SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Sunday, March 23, 2014

.. NA JULIUS NAYE KAIANZISHA NGOMA, KATUACHIA TUICHEZE...!

Ndugu,
Siku zote nakumbusha, kuwa historia ni mwalimu mzuri. Katika kujitahidi kwangu kuyaelewa haya yanayotokea sasa kuhusiana na Katiba na hotuba za waheshimiwa zenye kukinzana,
basi, nimeingia kwenye maktaba yangu kuyapitia maandiko mbali mbali.
Ni kuanzia ' Nyerere of Tanzania' kilichoandikwa na William Edgett Smith hadi ' Kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi' kilichoandikwa na Ali. A. Mohammed.
Katika Kuyachambua maandiko haya, kuna mahali nimekutana na hoja moja ya msingi sana kuhusiana na nini tunataka kama nchi. Ninaposoma maandiko haya ya kihistoria nabaini kuwa, katika mahusiano ya vyama na watu wa visiwani na bara, malengo ya wazee wetu na waasisi wa vyama vya ASP na TANU yalikuwa kufikia 'Muungano Kamili'. Na wamesema hayo hadharani kwa midomo yao.
Sasa, unaposikia leo kuwa yanatamkwa malengo ya kufikia' Mamlaka Kamili' ni lazima imuumize kichwa kila mwenye kufikiri kwa akili zake, na si za kuazima. Na inapohusu ' Mamlaka Kamili' kwenye nchi moja inayounda muungano wa nchi mbili uliozaa nchi moja ni lazima ionekane ajabu.
Na turudi nyuma basi kupitia maandiko. Turudi asubuhi ya Septemba 22, 1975. Kwa mujibu wa mwandishi Ali. A . Mohammed ( Kitabu cha Kuzaliwa kwa CCM), siku hiyo ilikuwa na upepo wa kiasi na baridi ya kiasi. Ni kwenye jiji la Dar es Salaam. Wajumbe wa TANU na ASP walikutana kumpendekeza mgombea wao wa Urais kwa uchaguzi wa Oktoba 26, 1975.
Na pendekezo lilikuwa la jina moja tu, lilitolewa na Aboud Jumbe,Rais wa ASP. Baada ya Aboud Jumbe kulitamka jina la Julius Nyerere, ukumbi ukalipuka kwa shangwe,... Nyerere , Nyerere, Nyerere...! Shangwe zilizodumu kwa dakika kumi nzima. Katika dakika hizo kumi hakuna kingine kilichofanyika wala kusikika isipokuwa kelele za shangwe tu. Hakukuwa tena na haja ya kutafuta uthibitisho wa jina hilo kwa kuwauliza wajumbe. Mkutano mzima ulimkubali Nyerere, anaandika Ali Mohammed.
Na Mwalimu Nyerere alipomaliza kuwashukuru wajumbe, akaja na habari iliyowashtua wajumbe. Alisema;
" Kwa mujibu wa Katiba yetu, nchi yetu ni nchi ya Chama kimoja. Ila, kwa sababu tunavyo vyama viwili, Katiba inapozungumzia juu ya Chama kimoja inachozungumzia kwa kweli ni Vyama viwili. Mimi naamini kuwa hii dosari katika Katiba yetu na si dosari ndogo. Sina idhini ya TANU wala ASP kwa kusema haya ninayoyasema. LAKINI NAAMINI KABISA KWAMBA SASA WAKATI UMEFIKA WA KUFIKIRIA JINSI YA KUONDOA DOSARI HILI." Julius Nyerere.
Naam, ndipo hapo Julius Nyerere alipokuja na pendekezo la kuunganisha vyama. Na lengo hasa ni kuelekea kwenye ' Muungano Kamili'. Julius Nyerere akawa ' ameianzisha ngoma'... Na hakika ametuachia tunaicheza mpaka sasa. Na ukiyapitia maandiko haya ya kihistoria, unaona chimbuko la mengine tunayoyashudia sasa...
Jumapili Njema.
Maggid Mjengwa,
Iringa.

0754 678 252.