SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, June 17, 2014

UDA YASISITIZA NIA YAKE YA KUBORESHA USAFIRI JIJINI DAR ES SALAAM

 Sehemu ya Mabasi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA
Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Robert Kisena, alipokua akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa makabidhiano ya sehemu ya kwanza ya magari 175 kati ya magari 1000 yaliyonunuliwa na Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), kutoka Kampuni ya Eicher ya India, Makao Makuu ya shirika hilo, jijini February 9, 2014
---
 
Na Mwandishi Wetu,
KAMPUNI ya Simon Group Limited imesisitiza dhamira yake ya kuboresha sekta ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam licha ya kampeni zinazoendelea kutoka kwa washindani binafsi ikiwa na lengo la kuvuruga mpango unaoendelea wa uwezekezaji katika Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) ili waweze kuitawala biashara ya usafiri.

Kwa mujibu wa taarifa ya UDA, mpango unaendelea wa kuifanya Dar es Salaam liwe jiji lenye urahisi katika usafiri kwa kufanya kazi kwa karibu na Serikali na Jiji.

“Tumeona taarifa ambazo zimekuwa zikichapishwa katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii kutoka katika kundi linalojiita Consortium of Concerned Tanzanians International wakijaribu kuwafanya watu waamini kila uwekezaji unaofanywa katika kuboresha mfumo wa usafiri jijini Dar es Salaam kupitia UDA hauna maana.

“Hili ni hatua inayosikitisha sana, tunajaribu kuuboresha mfumo wa usafiri Dar es Salaam kutoka katika msongamano ili kuwa katika hali inayoridhisha kwa kuongeza idadi ya magari na kuboresha huduma za usafirishaji lakini watu wengine wanatumia muda mwingi kufanya kampeni zenye lengo la kuhakikisha malengo hayo hayatimii,’’ ilisema taarifa hiyo kutoka kwa mwenyekiti ambaye pia ndiye Ofisa Mtendaji Mkuu, Robert Kisena.

Aliitaja kampeni hiyo iliyopewa jina la “Kampeni ya Kurudisha Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) Mikononi mwa wananchi” inajaribu kuligeuza mtaji suala la kujivunia umiliki wa kampuni hiyo kwa umma bila ya kuangalia ni vipi kampuni inaweza kusimamiwa kwa namna bora na kufanikiwa kutimiza malengo ya kurahisisha usafiri Dar es Salaam.

Alisema kwamba kampuni yake iliamua kuwekeza UDA baada ya kutangazwa kubinafsishwa kwake kwa sababu kampuni ya Simon Group Limited ilitaka kuleta mabadiliko yenye maana katika mfumo wa usafiri katika Jiji la Biashara la Dar es Salaam hasa katika mabasi ya abiria na usafirishaji kwa ujumla.

“Mpango wa kuboresha usafiri umeelezwa vizuri katika mipango yetu ya muda mfupi na muda mrefu inayoonyesha ni jinsi gani tuna mpango wa kusimamia mabadiliko haya hatua kwa hatua. Katika mpango wetu pia tumebainisha ni vipi tunajipanga kuihusisha Serikali na Jiji katika mpango mzima wa usafiri Dar es Salaam. Naamini hii ndio maana hasa ya uzalendo, kufanya kazi na serikali yako ili kutoa huduma bora kwa wananchi wake,’’ alieleza Kisena katika taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo ofisa huyo mtendaji mkuu alibainisha kwamba mpango walioudhamiria wa kampuni hiyo kuboresha huduma ya usafiri Dar es Salaam uko pale pale ukihusisha mradi wa kuwa na mabasi zaidi ya 3,000 pamoja na mabasi mengine ya kifahari 50 yenye viyoyozi na huduma ya internet.

Alisema kwamba sambamba na mpango huo, kampuni itasimamia sera ya kuwaajiri wataalamu wazawa badala ya kuwapa wataalamu wa kigeni kazi ambazo Watanzania wanazimudu.

“Kampuni ya Simon Group Limited inamilikiwa na Watanzania, katika hilo nitakuwa mtu wa mwisho kumkubali mtaalamu wa kigeni kuajiriwa  katika nafasi ambayo inaweza kushikwa na Watanzania wenzangu. Kama hatutopata mtaalamu Mtanzania, tutaleta wataalamu wa kuwapa mafunzo Watanzania ili baadaye wazichukue nafasi hizo. Kampuni yetu inalifanya hilo kama njia mojawapo ya kuwawezesha wazawa kiuchumi na kuwapa utaalamu.

Alisema kwamba tathmini inaonyesha kuwa ili kuwezesha mabasi yapatayo 3000 kufanya kazi hapo baadaye wataalamu wapatao 7800 watahitaji kupewa mafunzo na kuajiriwa.

Aliongeza kwamba mara baada ya mpango huo kukamilika, unyanyapaa miongoni mwa wanajamii kuhusu utumiaji wa mabasi ya uma hautokuwepo tena na watu wataacha kupaki magari yao katikati ya jiji, watanunua tiketi za UDA kwa njia ya mtandao jambo ambalo litapunguza msongamano Dar es Salaam.

“Ninataka kuwahakikishia Watanzania wote na wale wanaoendelea na kampeni zao kwamba mpango wa UDA kuboresha mfumo wa usafiri Dar es Salaam ni jambo linalowezekana, Tutafanya kazi kwa karibu na Serikali pamoja na Jiji ili kuona wakazi wa Dar es Salaam wanapata huduma rahisi na ya uhakika ya usafiri,’’ alisema