SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Sunday, March 24, 2013

WAKAZI WA ARUSHA KULIPIA ANKARA ZA MAJI SAFI NA MAJI TAKA KUPITIA M-PESA SASA‏

Mkuu wa Wilaya ya jiji la Arusha, John Mongella, akiongea wakati wa uzinduzi rasmi wa jinsi ya kulipia Ankara ya maji safi kupitia huduma ya M-PESA, kwa wakazi wa mkoa wa jiji la Arusha, kutoka kushoto ni Mwenyekiti kamati ya mawasiliano na ujenzi Zanzibar Bw. Makame Mshimba Mbaruk, Mwenyekiti wa bodi ya (AUWSA) Bw. Felix Mrema. 
Mkuu wa Wilaya ya jiji la Arusha, John Mongella, wa nne toka kushoto akifuatilia maelekezo toka kwa Mkuu wa Vodacom kanda ya kaskazini, Bw. Philemon Chacha jinsi ya kulipia  Ankara ya maji safi kupitia huduma ya M-PESA, mara baada ya kuzindua huduma hiyo mkoani humo ambapo wakazi wa jiji la Arusha watakuwa wakilipia Ankara za maji safi na maji taka kwa kupitia huduma hiyo, wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Mwenyekiti kamati ya mawasiliano na ujenzi Zanzibar Bw. Makame Mshimba Mbaruk, Mwenyekiti wa bodi ya (AUWSA) Bw.Felix Mrema na Mkuu wa kitengo cha huduma kwa wateja wa (AUWSA) Masoud Katiba.
Mkuu wa Wilaya ya jiji la Arusha, John Mongella, wa tano kutoka kushoto waliokaa, akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom na wa mamlaka ya maji safi na maji taka ya Arusha (AUWSA) mara baada ya hafla fupi ya uzinduzi wa kulipia Ankara za maji safi na maji kupitia huduma ya Vodacom M-PESA kwa wakazi wa jiji la Arusha.
****
Arusha, Zaidi ya wananchi 500,000 waishio katika manispaa ya Arusha sasa hawatahitaji tena kupanga foleni ili kulipia ankara za maji. Hii inafuatia ushirikiano baina ya Vodacom Tanzania na mamlaka ya maji safi na maji taka ya Arusha (AUWSA) utakaowezesha malipo hayo kufanyika kupitia huduma ya M-Pesa.
AUWSA ni mamlaka iliyoundwa kisheria chini ya sheria ya utoaji maji kifungu cha 272 ili kuendesha shughuli za upatikanaji wa maji safi na kusimamia maji taka mjini Arusha. AUWSA ilianza kufanya kazi zake kama taasisi huru mwezi Januari, 1998
Huduma ya M-Pesa ina mawakala zaidi ya 40,000 nchi nzima, hivyo kuwezesha urahisi wa malipo ya huduma ya maji kama hii mahala popote pale nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ushirikiano wa utoaji huduma hiyo ya malipo, Mkuu wa Wilaya ya jiji la arusha, John Mongella alisema kuwa hatua hii mpya itachangia kwa kiasi kikubwa kuleta huduma bora kwa wakazi wa mji wa Arusha katika viwango vya juu zaidi.
"Hili ni jambo la maana sana ambalo siyo tu kwamba limekuja kwa AUWSA, bali kwa watu wa Arusha kwa ujumla. Ninazishukuru pande zote mbili ambazo zimeshirikiana kufanikisha huduma hii. Nataka kuwahakikishia kuwa serikali imeazimia kuunga mkono juhudi za namna hii za kutumia utaalamu unaolenga kuinua maisha ya wananchi," alisema Mongella.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa AUWSA, Lucy Shushu Koya, alizungumzia jinsi ambavyo kwa kiwango kikubwa wakazi wa Arusha wataepuka usumbufu wa kutumia muda mrefu kwenye foleni za kulipia huduma ya maji na kusema: "Huduma hii ni hatua ya kipekee hasa ikizingatiwa kuwa kuanzia sasa muda ambao mteja angeutumia kusubiri kwenye foleni, badala yake atauingiza katika shughuli nyingine za kila siku kama kazi au biashara. Pia kufanya malipo kupitia M-Pesa kutarahisisha ufanyaji kazi wa mamlaka na kutoa nafasi ya kuongeza ubora wa huduma."
Mkuu wa Vodacom Kanda ya Kaskazini, Philemon Chacha, alisema: "Nawahimiza wakazi wa Arusha watumie huduma ya M-Pesa kulipia ankara za maji kutokana na kuwa ni huduma ya haraka na salama. Hii ni njia ya uhakika ya kuokoa muda malighafi muhimu ya muda, na hivyo ni vyema sote kuitumia."
Ili kufanya malipo kupitia M-Pesa, wateja wanashauriwa kupiga *150*00# kisha kuchagua namba 4, na baada ya hapo kuingiza namba ya biashara (230230). Kufuatia hatua hiyo watatakiwa kuingiza namba ya akaunti na namba ya siri (PIN), halafu watabonyeza 1 kuthibitisha, au 2 kusitisha mhamala.

CHANZO: bofya

0 comments:

Post a Comment