UJENZI wa barabara mbili za juu (fly-over) ili kupunguza foleni katika
Jiji la Dar es Salaam utaanza baadaye mwaka huu baada ya taasisi za
fedha za kimataifa kukubali kutoa fedha kugharamia mradi huo.
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Adam Kimbisa aliyasema hayo Dar es
Salaam alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Kumepambazuka
kinachorushwa na televisheni ya ITV, jana asubuhi.
Alisema Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
wamekubali kutoa fedha za kugharamia ujenzi wa barabara hizo na tayari
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imewasilisha bajeti ya ujenzi wa
barabara hizo katika maeneo ya Ubungo na Tazara.
“Hatua hii imekuja baada ya Jumatatu iliyopita Jiji kuandaa mkutano
mkubwa wa kimataifa wa kuzungumzia changamoto zinazolikabili Jiji la
Dar es Salaam ambapo viongozi wa mashirika haya ya fedha walihudhuria,”
alisema Kimbisa.
Alisema ingawa ujenzi utaanza mwaka huu lakini utakamilika ndani ya
kipindi cha miaka miwili au miwili na nusu, hatua itakayosaidia kwa
kiasi kikubwa kupunguza foleni katika barabara kubwa nne za Nyerere,
Morogoro, Kilwa na Bagamoyo.
“Barabara hizi nne ndizo zinazotumika kuwaleta watu mjini asubuhi
na kuwarejesha nyumbani jioni. Kwa ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam hivi
sasa barabara hizi hazitoshelezi na tumeona ni lazima tuanze kuchukua
hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo hili kwa kujenga barabara za
pembeni ili kusaidia,” alisema Kimbisa.
Alisema serikali imeamua kujenga barabara hizo mbili kwanza
kutokana na unyeti na ulazima wa kuwa na barabara za juu katika maeneo
hayo ya Ubungo na Tazara.
Alisema unyeti wa eneo la Ubungo unatokana na barabara ya Morogoro
kutumika na magari yote yanayotoka mikoani na nchi jirani kuja Dar es
Salaam na Tazara kunatokana na barabara ya Nyerere kutumiwa na watu
wengi wakiwemo wanaosafiri kwenda au kutoka nje ya nchi kupitia Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema Jiji pia limeainisha baadhi ya barabara za pembeni
zitakazosaidia kupunguza foleni katika barabara hizo kuu nne za
Nyerere, Morogoro, Bagamoyo na Kilwa.
Katika hatua nyingine Kimbisa alisifu ukarimu uliooneshwa na wakazi
wa Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Kiuchumi wa Dunia (WEF),
uliofanyika kwa siku tatu kuanzia Mei 5 hadi Mei 7, mwaka huu.
Imeandikwa na Na Oscar Mbuza.
Sunday, May 9, 2010
Barabara za juu Dar es Salaam sasa mwaka huu
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Sunday, May 09, 2010
Email This
BlogThis!
Share to Twitter
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment