa
Waziri wa Ujenzi Mhe. Eng. Gerson Lwenge (kushoto) wakati Kamati ya
Bunge ya Miundombinu iliposimama eneo la Goba ambapo itapita barabara ya
lami kutokea Tangi Bovu kuelekea Mbezi Mwisho katika barabara ya
Morogoro.
Waziri
wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (aliyenyoosha mikono) akitoa
taarifa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara za
kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam wakati alipokutana na
Kamati ya Bunge ya Miundombinu. Kulia kwa Waziri Magufuli ni Naibu
Waziri wa Wizara ya Ujenzi Eng. Gerson Lwenge na anayefuata ni Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga. Kushoto kwa
Waziri Magufuli ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe.
Peter Serukamba na wengine ni Wajumbe wa Kamati hiyo.
Mbunge
wa Viti Maalum (CCM) Mhe. Zaina Shamte Madabida (katikati) akichangia
jambo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipokutana na
Wizara ya Ujenzi kupitia maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara
za kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam. Wengine katika
picha ni Mhe. Mtutura Abdallah Mtutura (kushoto), Mbunge wa Tunduru
Kusini (CCM) na Mhe. Ritta Enesper Kabati (kulia), Mbunge wa Viti Maalum
(CCM).
Kamati
ya Bunge ya Miundombinu imefanya ziara ya kutembelea barabara ambazo
zinatarajiwa kuanza kujengwa pembezoni mwa jiji la Dar kwa ajili ya
kupunguza msongamano wa magari.
Kamati
hiyo ambayo imekutana na Waziri wa Ujenzi pamoja na Watendaji wa
Wizara, ilikuwa ikipitia shughuli zinazotekelezwa na Wakala wa Barabara
Tanzania (Tanroads) kwa mkoa wa Dar es salaam.
Akiongea
na Wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge ya Miundombinu, Waziri wa Ujenzi
Mhe. Dkt. John Magufuli ameeleza kuwa mbali na utekelezaji wa miradi
mbali mbali mikubwa ya maendeleo jijini Dar es Salaam lakini pia upo
mradi maalum wa kupunguza msongamano wa magari hapa jijini kwa
kuimarisha barabara zilizoko pembezoni mwa jiji ambazo ni viungo muhimu
kwa barabara kuu zinazoingia na kutoka mjini.
Mheshimiwa
Magufuli amebainisha kuwa katika awamu ya kwanza tayari jumla ya
kilometa 22 kati ya kilometa 78.9 za barabara za kuondoa msongamano
zimejengwa. Barabara hizo zilizokamilika zimetajwa kuwa ni; kuanzia
Kituo cha Mabasi Ubungo kupitia Kigogo hadi barabara ya Kawawa (Km 6.4),
kutoka Kigogo Roundabout/Kawawa kupitia bonde la Msimbazi hadi makutano
ya Mtaa wa Jangwani na Twiga (Km 2.72) ingawa bado katika barabara hii
kuna sehemu zimewekewa pingamizi mahakamani na hivyo kuzuia ujenzi
katika maeneo hayo kusimama. Barabara nyingine ni Jet Corner – Vituka –
Devis Corner (Km 12) na Ubungo Maziwa - Mabibo External/Mandela (Km
0.64).
Katika
hatua nyingine Waziri wa Ujenzi ameifahamisha Kamati hiyo ya Bunge
kuwa, katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 jumla ya kilometa 27.2
zitaanza kujengwa ikiwa ni awamu ya pili ya mpango huo.
Waziri
Magufuli alizitaja barabara ambazo katika awamu hii ya pili tayari
zimepata Makandarasi na ujenzi wake utaanza mara baada ya mikataba
kusainiwa hivi karibuni kuwa ni; Mbezi kupitia Malambamawili kuelekea
Kifuru hadi Kinyerezi ambayo ina urefu wa kilometa 14 lakini kwa mwaka
huu zitajengwa kilometa 4 zinazoanzia Kifuru hadi Kinyerezi. Barabara
nyingine ni Tegeta Kibaoni kupitia Wazo Hill kwenda Goba hadi Mbezi
Mwisho yenye urefu wa kilometa 20 ambapo kwa awamu hii zinajengwa
kilometa 7.
Aidha,
barabara ya kuanzia Tangi bovu hadi Goba itajengwa kilometa zote 9 na
Kimara Baruti hadi Msewe kilometa zote 2.6 pia zimejumuishwa katika
awamu hii.
Barabara
nyingine ambazo tayari zimepata Makandarasi na zinajengwa katika mwaka
huu wa fedha 2013/14 ni Kimara hadi Kilungule External/Mandela ambayo
ina urefu wa kilometa 9 lakini katika awamu hii itaanza kujengwa sehemu
ya Maji Chumvi hadi External/Mandela ambayo ina urefu wa kilometa 3.
Barabara nyingine ni Tabata Dampo hadi Kigogo yenye urefi wa kilometa
1.6.
Barabara zote hizi zinatarajiwa kukamilika katika kipindi cha kati ya mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na nusu.
Naye
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi Eng. Gerson Lwenge ambaye aliongozana
na Ujumbe wa Kamati hiyo kuzipitia barabara hizo zinazojengwa, alielezea
kuwa baadhi ya barabara ambazo ni ndefu imebidi kutoa kazi hizo kwa
awamu kulingana na muda uliopo na mgao wa fedha kwa mwaka huu. Hivyo
alielezea kuwa yale maeneo ambayo hayakujumuishwa katika awamu hii
yameingizwa katika mipango ya bajeti ya mwaka ujao wa 2014/2015.
Mhe.
Eng. Lwenge ameeleza kuwa miradi hii itakwenda sambamba na utekelezajiwa
mradi wa ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa daraja
la Kigamboni, ujenzi wa sehemu ya barabara kati ya Bendera Tatu na
Gerezani/KAMATA.
Miradi
mingine ambayo iko katika hatua mbali mbali za utekelezaji ni ununuzi
wa Boti ya usafiri kati ka Dar es Salaam na Bagamoyo pamoja na ujenzi wa
barabara za juu katika maungio yenye mkusanyiko wa magari mengi katika
barabara ya Mandela maeneo ya TAZARA na Ubungo.
Wakati
akihitimisha ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge ya
Miundombinu Mheshimiwa Peter Serukamba ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa
namna inavyosimamia utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na matengenezo ya
barabara kwa ujumla hapa nchini. Hata hivyo aliitaka wizara hiyo
kuangalia uwezekano wa kuijumuisha sehemu ya barabara kati ya Goba hadi
Chuo cha Ardhi kuingiza katika mpango huo wa kupunguza msongamano.
Mheshimiwa
Serukamba aliongeza kuwa, ingawa barabara hiyo ni ya changarawe imekuwa
ikitoa mchango mkubwa kupunguza msongamano hasa katika kipindi hiki
ambacho barabara ya Morogoro iko katika ujenzi mkubwa na hivyo magari
mengi kuitumia barabara mbadala.
0 comments:
Post a Comment