Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja
wa Mataifa limetaka kuanzishwa uchunguzi huru kufuatia shambulio kwenye
meli za kibinadamu zilizokuwa njiani kupeleka misaada katika ukanda wa
Gaza.
Taarifa ya Baraza la Umoja wa Mataifa imetokea
baada ya mashauriano yaliyochukua usiku kucha. Takriban wanaharakati 10
waliuawa wakati wanajeshi wa Israel walipoingia ndani ya meli hizo
kwenye mipaka ya kimataifa.
Taarifa hiyo imeafikiwa kati ya Uturuki na
Marekani, huku Uturuki ikisisitiza laana kali dhidi ya Israel nayo
Marekani ikaamua kutotoa maneno makali kwa mshirika wake huyo wa
karibu.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani
matukio yote yaliyosababisha vifo vya watu 10 na wengine wengi
kujeruhiwa pamoja na kufariji familia za waathirika.
Aidha baraza hilo limetaka meli hizo ambazo
zinazuiliwa mwambao wa Israel kuachiliwa mara moja. Punde baada ya
taarifa hizo kutolewa wapiganaji kadhaa wa Kipalestina walivuka mpaka na
kuingia upande wa Israel ambapo walikabiliana na wanajeshi huku wawili
wakiuawa.
Kwa upande wake mwakilishi wa Israel katika
Umoja wa Mataifa amesema wanajeshi wake walikuwa wakijikinga kutoka
mashambulio ya wanaharakati hao.
Israel yakemewa kwa kushambulia meli za Gaza
BBC Swahili.
Serikali ya Uturuki imelaani
Israel katika mkutano wa dharura wa baraza la usalama la umoja wa
mataifa kwa kushambulia meli zilizokuwa zinapeleka chakula cha msaada
katika ukanda wa Gaza hapo jana.
Takriban wanaharakati tisa wa Palestina waliuawa
baadhi wakiwa raia wa Uturuki, wakati Israel ilipovamia meli hizo
zikiwa baharini.
Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa nchi
hiyo Ahmet Davutoglu, serikali ya Israel imefanya mauaji na ameitaka
iombe radhi kwa kosa hilo, kuwachia meli hizo na kuwalipa fidia
wanaharakati wa kipalestina.
Waakilishi wa Israel kwenye mkutano huo wamesema
kuwa hatua ya wanajeshi wao ilikuwa ya kujilinda kutokana na tisho la
uvamizi.
Wakati huo huo, waziri wa ulinzi wa Israel,
Ehud Barack,ameelezea alitumai jamii ya kimataifa ingeelewa tisho la
usalama inalokabiliwa nalo kutoka kwa kundi la wapiganaji la hamas.
Lakini Hamas wanasema kuwa Israel haiwezi
kuendelea kudhalilisha wapalestina kwa kisingingizo cha usalama.
0 comments:
Post a Comment