SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, December 13, 2013

Majina ya waliofariki katika ajali ya basi la Burdan, Tanga

*Video Ya ITV Yenye Taarifa Hii Ya Ajali Imepachikwa Hapo Chini.

Basi la Burdan leo limepata ajali kijiji cha Taula Wilaya ya Handeni ambapo mmoja wa majeruhi amesema kuwa basi hilo lilikwaruzwa na lori wakati dereva akijaribu kulipita kwenye daraja, jambo lililosababisha basi hilo kukosa uelekeo na kusererekea bondeni katika mteremko mkali wa kilima cha Kwedikwazu.

Imeripotiwa kuwa mpaka sasa kuwa zaidi ya watu 12 wamefariki dunia huku 55 wakiachwa na majeraha mbalimbali. Majeruhi wanne wamepelekwa katika hospitali za MOI (Dar es Salaam) na KCMC (Moshi).

Taarifa zinazowanukuu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe na Daktari wa zamu hospitali ya 


Magunga ya Mkoa wa Korogwe, Dk John Hedes zimesema walipopoteza maisha katika ajali hiyo wametambuliwa kuwa ni dareva wa basi hilo Luta  Kundaeli Kimaro, Joyce Mokiwa (36) na mwanaye ambao ni wakazi wa National Housing, Msoke Mosha ambaye ni mwalimu wa Mgombezi, Bashar Shafii wa Kilole, Bryton wa eneo la Lutheran, Rehema Nassoro (23) mkazi wa Bagamoyo Kilole, Agnes Linus mkazi wa Mandera, Mariamu Juma, Asha Mahimbo, Msoke Mosha, Agnes Linus, Jimano Julius na Juma Athumani.

=========
TAARIFA YA IKULU KWA UMMA: RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA WALIOFARIKI AJALINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Lt(Mst) Chiku Galawa kufuatia vifo vya watu 12 na wengine 71 kujeruhiwa baada ya basi Na. T610 ATR la Kampuni ya Burudani lililokuwa likitokea Korogwe kwenda Dar es Salaam kupinduka katika Kijiji cha Taula mapema asubuhi ya tarehe 12 Desemba, 2013.

“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 12 vilivyotokea tarehe 12 Desemba, 2013 huku wengine 71 wakijeruhiwa, baada ya basi la Kampuni ya Burudani walilokuwa wakisafiria kutoka Korogwe kuelekea Dar es Salaam kupinduka katika Kijiji cha Taula”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Rais Kikwete amesema vifo vya watu hao ni pigo kubwa siyo tu kwa familia za watu waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo, bali pia Taifa letu kwa ujumla ambalo limepoteza nguvu kazi muhimu iliyokuwa bado inahitajika kwa ujenzi wa Taifa.

“Kutokana na msiba huo mkubwa uliotokea katika eneo la Mkoa wako, ninakutumia Salamu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu wewe Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Lt. (Mst) Chiku Galawa kwa kupoteza watu wengi kwa mara moja katika ajali hiyo.  Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Mahala Pema Peponi Roho za Marehemu wote, Amina”.

Rais Kikwete amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Tanga kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa familia, ndugu na jamaa waliopotelewa na wapendwa wao katika ajali hiyo, lakini amewahakikishia kwamba yuko pamoja nao katika kipindi hiki cha maombolezo.  Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira katika kipindi hiki kigumu wanachopitia wakiomboleza vifo vya ndugu zao.

Aidha Rais Kikwete amesema anawaombea kwa Mwenyezi Mungu majeruhi wote wa ajali hiyo waweze kupona haraka na kurejea katika hali zao za kawaida, ili waungane tena na ndugu na jamaa zao na kuendelea na maisha yao kama ilivyokuwa kabla ya kutokea kwa ajali.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

12 Desemba, 2013



SOURCE: BOFYA HAPA

0 comments:

Post a Comment