SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, January 22, 2013

SPIKA ASILINDE UFISADI KIWANDA CHA URAFIKI, WAZIRI KIGODA ASIKWEPE KUTOA MAJIBU - MNYIKA

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika.
*******
Tarehe 21 Januari 2012 gazeti la Tanzania Daima limemnukuu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara akieleza kuwa wameunda Kamati Ndogo ya Uchunguzi kuhusu ufisadi wa miaka mingi wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki lakini wanasubiri idhini ya Spika kamati hiyo ianze kazi. Habari hiyo imeeleza kuwa Spika ndiye anayekataa uchunguzi huo kufanyika.
Nikiwa mbunge wa Jimbo la Ubungo, mahala kilipo Kiwanda cha Urafiki nasisitiza umuhimu wa Spika kutoa kauli kwa umma kuhusu hatua alizochukua ikizingatiwa kwamba hata kabla ya kamati ndogo ya uchunguzi kuundwa nilishawasilisha kwa Spika wa Bunge maelezo binafsi kuhusu ufisadi huo na mpaka sasa hajatoa idhini yashughulikiwe.
Aidha, majibu ya Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdalah Kigoda kuwa anafuatilia suala hilo Wizarani hayajitoshelezi kwa kuzingatia kuwa zaidi ya nusu mwaka umepita toka atoe ahadi ya kufuatilia Wizarani; wafanyakazi wa Urafiki na wananchi kwa ujumla wanachohitaji kuelezwa ni hatua zilizochukuliwa mpaka sasa.
Waziri ameshuhudia mwenyewe matumizi mabaya ya mali za Kiwanda cha Nguo cha Urafiki alipotembelea Kiwanda hicho tarehe 28 Mei 2012 kufuatia mwito niliompa mara baada ya kuteuliwa kwake na kufika katika Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kushughulikia udhaifu wa kiutendaji, ufisadi dhidi ya mali za kampuni, kulinda maslahi ya wafanyakazi na kushughulikia kasoro zilizojitokeza katika mchakato wa ubinafsishaji.
Aidha, Serikali iweke hadharani ripoti ya matumizi ya mkopo wa dola milioni 27 (takribani bilioni 40) ambazo zilitumika kununua mitambo chakavu kutokana na mianya ya ufisadi.
Spika wa Bunge Anna Makinda aeleze sababu za kutoruhusu mpaka sasa kuundwa kwa Kamati Ndogo ya Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara kuchunguza na kuchukua hatua kwa kuwa kuchelewa kufanya hivyo ni sawa na kuelea ufisadi na kukwamisha wabunge kutimiza wajibu wa kikatiba wa kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi.
Meneja Mkuu Msaidizi Nassoro Baraza na Meneja wa Utawala Moses Swai wawajibike kwa umma kueleza namna walishorikiana na vigogo wa Serikali na CCM katika kuwezesha matumizi mabaya ya mali za Kiwanda cha Nguo cha Urafiki na kuweka hadharani mikataba yote tata ya upangishaji wa maeneo pamoja na uuzaji kiholela wa mali za kampuni.
Kwa nyakati mbalimbali wafanyakazi wametoa madai ambayo menejimenti haijayatolea majibu kwa umma mathalani kuuzwa kinyemela kwa mashine za usokotaji namba mbili ambazo ziliuzwa kama chuma chakavu na hadi leo hii hakuna mashine zilizowekwa kama mbadala na hivyo kupunguza uzalishaji pamoja na ajira. (mashine nyingine zilizouzwa ni pamoja na Blowroom mashine 4, carding mashine 88, Drowing mashine 32,Roving mashine 16, na Ring frem mashine 50).
Matumizi mabaya ya mali za kampuni yamepanuka kwa kiwango cha Kiwanda kufanya shughuli zilizo nje ya kazi ya msingi ya ubia wa uzalishaji wa nguo ambazo ni kupangisha majengo. Baadhi ya nyumba na majengo hayo wamewahi kupangishwa na mengine wanaendelea kupangishwa viongozi wa Serikali na CCM au makampuni yao au washirika wao wa kibiashara kwa nyakati mbalimbali kwa kiwango cha kulea utamaduni wa kulindana.
Pamoja na upangishaji wa nyumba, matumizi hayo mabaya ya mali za Kiwanda cha Nguo cha Urafiki yanahusisha pia upangishaji holela wa maeneo ya wazi na maghala ya kiwanda, uuzaji wa nyumba za wafanyakazi, mfano mzuri ni nyumba 50 za THB eneo la Manzese, na ukodishaji wa maeneo kwa ajili ya kufanya biashara ya mafuta. Hali hii imeambatana na uingizaji wa bidhaa za nje kwa mgongo wa kampuni ya Urafiki na uzalishaji wa zingine za Wachina kinyemela kinyume na ubia wenye msingi wa kulinda na kuendeleza viwanda vya ndani hali ambayo imeleta athari katika uchumi wa taifa na kupunguza ajira za uzalishaji.
Hali hii inasababisha serikali kupoteza pato na mauzo yanayotokana na uzalishaji huo, pia wafanyakazi wamepunguzwa kutoka wafanya kazi 6,000 hadi wafanya kazi 650 katika siku za karibuni na hivyo kusababisha kushuka kwa mapato ya serikali na kuongezeka kwa matatizo ya ajira hususan kwa vijana.
Aidha mchakato wa kutafuta mwekezaji mpya uliofanyika unaohusu kampuni ya China iliyokuwa ikimiliki hisa asilimia 51 uligubikwa na usiri na utata, na mara baada ya mchakato huo ulianza mchakato mwingine wa kinyemela wa kutaka kuuza hisa asilimia 49 zinazomilikiwa na Serikali kwa niaba ya Watanzania.
Kama inavyofahamika, moja ya viwanda vikubwa vya nguo hapa nchini vilivyojengwa wakati wa Awamu ya Kwanza ya Utawala wa nchi yetu chini ya Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kiwanda cha Nguo cha Urafiki ambacho kilijengwa miaka michache baada ya uhuru kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka nchi ya China. Baadaye kiwanda kilibinafsishwa kiholela na sasa kinaendeshwa kwa ubia kuanzia mwaka 1997 ambapo serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 49 ya hisa huku asilimia 51 zikiwa chini ya kampuni ya nchini China.
Pamoja na kuwa mwenye hisa nyingi ndiye anawajibika zaidi katika uendeshaji wa kiwanda kiuendeshaji na maslahi ya wafanyakazi, serikali kwa kuwa na hisa 49% kwa niaba ya watanzania ina wajibu wa pekee wa kufuatilia kwa karibu hali ya kiwanda kama sehemu ya kulinda viwanda vya ndani, kudhibiti hasara kwa serikali na kuzuia upotevu wa mali za umma. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka kumi wajibu huu umekuwa hautekelezwi ipasavyo hali ambayo imedidimiza kiwanda kwa kiwango kikubwa na kuathiri uzalishaji pamoja na kupunguza ajira.
Katika mikutano ya tatu na nne ya Bunge kwa nyakati na njia mbalimbali nilizieleza pia Wizara na mamlaka mbalimbali za serikali kuwa hali mbaya ya kiwanda inahusisha pia kukosekana kwa udhibiti katika mali za kampuni na pia kiwanda kuanza kufanya shughuli ambazo ziko nje ya kazi ya msingi ya ubia wa uzalishaji wa nguo. Niliitaka serikali kuchunguza na kuchukua hatua juu ya shughuli zinazoendelea kufanywa na Kiwanda cha Nguo cha Urafiki nje ya mikataba na misingi ya ubia.
Kutokana na hali hiyo nilitoa mwito kwa Serikali kuingilia kati kupitia Wizara ya Fedha hususani Ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) na Wizara ya Viwanda na Biashara kuchukua hatua zinazostahili juu ya kiwanda cha Urafiki. Aidha, kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara kuchukua hatua za kuisimamia serikali ili kuharakisha hatua za kunusuru kiwanda hiki kama ili kuonyesha pia mfano wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhusu viwanda vingine. Hata hivyo, mpaka sasa hakuna hatua kamili zilizochukuliwa na Wizara na Mamlaka husika hali ambayo imefanya aendelee kutaka uwajibikaji wa serikali hata baada ya mabadiliko ya baraza la mawaziri.
Matatizo ya kiwanda cha urafiki ni zaidi ya changamoto za kawaida kwa kuwa ni matokeo ya kasoro katika mchakato mzima wa ubinafsishaji, udhaifu wa kiutendaji wa miaka mingi pamoja na ufisadi uliokithiri unaohitaji uchunguzi maalum.
John Mnyika (Mb)
21 Januari 2013

0 comments:

Post a Comment