Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.
****
Na Khadija Mngwai
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limewataka viongozi wa klabu, akiwemo Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, kuitisha mikutano mikuu ya wanachama mara kwa mara.
Wanachama wa Simba wapatao 607 walikutana jijini Dar es Salaam siku chache zilizopita na kutangaza kumuengua Rage madarakani, wakidai ameshindwa kutekeleza ahadi alizoahidi wakati anaingia, lakini Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, imetengua uamuzi huo.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, amesema ukosefu wa amani katika klabu kongwe Tanzania, unasababishwa na kutoitisha mikutano mikuu ya mara kwa mara.
Osiah alisema ni vyema viongozi wa klabu hizo wakaliona tatizo hilo na kuhakikisha wanaitisha mkutano mkuu kila mwaka kwa mujibu wa katiba zinazowaongoza.
“Kamati ya Mgongolwa imeamua kubatilisha mkutano wa wanachama wa Klabu ya Simba juu ya maamuzi yao ya kumpindua Rage kutokana na mkutano huo kuwa batili, hivyo iwapo wanachama watahitaji kufanya mkutano ni lazima wakubaliane na kamati ya utendaji ya klabu yao kwa kuiandikia barua ili iweze kuridhia kwa lengo la kujenga na si kubomoa.
“Hata hivyo, viongozi wa klabu wametakiwa kuitisha mkutano ndani ya muda mwafaka ili kuweza kuondoa matatizo kama yaliyojitokeza katika klabu hiyo na suala hili nalisema kwa ajili ya klabu zote na si kwa Simba pekee,” alisema Osiah.
Hivi karibuni wanachama walifanya mkutano jijini Dar es Salaam na kutangaza kumvua madaraka Rage, lakini wiki iliyopita TFF ikatangaza kuwa mkutano huo ulikuwa batili.
HABARI NA GPL
0 comments:
Post a Comment