Mashabiki wawalaki Black Stars Ghana
Timu ya soka ya taifa ya Ghana
imerejea nyumbani kutoka kwenye Kombe la Dunia Afrika Kusini ikiwa
imekaribishwa na mashabiki wenye furaha kupita kiasi.
Maelfu ya mashabiki waliokuwa wakiimba na
kucheza waliwakaribisha wachezaji hao-wanaojulikana kama Black
Stars-kwenye uwanja wa ndege wa Accra.
Naibu waziri wa michezo Nii Nortey Duah
amewaambia wachezaji, " Mmeipeperusha bendera ya Ghana ipasavyo na pia
bara zima la Afrika."
Ghana, timu pekee kutoka Afrika iliyovuka hatua
ya makundi lakini ikang'olewa na Uruguay kwenye robo fainali katika
mechi iliyokuwa na utata wa aina yake.
Ni mara ya kwanza kwa Kombe la Dunia kufanyika
barani Afrika, na wengi walikuwa na matumaini timu moja kutoka barani
humo ingefika nusu fainali.
Ghana walitoka sare ya 1-1 na Uruguay katika
muda wa kawaida, lakini sekunde za mwisho za muda wa nyongeza Asamoah
Gyan alipokosa penati baada ya Luis Suarez wa Uruguay kuzuia kwa mikono
mpira uliokuwa unaingia golini.
Black Stars walijikuta wakitolewa kwenye
michuano hiyo baada ya Gyan kukosa penati hiyo kisha zilipopigwa penati
tano tano, Ghana walipoteza mbili dhidi ya Uruguay waliokosa moja.
Kulikuwa na vilio vya furaha katika uwanja wa
ndege wa Accra wakati ndege ya wachezaji wa Black Stars walipotua siku
ya Jumatatu jioni.
Mashabiki wa mpira, wengi ambao waliwasili saa
kadhaa kabla ya timu hiyo kufika, walipunga bendera za taifa za Ghana na
kupuliza vuvuzela kuwalaki mashujaa wao.
Nahodha wa Ghana, Stephen Appiah alisema:
"Tumejitahidi kwa kadri ya uwezo wetu lakini hatukuwa na bahati, hata
hivyo tutakwenda Brazil mwaka 2014 na tutakuwa washindani wakuu."
Awali Rais John Evans Mills aliwasihi Waghana
kutowabughudhi wachezaji licha ya kukatishwa tamaa na kushindwa kwao.
Amesema, " Ni bora tuendelee kuwaunga mkono na
tuwaonyeshe kuwa tumeshukuru kwa hatua waliyofika."
" Katika mechi ya Ijumaa, kulikuwa kuwepo
mshindi mmoja tu na kwa bahati mbaya, haikuwa Black Stars."
" Ndoto zatimia"
Siku ya Jumapili, watu walijikusanya
kuishangilia timu ya Ghana walipokuwa wakifanya ziara mjini
Johannesburg.
Awali Jumamosi, timu hiyo ilikutana na aliyekuwa
mke wake Nelson Mandela, Winnie Madikizela-Mandela mjini Soweto, kabla
ya kumtembelea Bw Mandela nyumbani kwake mjini Johannesburg.
"Ni bora tuendelee kuwaunga mkono na
tuwaonyeshe kuwa tumeshukuru kwa hatua waliyofika" Rais wa Ghana, John
Evans Mills
Baada ya kukutana kwao, ofisi ya Bw Mandela
ilisema, " Waliwakilisha bara la Afrika vilivyo na licha ya kutofuzu kwa
nusu fainali wanaweza kurejea nyumbani kwa kujiamini."
Golikipa Richard Kingson alisema, " Nimefurahi
kukutana na mtu muhimu kama Rais Mandela. Nilikuwa naye, nikimshika
mkono, Nimefurahi sana kukutana naye uso kwa uso."
Kevin-Prince Boateng alisema: " Ni ndoto
iliyotimia. Ni jambo zuri sana kwetu. Tumefurahi sana kukutana na mtu
huyu. Ni mtu mashuhuri." BBC SWAHILI.
0 comments:
Post a Comment