Afisa Mwandamizi wa
Benki ya Dunia Bw. Richard Martini (katikati) akitoa salaam za Mkurugenzi Mkazi
wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi Bw. Phillipe Dongier,
ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia vigezo vya tafiti vya
kimataifa katika kutoa matokeo ya Mapato na Matumizi ya Kaya
nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile (katikati) akitoa taarifa kwa vyombo vya
habari kuhusu matokeo ya utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi leo
jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Dkt. Albina Chuwa.
Sehemu ya waandishi wa habari wakati wa mkutano
huo.
Na Aron Msigwa –
MAELEZO, Dar es salaam.
Uwezo wa Mapato na
Matumizi ya Kaya Binafsi nchini kwa mwaka 2011/2012 unaonyesha kuongezeka
kutokana na maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika sekta ya elimu, afya,
umiliki wa biashara, shughuli za kilimo, umiliki wa Vifaa na Rasilimali , makazi
bora, ongezeko la shughuli za kiuchumi na ajira.
Akitoa taarifa ya
Utafiti ulioendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuangalia tathmini ya
kiwango cha umasikini wa kaya kwa kutumia kipato na masuala mengine yasiyo ya
umasikini wa kipato jana jijini Dar es salaam , Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
Dkt. Servacius Likwelile amesema kuwa kukua kwa kiwango cha elimu, matumizi ya
nishati ya umeme, hali ya makazi na umiliki wa rasilimali ni miongoni mwa sababu
za kuongezeka kwa uwezo wa mapato na matumizi ya
kaya.
Amesema kuwa utafiti
huo ulifanyika kuanzia mwezi Oktoba 2011 hadi Oktoba 2012 ambapo jumla ya kaya
10,186 kati ya 10,400 zilizokuwa zimelengwa zilihojiwa katika maeneo ya Dar es
salaam na maeneo mengine ya mijini na vijijini kwa Tanzania
Bara.
Amesema uchumi wa
Tanzania kwa sasa umekua kutokana na kuimarika kwa sekta za ujenzi,
usafirishaji, Elimu, shughuli za mawasiliano, huduma za afya na huduma za
kifedha.
“ Serikali imefanya
mambo makubwa na sasa uchumi wa Tanzania umekua kutokana na juhudi kubwa
zilizofanywa katika kuboresha miundombinu ,kuwekeza katika sekta ya elimu,
usafirishaji, mawasiliano pamoja na ongezeko la huduma za kifedha”
amesema.
Amesema kumekuwa na
jitihada mbalimbali zilizofanywa na serikali zikiwemo kuongeza ujenzi wa shule
Zaidi hasa zile za sekondari ambazo zimewezesha kupanda kwa kiwango cha
wanafunzi wanaojiunga katika elimu ya sekondari kutoka 15% mwaka 2007 hadi
asilimia 29% 2011/12.
Amefafanua kuwa idadi
ya kaya zinazoishi katika nyumba zilizojengwa kwa vifaa vya ujenzi vya kisasa, paa za
kisasa, vigae na matumizi ya zege na kuta imara tangu mwaka 2007 imeongezeka kwa
66%.
Ameongeza kuwa matokeo
ya utafiti yanaonyesha kuwa asilimia 4% ya kaya zinamiliki pikipiki, 55%
zinamiliki radio na 57% ya kaya zote angalau mwanakaya mmoja anamiliki simu ya
mkononi na kufafanua kuwa kiasi cha asilimia 78 ya kaya za maeneo ya mengine ya
mjini na asilimi 88 ya kaya za Dar es salaam zinamiliki angalau simu moja ya
mkononi.
Katika hatua nyingine
Dkt. Servacius ameeleza wastani wa kiwango cha umasikini wa chakula kitaifa ni
asilimia 9.7 na kuongeza kuwa kiwango hicho kinafikia asilimia 11.3 kwa maeneo
ya vijijini huku Dar es salaam ikiwa na kiwango cha chini kabisa cha umasikini
wa chakula kwa asilimia 1.0 na maeneo mengine ya mjini yakiwa na umasikini wa
chakula kwa asilimia 8.7.
Amesema miji mikubwa
ina kiwango cha chini cha umasikini wa chakula kwa asilimia 1.0 ambapo wananchi
wanaoishi maeneo mengine ya mjini wana umasikini wa chakula wa asilimia
8.7.
Ameongeza kuwa
umasikini wa mahitaji ya msingi kwa Tanzania bara ni asilimia 28.2
ikilinganishwa na asilimia 33.3 kwa maeneo ya vijini na asilimia 21.7 kwa maeneo
mengine ya mjini na kubainisha kuwa Dar es salaam ina kiwango cha chini cha
umasikini wa mahitaji ya msingi cha asilimia 4.1.
Kwa upande wake Afisa
Mwandamizi wa Benki ya Dunia Bw. Richard Martini akitoa salaam za Mkurugenzi
Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi Bw. Phillipe
Dongier, ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia vigezo vya tafiti
vya kimataifa katika kufuatilia hali ya umasikini na kipato
nchini.
Amesema twakimu za
utafiti huo zilizotolewa zinaonyesha hali halisi ya maisha wanayoishi wanachi na
kuongeza kuwa zitaisaidia serikali, wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo
kuelewa na kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo na kukabiliana na
changamoto za umasikini zilizopo nchini.
0 comments:
Post a Comment