MIAKA 11 TANGU KIFO CHA BABA WA TAIFA, ALIYOYACHUKIA NDIYO TUNAYOYATENDA
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kesho kutwa, Watanzania wataadhimisha miaka kumi na moja tangu kifo cha muasisi wa Taifa, hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyetutoka Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph, jijini London. Wakati huu tunapoadhimisha miaka 11 tangu Mwalimu alipotutoka, nchi yetu ipo kwenye vuguvugu kubwa la kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge hapo Oktoba 31, siku 17 tu baada ya maadhimisho hayo.
Katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu tumeshuhudia ahadi nyingi tamu kweli kweli kutoka kwa wagombea, huku kila mmoja akiwasilisha kwa namna alivyoweza. Mimi sina haja ya kurudia au kunukuu ahadi hizo.
Lakini mimi kama mwananchi wa kawaida nawakumbusha wagombea na wananchi kwa ujumla kwamba, Baba wa Taifa tunayemuenzi hakuwa muongo aliyejaa hadaa za kujipatia uongozi kama baadhi ya wagombea wetu wanavyojinadi sasa kwa kutumia ahadi ambazo hazihitaji elimu kubwa kuzitambua kuwa zina uongo ndani yake.
Wito wangu kwa wananchi ni kwamba tunapaswa kuwachagua viongozi ambao watayachukia kwa dhati mambo ambayo Baba wa Taifa aliyapinga na kuyakemea vikali enzi za uhai wake. Mfano wa mambo hayo ni Rushwa, ukabila, udini, ubaguzi na matumizi mabaya ya madaraka.
Ni vema tukatambua kuwa, mahali tulipofikia sasa pana harufu ya yale ambayo yalikuwa yakimtia ukakasi Baba wa Taifa, macho na masikio yetu yamesikia na kuona jinsi tunavyotumikia chini chini yale tuliyokatazwa na mwalimu.
Hebu tujisahihishe kwa kujiuliza, Je, tunayoyashuhudia kwenye siasa zetu bila kujali vyama vyetu ndiyo aliyoyasimamia mwalimu au tumekengeuka kwa kila mmoja wetu kuweka kando maslahi ya taifa na kuendekeza faida binafsi?
Kama nilivyosema huu ni mwaka wa 11 tangu tuachiwe wosia wa kuhakikisha kila mtanzania anapiga kufa na kupona kushindana na maadui watatu wa nchi yetu ambao ni Ujinga, Umaskini na Maradhi. Naamini hii ndiyo dira sahihi ya viongozi wetu na wananchi wote kwa ujumla.
Ni imani yangu kwamba, hamasa ya viongozi wetu ndani na nje ya vyama vya siasa itakuwa ni kuwasaidia watanzania kupambana na hatimaye kuwashinda maadui hao watatu haraka ili taifa letu liweze kupambana na changamoto za ulimwengu wa sayansi na teknolojia.
Nikisema hivyo sitarajii kuona siasa za makundi, visasi, ukabila, udini na hata ukanda zikipewa nafasi kwenye nchi yetu kwa sababu haziwezi kutusaidia kwenye harakati zetu za kujikomboa kiuchumi. Bila shaka hili si jambo jipya lilishasemwa na baba wa taifa miaka mingi iliyopita.
Mwalimu Nyerere katika uongozi wake hakuwahi kujifikiria mwenyewe na familia yake, bali furaha na nia yake siku zote ilikuwa ni kwa watanzania wote. Naweza kumsemea bila woga kwamba moyo wake ulikuwa umeandikwa, ‘Tanzania kwanza mimi na familia yangu tumo ndani yake’.
Maandishi haya natamani yaandikwe ndani ya kila moyo wa Mtanzania, ili uzalendo wa nchi yetu utukuzwe zaidi ya maslahi binafsi. Naamini kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kikiambatana na andiko hili mioyoni mwetu siasa haziwezi kutugawa wala kutugombanisha.
Nabii Yesu katika sala yake alisema: “Mapenzi yako yatimizwe,” akimaanisha mapenzi ya Mungu aliyemtuma yatangulie mbele na yale aliyotaka yeye yabaki kuwa ziada.
Alama hii ya unyenyekevu kwa Mungu wake ilimpa uvumilivu hata mahali alipoonewa na watu ambao alikuwa na uwezo wa kuwadhuru kwa uwezo wake wa kimungu.
Jambo la kujiuliza ni wangapi kati yetu ambao tunakwenda kuadhimisha miaka 11 tangu kifo cha Mwalimu huku mioyoni mwetu tukiwa na maadishi yanayosomeka “Mapenzi ya Tanzania Yatimizwe?”
Naangalia kushoto na kulia kwangu kuona ni mikono mingapi ya viongozi na wanasiasa wetu wa leo ambao toka ndani ya nafsi zao wana alama ya uzalendo kwa taifa. Wakati nasubiri hilo najiona ni mwenye jukumu pia hivyo natangulia kuinua mkono wangu.
Nafanya hivyo kama ishara ya kuueleza umma kwamba moyoni mwangu nchi yangu itakuwa mbele ya maslahi yangu binafsi yatabaki kuwa kitu cha ziada. Watanzania wengine walio tayari kuthibitisha uzalendo wao tuungane kumuenzi Mwalimu wa kweli toka ndani ya mioyo yetu.
Nimalize kwa kuwakumbusha wazalendo wenzangu kwamba vita yetu dhidi ya Umaskini, Ujinga na Maradhi, ingali mbichi, mambo ya siasa yasitupoteze lengo tukashindwa kusonga mbele.
Napasua Jipu kwa kusema nawapenda Watanzania wenzangu! Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.
HABARI NA http://www.globalpublishers.info/
0 comments:
Post a Comment