Mbunge wa jimbo la Ubungo (CHADEMA) Mh. John Mnyika.
Nimemtumia
ujumbe Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kumshauri ajiuzulu
kutokana na kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es
Salaam kinyume na maelezo yake ya uongo aliyoyatoa bungeni tarehe 4
Februari 2013.
Aidha,
Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Mamlaka zinazohusika na huduma
ya maji jijini (DAWASA na DAWASCO) watoe maelezo kwa umma juu ya sababu
za kweli za matatizo ya maji kujirudia rudia katika Jiji la Dar Es
Salaam.
Pia,
wajieleze kwa umma ni kwanini wananchi wasipendekeze Rais awachukulie
kwa uzembe, kuisababishia hasara Serikali, kuathiri uchumi wa nchi na
maisha ya wananchi kwa kukosa maji mara kwa mara ambayo ni huduma ya
msingi ya binadamu na malighafi muhimu katika uzalishaji.
Itakumbukwa
kwamba tarehe 4 Februari 2013 niliwasilisha hoja binafsi bungeni juu ya
hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji katika jiji la Dar Es
Salaam, nikipendekeza Bunge kuingilia kati kuweza kuisimamia Serikali
kuchukua hatua za haraka.
Iwapo
hoja hiyo ingejadiliwa na maazimio yote kutekelezwa matatizo ya maji
katika Jiji la Dar Es Salaam mpaka hatua ya sasa yangekuwa yamepungua
katika maeneo mbalimbali kutokana na hatua ambazo nilipendekeza
zichukuliwe.
Hata
hivyo, badala ya kuunga mkono hoja hiyo ambayo ingeisaidia Wizara yake
na kurekebisha udhaifu uliokuwepo na hivyo kumrejeshea imani kwa umma
ambavyo ilikuwa imepungua; Waziri Maghembe akaamua kinyume cha kanuni za
Bunge kutoa hoja ya kuondoa hoja niliyowasilisha.
Katika
hatua hiyo nilijaribu kutumia kanuni za Bunge kuweza kutoa ufafanuzi
juu ya uongo wa Waziri Prof. Maghembe na hatua ambazo Bunge lilipaswa
kuchukua. Hata hivyo Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai aliamua kukiuka
kanuni kumlinda hali ambayo ilichochea vurugu bungeni.
Mara
baada ya kurejea bungeni tarehe 10 Februari 2013 nilihutubia wananchi
na kuwaeleza kusudio la kuandaa maaandamano kwenda Wizara ya Maji iwapo
katika kipindi cha ndani ya wiki mbili Waziri Prof. Maghembe
asingejitokeza kutoa maelezo kwa umma kuhusu masuala yote ambayo
alipaswa kuyajibu bungeni juu ya hatua za haraka zilizopaswa
kuchukuliwa.
Ndani
ya wiki hizo mbili Waziri Maghembe alijitokeza mara mbili kuzungumzia
masuala ya maji Dar Es Salaam; kupitia mikutano ya CCM ikiwemo katika
kata ya Goba jimboni Ubungo na katika mkutano wake na wafanyakazi DAWASA
na DAWASCO tarehe 21 Februari 2013 na kueleza hatua za haraka ambazo
angesimamia zichukuliwe.
Hata
hivyo, baada ya wiki moja bila ya Waziri wa Maji na Wizara kwa ujumla
kuonyesha kwa matendo kuisimamia kwa karibu EWURA, DAWASA, DAWASCO na
Manispaa ya Kinondoni kuchukua hatua za haraka ambazo nilizieleza kwenye
hoja binafsi, niliamua kuchukua hatua zaidi.
Nilitangaza
kuongoza maandamano ya wananchi tarehe 16 Machi 2013 kwenda Wizara ya
Maji ili kupata majibu na kuisimamia Serikali kuchukua hatua za haraka.
Hata hivyo maandamano hayo yalizuiliwa na Jeshi la Polisi kwa sababu
zisizo za msingi na kuombwa kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Nilikata
rufaa lakini toka wakati huo mpaka anaondelewa katika nafasi yake
Waziri Dr Emmanuel Nchimbi alikwepa kuchukua hatua dhidi ya aliyekuwa
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela kwa kuvunja
sheria, kusababisha hasara na kuwanyima haki ya msingi wananchi ya
kufikisha ujumbe kwa Serikali.
Maandamano
hayo yangefanyika na hatua kuchukuliwa matatizo yangepungua tofauti na
ilivyo sasa, hivyo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Pereira Silima
anapaswa kueleza umma lini rufaa hiyo itashughulikiwa maandamano yaweze
kufanyika wananchi wapate majibu ya hatua za haraka nilizopendekeza
ndani na nje ya Bunge.
Zaidi
ya nusu mwaka umepita toka Waziri Prof. Maghembe atoe ahadi ambazo
ameshindwa kusimamia utekelezaji wake na hivyo kupaswa kujiuzulu. Iwapo
Waziri Prof. Maghembe hatajiuzulu nitaeleza hatua zaidi ambazo
nitachukua.
Wakati
hatua hizo zikisubiriwa, natoa mwito kwa DAWASA na DAWASCO kuhakikisha
kwamba katika kipindi kisichozidi wiki moja huduma za maji zinarejea
katika maeneo ambayo yalikuwa yakipata mgawo wa maji.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
10/01/2013
0 comments:
Post a Comment