SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, May 7, 2010

Uwekezaji unufaishe wananchi-Tibaijuka

Wataka mkutano wa WEF utumike kuitangaza Afrika

Na Tumani Makene
NCHI za Afrika zimetakiwa kuwa macho na wawekezaji kutoka nje bila kujali sehemu wanayotoka na kuhakikisha rasrimali zinazohusika katika uwekezaji zinawanufaisha wananchi wenyeji kwanza.

Ili mataifa hayo na wananchi wake kwa ujumla waweze kunufaika ni muhimu serikali zikahahakisha uwepo wa ulali ulio sawa wa faida inayotokana na uwekezaji unaofanyika katika nyanja mbalimbali.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam mmoja wa Wenyeviti Wenza wa Mkutano wa Uchumi wa Dunia (WEF) kwa Afrika, Profesa Anna Tibaijuka alipoulizwa na waandishi wa habari hali ya uwekezaji kwa sasa ambapo China inaonekana kuja juu na kutishia kuzipiku nchi za magharibi.
Prof. Tibaijuka pamoja na wenyeviti wenza wengine wa WEF walikuwa wakizungumza na waandishi wa habari juu ya matarajio yao kwa mkutano huo ulioanza jana na masuala mengine mbalimbali ya kimataifa na kitaifa.
Prof. Tibaijuka ambaye ni mmoja wa Watanzania wenye nyadhifa kubwa kimataifa, akiwa ni Mkurugenzi wa Shirika la Makazi Duniani (UN-HABITAT), alisema kuwa suala la ulali ulio sawa wa faida ni muhimu kuzingatiwa katika wakati huu ambapo wawekezaji wanapigana vikumbo kutafuta maeneo ya kuwekeza.
"Ni kweli China kwa sasa inakuja juu katika masuala ya uwekezaji, lakini mimi ninachosema ni lazima tuwe macho na wawekezaji hawa, awe nani au nani, bila kujali wanakotoka lazima sisi tufikirie tunapata nini, lazima kuwepo na balance situation (ulali sawa) katika masuala haya, win-win situation (kila upande unufaike) baina yetu na wawekezaji lazima izingatiwe.
"Ni kweli wanapaswa kupata faida lakini pia lazima sisi tujinufaishe katika uwekezaji, inawezekana wao wakawa hawana matatizo lakini tukawa na matatizo yanayokwaza kupata hiyo faida kama vile miundombinu mibovu, sera na mazingira mengine...tuwashirikishe wageni sawa lakini kwa manufaa ya watu wetu," alisema Prof. Tibaijuka.
Akizungumzia umuhimu wa reli katika maendeleo ya nchi maskini kama Tanzania, alisema ni vigumu kufanikisha suala la kilimo bila kuwa na miundombinu madhubuti ya usafiri wa reli.
Alitoa mfano kuwa TAZARA ni reli pekee ambayo ilijengwa baada ya nchi za Afrika kupata uhuru, hali ambayo inaziweka katika mazingira magumu nchi hizo kushindana kibiashara, kwani njia nyingine za uchukuzi ni ghali, hivyo kuongeza ughali wa bidhaa pia.
Katika hatua nyingine, Wenyeviti wa Wenza wa WEF walisema mkutano huo unapaswa kuwa fursa ya pekee kwa nchi za Afrika hususani mwenyeji wake Tanzania, kujitangaza na kunufaika kutoka kwa wawekezaji wakubwa wa kimataifa.
Profesa Anna Tibaijuka alisema kuwa huu wakati mwafaka kwa Nchi za Bara la Afrika kutumia fursa ya mkutano huu kujitangaza ili kunufaika na uwekezaji kwenye maeneo muhimu kama ujenzi wa miundombinu, badala ya kubaki 'kulia lia' juu ya changamoto zinazokabiliana nazo katika kuziendeleza nchi zao na wananchi kwa ujumla.
"Huu ni wakati wa kuionesha dunia kuwa Afrika ni bara ambalo liko katika mwendo au muda wa mpito kuelekea katika maendeleo, lakini pia nategemea mkutano huu utazungumzia kwa kina na kutoa suluhisho juu ya tatizo kubwa ambalo sasa linaikabili Afrika na dunia kwa ujumla, tatizo la makazi duniani. Kwa sasa dunia inakabiliwa na wimbi kubwa la uhamaji wa watu kutoka vijijini kwenda mjini.
"Kama hali hiyo haitatafutiwa ufumbuzi, basi amani na utulivu wa dunia utakuwa mashakani kwa sababu huko wanakokimbilia hakujaandaliwa vizuri, watahitaji huduma za jamii kama vile elimu, maji, na nyingine nyingi, asilimia kubwa ya wananchi wanaoishi mjini kwa sasa hawana huduma hizo muhimu, mbaya kabisa maisha wanayoishi si ya ubinadamu, hii ni hatari," alisema Prof. Tibaijuka.
Alisisitiza kuwa lazima Afrika iwekeze katika maendeleo ya jamii, kwa ajili ya manufaa ya Waafrika, huku akionya kuwa kama suala la makazi halitapewa kipaumbele kimataifa kama katika mkutano wa WEF basi linaweza kuwa janga la pili baada ya Ugonjwa wa Ukimwi.
Kwa upande wake Ajai Chowdhry kutoka India alisema kuwa nchi za Afrika zinaweza kujifunza kutoka nchi yake ambayo miaka ya 90 ilikuwa katika mgogoro mkubwa wa fedha kiasi cha kutishia uchumi wake, lakini waliamua kuwekeza katika teknolojia na taasisi za fedha, ambapo wananchi walikuwa wanaweza kupata huduma hizo mpaka vijijini.
Naye Pat Devies kutoka Afrika ya Kusini alisema kuwa Waafrika wanapaswa kuwa na mitazamo chanya juu ya kufikia mafanikio ya uchumi katika nchi zao, huku wakifikiria kwa makini vikwazo ambavyo vimekuwa vikizuia maendeleo hasa katika nyanja ya biashara kwa bara hilo la kwa muda mrefu sasa. "Afrika inapaswa kuboresha maisha a watu wake sasa," alisema.
Bw. Joergen Ole Haslestad kutoka Norway akionekana kufurahishwa na hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuweka mkakati wa Kilimo Kwanza kuinua kilimo nchini, alisema kuwa Tanzania na Afrika kwa ujumla inapiga hatua kuelekea maendeleo.
Naye Bw. Kuseni Douglas Dlamini kutoka Afrika Kusini alisema kuwa sasa ni wakati wa Afrika kufungua minyororo ambayo imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya nchi moja moja na bara zima kufikiwa. 

0 comments:

Post a Comment