Meneja wa kituo cha Sengerema FM Redio, Ndg. Felician Ncheye, akitoa nasaha za ukaribisho kwa washiriki wa mradi wa SHUGA na mgeni rasmi. Katikati ni Mgeni rasmi Mratibu wa UKIMWI halmashauri ya Sengerema mkoa wa Mwanza kupitia mradi wa TACAIDS, Ndg. Geofrey Mabu na Kulia ni Afisa Mipango VVU/UKIMWI UNESCO, Ndg. Herman Mathias.Picha zote na Zainul Mzige.
**************************************
Na Mwandishi wetu, SENGEREMA - MWANZA
Redio za jamii nchini zimeaswa kutumika vizuri katika kuelimisha kamii juu ya kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kupitia vipindi vya redio.
Hamasa hiyo imetolewa na Ndg Geofrey Mabu ambaye ni mratibu wa UKIMWI halmashauri ya Sengerema mkoa wa Mwanza kupitia mradi wa TACAIDS wakati akifungua warsha ya siku tatu ya mradi mpya ujulikanao kama SHUGA, unaotekelezwa na shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana Shirika la Mfuko wa Watoto (UNICEF) inayofanyika katika kituo cha Redio Jamii Sengerema mkoani Mwanza.
Mabu amesema kuwa mradi huo umekuja wakati muafaka ambapo malengo yake yakizingatiwa na kutekelezwa kama ilivyopangwa utasaidia kufikia malengo ya serikali ya kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI hadi Zero.
Mgeni rasmi Mratibu wa UKIMWI halmashauri ya Sengerema mkoa wa Mwanza kupitia mradi wa TACAIDS, Ndg. Geofrey Mabu akifungua warsha ya siku tatu ya mradi mpya kuhamasisha Vijana kuhusu udhibiti wa Maambukizi mapya ya VVU ujulikanao kama SHUGA.
Amesema kuwa redio za jamii ni kiungo muhimu katika kuelimisha jamii na kuwa kama zitatumika vizuri kusambaza elimu ya UKIMWI kupitia vipindi vyake zitasaidia kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali kupitia TACAIDS.
Vile vile ameziomba redio zitakazoshiriki katika mradi huu, kutumia vizuri fursa hii waliyoipata kuhakikisha wanafanikisha malengo ya mradi kwa kiwango cha juu kwa kufanya hivyo pia watakuwa wamelinusuru taifa na janga hili la UKIMWI.
Mshauri na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu akitoa maelezo kuhusu madhumuni ya warsha inayohusisha mradi wa SHUGA.
Awali Mkufunzi wa Radio za jamii kutoka shirika la UNESCO Bi Rose Mwalimu akitoa ufafanuzi wa malengo ya semina hiyo, amesema kuwa mradi huu wa SHUGA unalenga kupambana na maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI kwa vijana hapa nchini kupitia vipindi vya mchezo wa redio kubadili tabia.
Amezitaja redio 10 zinazoshiriki katika mradi huu nchini Tanzania kuwa ni FADECO Redio ya Karagwe mkoani Kagera, ORS ya Manyara, Sengerema FM mkoani Mwanza, Pangani FM ya mkoani Tanga na Kahama FM kutoka Shinyanga.
Nyingine ni Kitulo FM ya Makete Njombe, Kyela FM ya Mbeya, Nuru FM kutoka Iringa, Pambazuko FM Ifakara na Kwanza Jamii Redio FM kutoka Njombe.
Afisa Mipango VVU/UKIMWI UNESCO, Ndg. Herman Mathias akitoa mada kuhusu VIjana, Balehe na Mahusiano ya Ngono wakati warsha ya siku tatu ya mradi mpya kuhamasisha Vijana kuhusu udhibiti wa Maambukizi mapya ya VVU ujulikanao kama SHUGA.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia kwa umakini mada zilizokuwa zikitolewa na wakufunzi.
Mshiriki kutoka Kahama FM Redio, Makunga Peter akiuliza jambo kutoka kwa mkufunzi (hayuko pichani).
Afisa Mipango VVU/UKIMWI kutoka UNICEF, Bi. Alice Ijumbe akitoa mada kuhusu kiwango cha Maambukizi ya VVU kwa Vijana na hali ya Afya ya Uzazi Salama wakati wa mafunzo hayo.
Mshiriki wa warsha ya siku tatu ya mradi mpya kuhamasisha Vijana kuhusu udhibiti wa Maambukizi mapya ya VVU ujulikanao kama SHUGA kutoka Sengerema FM Redio, Peter Marlesa akijenga hoja kuhusu viashiria hatarishi vya maambukizi ya VVU kwa vijana.
Pichani juu na chini washiriki wa warsha ya siku tatu ya mradi wa SHUGA wakiwa katika vikundi kazi.
Mgeni rasmi Ndg Geofrey Mabu wa TACAIDS, wakufunzi wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa warsha ya siku tatu ya mradi mpya kuhamasisha Vijana kuhusu udhibiti wa Maambukizi mapya ya VVU ujulikanao kama SHUGA.