SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, November 15, 2013

MAKUNDI YA WAASI DRC WATAKIWA KUWEKA SILAHA CHINI

Balozi wa China Liu Jieyi ambaye nchi yake ni Rais wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Novemba, akielezea yale yaliyojiri wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Usalama uliofanyika jana alhamisi na kujadili hali ya Jamhuri ya Kidemokrasia. Tamko la Rais wa Baraza ambalo limeridhiwa na wajumbe wote 15 wanaounda Baraza la Usalama, wametoa wito kwa makundi ya waasi katika DRC kuweka chini silaha zao, makundi hayo ni pamoja na kundi la M23. Mbali ya kuweka silaha chini yametakiwa pia kuvunjika. Vivile Baraza hilo pamoja na kutambua kwamba kundi la waasi la M23 limemwaga damu ya wananchi wengi wa DRC pia limepoteza maisha ya walinzi wa amani wanaohudumu katika Misheni ya MONUSCO na kwa sababu hiyo Baraza limerejea wito wake kwamba litaendelea kuunga mkono walinzi wa amani maarufu kama Blue Helmet katika utekelezaji wa majukumu yao.

Na Mwandishi  Maalum

Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa  jana alhamis limetoa wito  linaolitaka kundi la wapiganaji la M23 kuvunja kundi hilo  mara moja ikiwa ni pamoja na kuweka silaha zao chini.
Aidha   Baraza hilo limekaribisha tamko la awali  la kundi hilo la M23 kwamba limeamua kumaliza uasi wake na umwagaji damu dhidi ya  Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Kongo.
Katika   mkutano wake ulIojadili hali  katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,   Balozi  Liu Jieyi wa   China  ambaye ndiye  Rais wa  Baraza Kuu la Usalama  kwa mwezi huu wa  Novemba na akizungumza kwa niaba ya wajumbe  15 wa Baraza amesema.
 “Baraza linatoa wito wa hitimisho na utekelezaji wa makubaliano ya mazungumzo ya Kampala ambayo pamoja na  mambo mengine yanatoa  fursa ya   upokonyaji wa silaha na  kuvunjwa kwa kundi la  M23 na uwajibikaji kwa wakiukaji wa haki za binadamu.
Mazungumzo hayo ya Kampala maarufu kama ‘Kampala Talks’ yanafanyika  chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Mkutano wa Kimataifa wa Eneo la Maziwa Makuu, ( ICGLR), Rais  Yoweri Kaguta Museven pamoja na  Waziri wa Ulinzi wa Uganda, Crispus Kiyonga.
Kwa mujibu wa  taarifa ya Rais wa Baraza Kuu la Usalama  ( Presidential Statement )  Baraza hilo limeonyesha  wasi wasi  kuhusu  mwendelezo wa tishio la usalama kutoka kundi la Forces Democratique de Liberation du Rwanda ( FDLR).
Kutokana na  wasi wasi huo, Baraza Kuu linahimiza umuhimu wa  kusambaratishwa kwa kundi hilo pamoja na makundi mengine  yenye silaha.
Aidha  Baraza  Kuu la  Usalama ,  limelaani kwa nguvu zake zote kuhusu kuendelea kwa  vitendo vya  ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,  unaofanywa na makundi yenye silaha   yakiwamo  mauaji ya papo  kwa papo, unyanyasaji  wa kijinsia na matumizi makubwa ya watoto  katika vita.
Vile vile     Baraza hilo pia  limetambua kuwa   katika kipindi cha miezi  19 ya uasi wa kundi la M23, kundi hilo limeua walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu katika DRC kupitia  Misheni ya Kutuliza Amani maarufu kama  MONUSCO inayoongozwa na  Bw. Martin Kobler, ambaye ni  Mwakilishi Maalum wa  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika DRC.
Na kwa sababu hiyo Baraza Kuu la Usalama   limerejea tena wito wake kwamba litaendelea   kuwaunga mkono  walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa,  maarufu kama  Blue Helmet katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kundi la  M23 ambalo hivi karibuni  lilipata kichapo cha aina yake kutoka MONUSCO  linaundwa  na wanajeshi ambao waliasi kutoka jeshi la kitaifa la DRC mwezi  wa Nne,kundi ambalo  pamoja na makundi mengine yenye silaha yamekuwa mara kwa mara  yakipambana na majeshi ya  serikali  (FRDC).
Katika  mwaka uliopita mapigano kati ya makundi ya waasi na majeshi ya serikali yalisababishwa zaidi ya watu 100,000 kuyakimbia makazi yao na hivyo kuongeza uzito wa jukumu la  kutoa  misaada ya kibinadamu katika eneo ambalo tayari zaidi ya watu  2.6 milioni ni wakimbizi wa ndani huku wengine  6.4 milioni wakihitaji msaada wa chakula na  huduma za dharura.
Aidha Baraza Kuu linahimiza Umoja wa Mataifa, na washirika wake wengine kuendelea na jitihada zake katika utekelezaji wa  Mpango Mpana wa Kisiasa  kwaajili ya  DRC na  Maziwa Makuu  uliosainiwa na nchi 11  na   wadhamini wanne  mapema mwaka huu ,  mpango unaolenga katika kuleta Amani  ya kudumu katika  eneo la Maziwa Makuu.
NA MICHUZI MATUKO

0 comments:

Post a Comment